Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tarehe ya Hati za Zamani Hujulikanaje?

Tarehe ya Hati za Zamani Hujulikanaje?

Tarehe ya Hati za Zamani Hujulikanaje?

MNAMO 1844, msomi mmoja wa Biblia, Konstantin von Tischendorf alitembelea makao ya watawa ya Mt. Catherine, yaliyo chini ya Mlima Sinai huko Misri. Akipekua-pekua maktaba za makao hayo alipata hati fulani za ngozi. Tischendorf ambaye alikuwa mchunguzi wa mwandiko wa kale, * alitambua kwamba hati hizo za ngozi zilikuwa kurasa za Septuajinti, tafsiri ya Kigiriki ya Maandiko ya Kiebrania, au “Agano la Kale.” Aliandika hivi: “Sikuwa nimewahi kuona hati zozote zinazoweza kusemwa kuwa za kale kuliko kurasa hizo za Sinai.”

Inasemekana kwamba maandishi hayo ambayo ni sehemu ya hati iliyokuja kuitwa Hati ya Sinai (Kodeksi ya Sinai), yaliandikwa katika karne ya nne W.K. Hati hiyo ya Sinai ni moja kati ya maelfu ya hati za kale za Maandiko ya Kiebrania na Kigiriki ambazo wasomi huchunguza.

Historia ya Mwandiko wa Kigiriki

Bernard de Montfaucon (1655-1741), mtawa wa makao ya Mtakatifu Benedict, alianzisha utaratibu wa kuchunguza hati za Kigiriki. Baadaye, wasomi wengine walichapisha matokeo ya uchunguzi wao. Tischendorf alifanya kazi ngumu ya kuandika orodha ya hati za kale zaidi za Biblia katika Kigiriki zilizokuwa katika maktaba mbalimbali huko Ulaya. Pia alienda huko Mashariki ya Kati mara kadhaa ili kuchunguza mamia ya hati, na akachapisha matokeo ya uchunguzi wake.

Katika karne ya 20, wachunguzi wa mwandiko wa kale walipata vifaa zaidi vya kuwasaidia. Mojawapo ya vifaa hivyo ni orodha aliyoandika Marcel Richard ya majina 900 hivi yanayofafanua hati 55,000 za Kibiblia na zisizo za Kibiblia zilizoandikwa katika Kigiriki, zinazopatikana katika maktaba 820 au zinazomilikiwa na watu binafsi. Orodha hiyo kubwa huwasaidia watafsiri na wachunguzi wa mwandiko wa kale kujua kwa usahihi zaidi hati ziliandikwa lini.

Jinsi Ambavyo Tarehe ya Hati Hujulikana

Hebu wazia unasafisha dari la nyumba ya zamani kisha unapata barua ambayo imechakaa, iliyoandikwa kwa mkono, na haina tarehe. Huenda ukajiuliza, ‘Barua hii iliandikwa lini?’ Kisha unapata barua nyingine ya kale. Mtindo, mwandiko, alama za vituo, na mambo mengine yanafanana na barua ya kwanza. Unafurahi kugundua kwamba barua ya pili ina tarehe. Ingawa hujui mwaka ambao barua ya kwanza iliandikwa, huenda sasa ukapata mambo ya kukusaidia kukadiria kipindi ambacho barua hiyo isiyo na tarehe iliandikwa.

Waandishi wengi wa kale hawakuandika tarehe ambayo walimaliza kunakili hati za Biblia. Ili kukadiria tarehe hiyo, wasomi hulinganisha hati hizo na hati nyingine, kutia ndani hati za zamani zisizo za Kibiblia ambazo tarehe zake zinajulikana, wakichunguza mambo kama vile mwandiko, alama za vituo, ufupisho wa maneno, na kadhalika. Hata hivyo, mamia kadhaa ya hati zenye tarehe zimepatikana. Zikiwa zimeandikwa kwa mkono katika Kigiriki, hati hizo ni za kati ya mwaka wa 510 W.K. hadi 1593 W.K.

