Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Reli Iliyochukua Zaidi ya Miaka 120 Kujengwa

Reli Iliyochukua Zaidi ya Miaka 120 Kujengwa

Reli Iliyochukua Zaidi ya Miaka 120 Kujengwa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

FEBRUARI 3, 2004, gari-moshi lenye urefu wa zaidi ya kilomita moja liliingia kwa utaratibu kwenye Kituo cha Gari-Moshi cha Darwin katika Eneo la Kaskazini la Australia ambalo halina watu wengi. Maelfu ya watu walikusanyika ili kulishangilia. Gari-moshi hilo linaloitwa The Ghan, lilikuwa tu limemaliza safari yake ya kwanza ya kilomita 2,979 iliyochukua siku mbili kutoka kusini hadi kaskazini mwa bara hilo.—Ona sanduku “Chanzo cha Jina,” kwenye ukurasa wa 25.

Zaidi ya watu 2,000 waliokuwa na kamera walikusanyika kando ya reli, kwa hiyo gari-moshi lilihitaji kupunguza mwendo lilipokaribia jiji la Darwin. Hilo lilifanya lichelewe kwa dakika 30 hivi. Lakini hakuna mtu aliyelalamika. Tayari watu wa Australia walikuwa wamengojea tukio hilo kwa zaidi ya karne moja. Reli hiyo kutoka Adelaide hadi Darwin, inayopitia maeneo makame zaidi, yenye joto zaidi, na yenye watu wachache zaidi duniani, ilichukua miaka 126 kukamilishwa.

Kwa Nini Reli Hiyo Ilihitajika?

Mwishoni mwa miaka ya 1870, wakaaji wa kijiji kidogo cha Adelaide, kilichoko mashariki mwa ghuba inayoitwa Ghuba Kuu ya Australia, walitaka sana kusitawisha eneo hilo kiuchumi na kuanzisha njia itakayotumiwa na wafanyabiashara ambayo itaunganisha eneo hilo na eneo la kaskazini ya mbali. Marekani ilikuwa imemaliza ujenzi wa reli yake iliyounganisha eneo la mashariki na magharibi ya nchi hiyo mnamo 1869. Wakiwa na wazo hilo akilini, wakaaji wa Adelaide walitumaini kujenga reli ambayo ingeunganisha kijiji chao na Port Darwin, kama jiji la Darwin lilivyokuwa likiitwa wakati huo. Mbali na kuwawezesha watu kufika maeneo ya ndani ya nchi hiyo, reli hiyo ingepunguza muda wa kusafiri hadi Asia na Ulaya.

Wazo hilo lilionekana kuwa rahisi, lakini reli hiyo ingehitaji kupita kwenye vilima na safu za milima zenye miamba, vichaka vikubwa, na jangwa lenye mchanga na mawe ambalo sehemu zake zinakuwa vinamasi au mito mikubwa wakati wa mvua. Baada ya kujaribu mara mbili kuvuka eneo hilo lenye mazingira magumu, mwishowe mvumbuzi John Stuart, alifaulu katika jaribio la tatu mnamo 1862. Lakini walipokuwa njiani, yeye na wenzake karibu wafe kwa kukosa chakula na maji.

Joto Jingi, Dhoruba za Mchanga, na Mafuriko

Licha ya vipingamizi hivyo, wakaaji wa Adelaide hawakuvunjika moyo. Mnamo 1878, walianza kujenga reli katika jiji la Port Augusta. Wakitumia vifaa vya kawaida, farasi, na ngamia, wafanyakazi 900 wa reli walijenga reli wakielekea kaskazini kwa kufuata vijia vilivyotumiwa na Wenyeji wa Asili wa Australia kupitia Milima ya Flinder. Njia hiyo ilipitia karibu na visima vya eneo hilo, kwa kuwa magari-moshi ya mvuke huendeshwa kwa maji.

Ilichukua miaka miwili na nusu kujenga kilomita 100 za kwanza za reli hiyo. Nyakati nyingine, wakati wa kiangazi joto lilifikia nyuzi 50 Selsiasi. Joto hilo lilifanya kucha zipasuke, wino ukauke kwenye kalamu hata kabla ya kuandika, na vyuma vya reli vijipinde. Ilikuwa kawaida kwa magari-moshi kuanguka. Baada ya dhoruba za mchanga, ilibidi wafanyakazi waondoe marundo ya mchanga yaliyofunika kilomita nyingi za reli. Nyakati nyingine mchanga ungefikia kimo cha mita mbili. Mara nyingi wafanyakazi walisimama wasijue la kufanya huku dhoruba nyingine zikifunika reli walizokuwa wametoka tu kufukua.

