Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ “Nchini Uingereza mtoto anapofikia umri wa miaka sita atakuwa ametazama televisheni kwa mwaka mmoja, na zaidi ya nusu ya watoto wenye umri wa miaka mitatu wana televisheni katika vyumba vyao.”—THE INDEPENDENT, UINGEREZA.
▪ Nchini China, asilimia 31.4 ya watu walio na umri wa zaidi ya miaka 16 waliohojiwa walisema kwamba ni wafuasi wa dini. Ikiwa idadi hiyo inawakilisha taifa lote, uchunguzi huo unaonyesha kwamba “karibu watu milioni 300 ni wafuasi wa dini . . . tofauti kabisa na idadi rasmi iliyotolewa ya watu milioni 100.”—CHINA DAILY, CHINA.
Madhara Ni Mengi Kuliko Faida
Miaka kadhaa iliyopita, wanasiasa na wanamazingira Waholanzi walifikiri kwamba wamepata suluhisho la tatizo la nishati, yaani, kutumia jenereta zinazoendeshwa kwa mafuta yanayotokana na mimea hasa mafuta ya mawese. Badala ya kusuluhisha tatizo wamesababisha “madhara makubwa kwa mazingira,” linasema gazeti The New York Times. “Uhitaji mkubwa wa mafuta ya mawese huko Ulaya ulisababisha ukataji wa misitu mikubwa ya mvua huko Kusini-Mashariki ya Asia na matumizi ya mbolea za kemikali kwa wingi.” Ili michikichi mingi iweze kupandwa, maeneo hayo yalilazimika kukaushwa maji na majani yaliyooza yalichomwa, na hivyo kusababisha gesi “nyingi sana” ya kaboni kuingia hewani. Kwa sababu hiyo, linasema gazeti Times, Indonesia imekuja kuwa “nchi ya tatu ulimwenguni inayotokeza gesi za kaboni kwa wingi zaidi, ambazo wanasayansi wanaamini zinaongeza kiwango cha joto ulimwenguni.”
“Saa ya Maangamizi” Yasogezwa Mbele
Saa ya maangamizi, iliyoanzishwa na wanasayansi wa kuchunguza mambo ya atomiki (Bulletin of Atomic Scientists) ili kuonyesha jinsi wanadamu wanavyokaribia msiba wa nyuklia, imesogezwa mbele kwa dakika mbili. Sasa saa hiyo inasema ni dakika tano kabla ya saa sita usiku, saa “inayosemekana kuwa mwisho wa ustaarabu.” Saa hiyo imesogezwa mara 18 tu katika historia yake ya miaka 60. Ilisogezwa mara ya mwisho mnamo Februari 2002, baada ya mashambulizi ya majengo ya World Trade Center huko New York. Kuendelea kutengenezwa na kuwepo kwa silaha za kinyuklia kutia ndani kukosa kuhifadhi vizuri vifaa vya kutengeneza nyuklia ni “dalili za kushindwa kutatua matatizo yanayosababishwa na teknolojia yenye uharibifu zaidi duniani,” inasema taarifa ya wanasayansi hao. Isitoshe, taarifa hiyo iliendelea kusema, “hatari zinazosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa ni mbaya kama zile zinazotokezwa na silaha za nyuklia.”
Mikazo Wakati wa Uja-Uzito
Kulingana uchunguzi wa karibuni, mfadhaiko ambao mama mjamzito hukabili kwa sababu ya mabishano au jeuri anayotendewa na mwenzi wa ndoa inaweza kuathiri vibaya sana afya ya kiakili ya mtoto. Profesa Vivette Glover, wa Chuo cha Imperial huko London, anasema hivi: “Tuligundua kwamba mwanamke akitendewa kwa jeuri na mwenzi wake anapokuwa mjamzito, ukuzi wa baadaye wa mtoto huathiriwa. Baba huchangia sana katika ukuzi huo.” Anaeleza kwamba uhusiano wa wazazi “unaathiri usawaziko wa kemikali na homoni katika mwili wa mama, jambo ambalo huathiri ubongo wa mtoto mchanga.”
Madereva Wanaoendesha Bila Kukaza Fikira
Madereva ambao wanatumia barabara ileile kila siku, mara nyingi hufanya hivyo bila kutumia sehemu ya ubongo ambayo huchochea kufikiri, anasema Michael Schreckenberg, mwanasayansi wa masuala ya barabara wa Chuo Kikuu cha Duisburg-Essen, Ujerumani. Wakiwa kwenye barabara wanazofahamu vizuri, madereva hao hufikiria mambo mengine badala ya kukaza fikira barabarani. Kwa sababu hiyo, inachukua muda mrefu zaidi kutambua hatari. Schreckenberg anawatia moyo madereva wanaotumia barabara ileile wakumbuke kuwa macho na wasikengeushwe.