Kuchunguza Mwandiko

Wachunguzi wa mwandiko wa kale hugawanya mwandiko wa kale wa Kigiriki katika sehemu mbili kuu, yaani, mwandiko wenye herufi zilizosimama unaotumiwa kwenye vitabu (book hand), na mwandiko wenye herufi zilizounganishwa (cursive) ambao hautumiwi katika vitabu. Waandishi Wagiriki pia walitumia mitindo mbalimbali ya herufi, kama vile herufi kubwa, herufi kubwa zilizounganishwa (uncial), herufi zilizounganishwa (cursive), na mwandiko wa herufi ndogo (minuscule). Aina moja ya mwandiko uliotumiwa katika vitabu, yaani, ule wa herufi kubwa zilizounganishwa, ulitumiwa kuanzia karne ya nne K.W.K. hadi karne ya nane au ya tisa W.K. Mwandiko wa herufi ndogo, ulitumiwa kuanzia karne ya 8 au 9 W.K. hadi katikati ya karne ya 15 wakati mashini za kuchapishia zenye herufi zilizopangwa zilipoanza kutumiwa huko Ulaya. Mwandiko wa herufi ndogo ungeweza kuandikwa kwa haraka zaidi na bila kutumia nafasi kubwa, na hivyo kuokoa wakati na ngozi ya kuandikia.

Wachunguzi wa mwandiko wa kale wana njia mbalimbali wanazopenda kutumia ili kujua hati iliandikwa lini. Kwa kawaida, kwanza wao huchunguza hati kwa ujumla, kisha wanaichunguza kwa makini zaidi, wakichunguza kwa undani kila herufi. Kwa kuwa muda mrefu ungepita kabla ya mtindo wa mwandiko kubadilika, kuchunguza herufi kwa undani kungewapa picha ya kijuujuu tu ya wakati ambapo hati iliandikwa.

Inapendeza kujua kwamba kuna njia nyingine za kukadiria tarehe kwa usahihi zaidi. Hilo linatia ndani kutambua mtindo fulani wa mwandiko na kujua ulianza kutumiwa lini. Kwa mfano, katika maandishi ya Kigiriki ya baada ya mwaka wa 900 W.K., waandishi walianza kutumia sana herufi zilizounganishwa. Waandishi pia walianza kutumia mtindo wa kuandika herufi fulani za Kigiriki chini ya mstari (infralinear) na vilevile kutumia alama za kuwasaidia kutamka maneno.

Kwa ujumla mwandiko wa mtu haubadiliki. Hivyo, mara nyingi maandishi yanaweza kukadiriwa kuwa yalikamilishwa katika kipindi cha miaka 50. Isitoshe, nyakati nyingine waandishi walinakili kutoka hati za zamani, na hivyo kufanya nakala yao ionekane kuwa ya zamani kuliko ilivyo kwa kweli. Hata hivyo, licha ya matatizo hayo yote, wachunguzi wamefaulu kujua tarehe za hati fulani muhimu za Biblia.

Kujua Tarehe za Hati Muhimu za Biblia ya Kigiriki

Hati ya Aleksandria (Kodeksi ya Aleksandria), ambayo sasa imewekwa katika Maktaba ya Uingereza, ilikuwa moja ya hati muhimu za kwanza za Biblia kuchunguzwa na wasomi. Ina sehemu kubwa ya Biblia na imeandikwa katika herufi kubwa zilizounganishwa za Kigiriki kwenye ngozi nyembamba. Inasemekana kwamba kodeksi hiyo iliandikwa mapema katika karne ya tano W.K., hasa kwa sababu ya mabadiliko katika mwandiko huo wa herufi kubwa zilizounganishwa ulioonekana kati ya karne ya tano na ya sita. Mabadiliko hayo ya mwandiko yanaonekana katika hati yenye tarehe inayoitwa Dioscorides ya Vienna. *

