Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hariri ya Buibui

Hariri ya Buibui

Je, Ni Kazi ya Ubuni?

Hariri ya Buibui

▪ Ingawa ni nyepesi kuliko pamba, hariri hiyo ni imara kuliko chuma. Kwa miaka mingi, wanasayansi wameichunguza hariri inayosokotwa na aina fulani ya buibui. Hariri ambayo buibui huyo anatumia kupanda na kushuka kwenye utando wake, imewavutia sana watu kwani ndiyo hariri ngumu zaidi kati ya hariri saba zinazosokotwa na buibui huyo. Hariri hiyo ni ngumu na haipenyi maji kama hariri inayotengenezwa na nondo wa hariri, ambayo mara nyingi hutumiwa kutengeneza vitambaa.

Fikiria hili: Nyuzi zinazotengenezwa viwandani kama vile Kevlar huhitaji joto jingi na hutumia kemikali za kuyeyushia. Kinyume na hilo, buibui husokota hariri katika joto la kawaida na kutumia maji kuyeyusha. Isitoshe, hariri ya buibui ni ngumu kuliko Kevlar. Utando uliofanyizwa kwa hariri hiyo ukipanuliwa uwe na ukubwa wa kiwanja cha mpira unaweza kusimamisha ndege kubwa ya abiria ikiwa katika mwendo!

Haishangazi kwamba watafiti wanavutiwa sana na ugumu wa hariri hiyo. “Wanasayansi wangependa kuchunguza hariri hiyo kwa undani ili waweze kuitumia kutengeneza mavazi yasiyopenya risasi na nyaya za kushikilia madaraja,” anaandika Aimee Cunningham katika gazeti Science News.

Lakini si rahisi kutengeneza kitu kama hariri hiyo kwani inatengenezwa ndani ya mwili wa buibui na wataalamu hawajaelewa kwa undani jinsi inavyotengenezwa. “Tunajihisi kuwa duni tunapotambua kwamba watu wengi wenye akili wanajaribu kutengeneza kitu ambacho buibui wanaoishi katika nyumba zetu hutengeneza kiasili,” anasema mwanabiolojia Cheryl Y. Hayashi, aliyenukuliwa katika gazeti Chemical & Engineering News.

Una maoni gani? Je, buibui na hariri yake iliyo ngumu kama chuma ilitokea yenyewe au ilibuniwa na Muumba mwenye akili?

[Picha katika ukurasa wa 24]

Picha ya darubini ya buibui akitoa hariri

[Picha zimeandalewa na]

Copyright Dennis Kunkel Microscopy, Inc.