Kisha mvua ikaanza kunyesha. Baada ya muda mfupi tu, mito ikafurika, ikapinda reli, ikafagilia mbali kazi ya miezi mingi na kufanya magari-moshi yaliyokuwa yamebeba abiria kukwama. Dereva mmoja wa gari-moshi aliwinda mbuzi-mwitu ili kuwalisha abiria. Miaka mingi baadaye, abiria wa gari-moshi lililokuwa limekwama waliangushiwa chakula kutoka kwenye ndege.

Baada ya mvua, mimea ya jangwani ilichipuka na kuleta nzige wengi. Wakati mmoja, reli zilijaa mafuta ya nzige waliopondwa-pondwa hivi kwamba kichwa kingine cha gari-moshi kilihitajika ili kusukuma gari-moshi kutoka nyuma. Tatizo lingine lilikuwa panya. Panya hao walikula chochote ambacho kingeweza kuliwa, kutia ndani vyakula, turubai, lijamu, na hata mabuti. Makaburi yaliyo kando ya reli hiyo ni kikumbusho cha mlipuko wa homa ya matumbo iliyosababishwa na mazingira machafu ya kambini wakati ujenzi huo ulipoanza.

Ili wajifurahishe, nyakati nyingine wahudumu wa gari-moshi waliwafanyia abiria mzaha. Pindi moja, wakati sungura walipozaana sana katika eneo la Alice Springs, wafanyakazi hao waliingiza sungura wengi ndani ya gari-moshi, The Ghan. Siku iliyofuata abiria walipofungua milango ya vyumba vyao kwenda kupata kiamsha-kinywa, walikutana na “sungura wengi walioruka huku na huku kwa woga,” kinasema kitabu The Ghan—From Adelaide to Alice. Wakati mwingine, mtu fulani alimwachilia kangaruu mdogo kwenye vyumba vya kulala vya gari-moshi hilo.

Nyakati nyingine, Wenyeji wa Asili wa Australia walioishi maeneo ya mbali walikaribia reli gari-moshi lilipokuwa likipita. Wakiwa wamesimama mbali kidogo, waliona watu ndani ya gari-moshi. Mwanzoni, wenyeji hao walikuwa na wasiwasi na hata waliogopa. Kwa kweli wengine wao walidhani “nyoka mkubwa sana” amewameza abiria hao wakiwa hai.

Ujenzi Wasimamishwa kwa Muda Mrefu

Baada ya miaka 13 ya kazi ngumu, reli hiyo ilipokuwa imebaki kilomita 470 hivi kufika Alice Springs, pesa za ujenzi ziliisha. ‘Ujenzi huo ulikuwa mkubwa sana hivi kwamba wakaaji wa kijiji hicho hawangeweza kuukamilisha,’ linasema jarida Australian Geographic. Mnamo 1911, utawala wa jimbo ulichukua mradi huo na kuendeleza ujenzi wa reli hiyo hadi Alice Springs. Hata hivyo, mipango ya kujenga reli hiyo hadi Darwin, mji ulio kilomita 1,420 kaskazini iliahirishwa.

Gari-moshi, The Ghan, lilipofika kwa mara ya kwanza huko Alice Springs mnamo 1929, wakaaji 200 hivi wa mji huo walijitokeza kushangilia tukio hilo. Wakaaji hao walistaajabia gari-moshi hilo lenye vyumba vya kulia, lakini kilichowashangaza hata zaidi ni bafu zake maridadi. Siku hizo, bafu lenye beseni ya kuogea lilionwa kuwa jambo geni na la anasa. Mji wa Alice Springs uliendelea kuwa kituo cha mwisho cha reli hiyo upande wa kaskazini hadi mwaka 1997. Mwaka huo, serikali na utawala wa jimbo zilikubali kukamilisha reli hiyo iliyokuwa imesubiriwa sana kutoka Alice Springs hadi Darwin. Ujenzi huo ulianza 2001.

Mashini kubwa zililaza reli yenye urefu wa kilomita 1.6 kwa siku, ambayo ilipitia juu ya angalau madaraja mapya 90 yasiyoweza kuharibiwa na mafuriko. Ujenzi huo ungegharimu dola bilioni 1.3 za Australia (karibu dola bilioni 1 za Marekani). Ilisemekana kwamba ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,420 ndio “mradi wa ujenzi uliokuwa mkubwa zaidi nchini Australia,” nao ulimalizika kabla ya muda uliotarajiwa, mnamo Oktoba 2003 ukiwa umegharimu kiasi kidogo kuliko ilivyokadiriwa.