Hati nyingine muhimu ambayo wasomi walichunguza ni ile Hati ya Sinai (Kodeksi ya Sinai), ambayo Tischendorf aliipata katika makao ya watawa ya Mt. Catherine. Iliandikwa katika Kigiriki kwa mwandiko wa herufi kubwa zilizounganishwa, nayo inatia ndani sehemu ya Maandiko ya Kiebrania kutoka Septuajinti ya Kigiriki na pia Maandiko yote ya Kigiriki ya Kikristo. Kurasa 43 za kodeksi hiyo zinapatikana huko Leipzig, Ujerumani; kurasa 347 ziko katika Maktaba ya Uingereza jijini London; na visehemu vya kurasa 3 vinapatikana huko St. Petersburg, Urusi. Hati hiyo inakadiriwa kuwa iliandikwa mwishoni mwa karne ya nne W.K. Tarehe hiyo inaungwa mkono na maelezo ya pambizoni ya vitabu vya Injili yaliyoandikwa na mwanahistoria Eusebio wa Kaisaria aliyeishi karne ya nne. *

Hati ya tatu muhimu ni ile Hati Na. 1209 ya Vatikani (Kodeksi ya Vatikani), ambayo hapo awali ilikuwa na Biblia nzima katika Kigiriki. Kodeksi hiyo iliorodheshwa kwa mara ya kwanza kwenye orodha ya Maktaba ya Vatikani mnamo 1475. Hati hiyo yenye kurasa 759 za ngozi nyembamba zilizoandikwa katika Kigiriki kwa herufi kubwa zilizounganishwa, ina vitabu kadhaa vya Biblia, isipokuwa sehemu kubwa ya Mwanzo, sehemu fulani za Zaburi, na sehemu fulani za Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Wasomi wanasema hati hiyo iliandikwa mapema katika karne ya nne W.K. Walipataje tarehe hiyo? Maandishi yake yanafanana na yale ya Hati ya Sinai ambayo pia ni ya karne ya nne. Hata hivyo, Kodeksi ya Vatikani huonwa kuwa iliandikwa mapema kidogo. Kwa mfano, kutia ndani mambo mengine, haina marejeo ya pambizoni ya Eusebio.

Hazina Kutoka Kwenye Takataka

Mnamo 1920, mafunjo yaliyochimbuliwa katika rundo la takataka huko Misri ya kale yaliletwa kwenye Maktaba ya John Rylands huko Manchester, Uingereza. Msomi Colin Roberts alipokuwa akichunguza rundo hilo lililotia ndani barua, risiti, na hati za sensa, aliona kipande cha hati chenye mistari kutoka sura ya 18 ya Yohana. Kipande hicho cha hati ndicho kilichokuwa maandishi ya zamani zaidi ya Kigiriki ya Kikristo kuwahi kugunduliwa kufikia wakati huo.

Kipande hicho kilikuja kuitwa Mafunjo Na. 457 ya John Rylands, ambayo yanajulikana ulimwenguni pote kama P52. Inasemekana kwamba kipande hicho kilichoandikwa katika Kigiriki kwa herufi kubwa zilizounganishwa, kiliandikwa mwanzoni mwa karne ya pili, makumi kadhaa tu ya miaka baada ya Yohana kuandika Injili yake! Jambo la kupendeza ni kwamba, maandishi hayo yanafanana sana na hati zilizopatikana muda mrefu baadaye.

Za Kale Lakini Sahihi!

Katika kitabu chake The Bible and Archæology, mchambuzi Mwingereza Sir Frederic Kenyon aliandika hivi kuhusu Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo: “Ukweli na usahihi wa vitabu vya Agano Jipya, unaweza kusemwa kuwa umethibitishwa.” Vivyo hivyo msomi William H. Green alisema hivi kuhusu usahihi wa Maandiko ya Kiebrania: “Yaweza kusemwa kwa uhakika kwamba hakuna kazi yoyote nyingine ya kale ambayo imepitishwa kwa usahihi hivyo.”

Maneno hayo yanatukumbusha maneno ya mtume Petro: “Wanadamu wote ni kama majani, na utukufu wao wote ni kama ua la majani; majani hukauka, na ua huanguka, bali neno la Yehova linadumu milele.”—1 Petro 1:24, 25.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 ‘Uchunguzi wa mwandiko wa kale na wa Enzi za Kati unaitwa paleography. Uchunguzi huo hushughulikia hasa maandishi yaliyo katika vitu vinavyoharibika kwa urahisi, kama vile mafunjo, ngozi, au karatasi.’—The World Book Encyclopedia.

^ fu. 16 Dioscorides ya Vienna iliandikwa hasa kwa ajili ya Juliana Anicia, ambaye alikufa mnamo 527 au 528 W.K. Hati hiyo “ni mfano wa hati ya mapema zaidi ya ngozi inayopatikana yenye mwandiko wa herufi kubwa zilizounganishwa ambayo tarehe yake inaweza kukadiriwa.”—An Introduction to Greek and Latin Palaeography, cha E. M. Thompson.

^ fu. 17 Vile vinavyodhaniwa kuwa vitabu vinavyokubaliwa vya Eusebio ni orodha ya jedwali au marejeo ya pambizoni “yanayoonyesha masimulizi katika kila Injili ambayo yanafanana na masimulizi mengine.”—Manuscripts of the Greek Bible, cha Bruce M. Metzger.

[Blabu katika ukurasa wa 21]

Kwa kuchunguza kwa uangalifu hati zenye tarehe, wachunguzi wa mwandiko wa kale wanaweza kujua ni lini hati zisizo na tarehe ziliandikwa

[Sanduku katika ukurasa wa 20

Kitabu cha Kukunjwa cha Isaya cha Bahari ya Chumvi

Kitabu cha kwanza cha kukunjwa cha Isaya cha Bahari ya Chumvi kilichopatikana mnamo 1947, kilikuwa kimeandikwa kwenye ngozi katika maandishi ya Kiebrania ya kabla ya Wamasora. Inasemekana kwamba kiliandikwa mwishoni mwa karne ya pili K.W.K. Wasomi walipataje tarehe hiyo? Walilinganisha maandishi hayo na maandishi mengine ya Kiebrania na wakakata kauli kwamba kiliandikwa kati ya 125 K.W.K. na 100 K.W.K. Mbinu ya kupima umri wa vitu vya kale inayoitwa kaboni-14 ilithibitisha usahihi wa tarehe hiyo.

Kwa kushangaza, vitabu vya kukunjwa vya Bahari ya Chumvi vinapolinganishwa na vile vilivyoandikwa karne nyingi baadaye na waandishi walioitwa Wamasora hakuna mabadiliko yoyote ya kimafundisho yanayoonekana. * Tofauti pekee zinazoonekana ni zile zinazohusu njia ya kuandika maneno na sarufi. Jambo lingine linalopendeza ni kwamba Tetragramatoni, yaani, zile herufi nne za Kiebrania ambazo zinaunda jina la Mungu, Yehova, zinapatikana katika vitabu vya kukunjwa vya Isaya.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 34 Wamasora, ambao walikuwa wanakili Wayahudi waliokuwa makini sana, waliishi mwishoni mwa karne ya kwanza W.K.

[Chati/Picha katika ukurasa wa 20, 21]

 

Mwandiko wa Kigiriki

Mwandiko wa herufi kubwa zilizounganishwa (uncial)

Kuanzia karne ya 4 K.W.K. hadi karne ya 8 au 9 W.K.

Mwandiko wa herufi ndogo

Kuanzia karne ya 8 au 9 W.K. hadi karne ya 15 W.K.

Hati Muhimu

400

200

Kitabu cha Kukunjwa cha Bahari ya Chumvi

Mwishoni mwa karne ya 2 K.W.K.

K.W.K.

W.K.

100

Kipande cha Mafunjo Na. 457 ya John Rylands

125 W.K.

300

Hati Na. 1209 ya Vatikani

Mapema katika karne ya 4

Hati ya Sinai

Karne ya 4

400

Hati ya Aleksandria

Mapema katika karne ya 5

500

700

800

[Picha katika ukurasa wa 19]

Juu: Konstantin von Tischendorf

Kulia: Bernard de Montfaucon

[Picha zimeandaliwa]

© Réunion des Musées Nationaux/ Art Resource, NY

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]

Dead Sea Scroll: Shrine of the Book, Israel Museum, Jerusalem

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

Typographical facsimile of Vatican Manuscript No. 1209: From the book Bibliorum Sacrorum Graecus Codex Vaticanus, 1868; Reproduction of Sinaitic Manuscript: 1 Timothy 3:16, as it appears in the Codex Sinaiticus, 4th century C.E.; Alexandrine Manuscript: From The Codex Alexandrinus in Reduced Photographic Facsimile, 1909, by permission of the British Library