Kivutio Katika Maeneo ya Vijijini

Leo, jiji la kisasa la Adelaide bado ndicho kituo ambacho gari-moshi The Ghan huanzia safari yake kila alasiri ili kuvuka bara hilo. Likiacha eneo hilo, gari-moshi hilo lenye mabehewa 40 yanayovutwa na vichwa viwili, hujipinda-pinda kilomita 300 hivi kwenye mashamba ya ngano likielekea kaskazini hadi Port Augusta. Linapofika mji huo, mandhari ya eneo huanza kubadilika na kuwa nchi kame yenye mchanga na vichaka vingi.

Baada ya kutoka Port Augusta, gari-moshi hilo hupita juu ya reli inayoweza kutumiwa katika majira yote ambayo iko kilomita zaidi ya 250 magharibi mwa reli ya zamani iliyokuwa ikikumbwa na mafuriko. Usiku unaingia gari-moshi hilo likiwa jangwani. Huku abiria wakiwa wamelala, gari-moshi hilo linasafiri kwa utaratibu likipita maziwa yenye maji ya chumvi ambayo huwa yamekauka kwa kipindi kirefu cha mwaka lakini hung’aa kunapokuwa na mbalamwezi baada ya mvua kunyesha. Kuna nyota nyingi wakati wa usiku kwenye anga lisilo na mawingu. Hata hivyo, hakuna kelele kama za gari-moshi la zamani kwa kuwa reli hizo zimeunganishwa vizuri ili kupunguza gharama za ukarabati.

Alfajiri, jangwa lililo karibu na mji wa Alice Springs huwa na rangi nyekundu na dhahabu jua linapoanza kuchomoza. Abiria mmoja alisema hivi: “Mandhari hiyo inapendeza sana. Hata ukiwa ndani ya gari-moshi unaweza kuhisi joto la jua. Jua linachomoza kwenye jangwa hilo kubwa lenye rangi mbalimbali lakini linaloogopesha kwa sababu halina watu. Jangwa hilo kubwa linakufanya ujihisi duni.”

Kutoka Vijijini Hadi Maeneo ya Kitropiki

Baada ya kusimama kwa muda saa za alasiri huko Alice Springs, gari-moshi hilo huendelea na safari hadi mji wa Katherine, kisha linaelekea kituo chake cha kaskazini kwenye mji wa kitropiki wa Darwin. Wakiwa ndani ya mabehewa yenye mfumo wa kupunguza joto, “abiria kwenye gari-moshi hilo husafiri kwa raha mustarehe,” anasema Larry Ierace, meneja wa gari-moshi The Ghan wakati wa safari ya kwanza ya gari-moshi hilo. Wanapotazama nje, abiria hao wanaweza kuwazia hali ngumu ambazo wajenzi wa kwanza wa reli hiyo walizikabili.

Mbali na kuchangia ukuzi wa biashara na kuwa mojawapo ya gari-moshi zinazosafiri kilomita nyingi zaidi ulimwenguni, gari-moshi The Ghan, limeleta maisha ya mjini katika sehemu za vijijini. Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 19 ambaye ni Mwenyeji wa Asili wa Australia alisema hivi alipoona gari-moshi hilo lilipokuwa likifanya safari yake ya kwanza Februari 2004: “Sijawahi kuona gari-moshi kamwe maishani mwangu. Ni maridadi sana.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]

Chanzo cha Jina

Jina The Ghan ni ufupisho wa jina la utani The Afghan Express. Watu hawajui jinsi ambavyo gari-moshi hilo lilikuja kupewa jina la wafuga ngamia wa Afghanistan. Hata hivyo, jina hilo linatukumbusha wahamiaji hao ambao walistahimili hali ngumu ili kuanzisha vijiji katika maeneo ya mbali ya Australia. Ingawa kwa ujumla wanaitwa wenyeji wa Afghanistan, wengi wao walitoka sehemu mbalimbali kama vile, Baluchistan, India Kaskazini, Misri, Pakistan, Uajemi, na Uturuki.

Walitumia ngamia kusafiri katika sehemu hizo za vijijini. Ngamia hao walitii walipoamriwa wainame au kuinuka. Msafara wa ngamia 70 hivi ulitumiwa kusafirisha watu na mizigo kwa mwendo wa kilomita sita kwa saa. Wakati usafiri wa barabara na reli ulipoanza kutumiwa, wafuga ngamia hao waliwaachilia huru ngamia wao. Leo, mamia ya maelfu ya ngamia hao huranda-randa mwituni huko Australia ya kati.—Ona Amkeni! la Aprili 8, 2001, ukurasa wa 16-17.

[Picha katika ukurasa wa 23 zimeandiliwa na]

Northern Territory Archives Service, Joe DAVIS, NTRS 573

[Picha katika ukurasa wa 25]

Train Photos: Great Southern Railway