Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kuwasaidia Vijana Wakabiliane na Hali Ngumu (Machi 2007) Nina umri wa miaka 18, na mambo yaliyosemwa kuhusu simu ya mkononi na matumizi ya Intaneti yalinifaa sana. Niliwasiliana na watu ambao sikuwajua kwenye Intaneti. Muda si muda, niliingia kwenye mtego ulioletwa na mawasiliano na watu wabaya. Hali yangu ya kiroho ilizorota mara moja. Hata nilikubali kukutana na baadhi ya watu hao ana kwa ana. Inasikitisha kwamba hilo liliongoza kwenye mwenendo mpotovu kiadili. Ninasali kwamba makala hii itawasaidia wengine waepuke maumivu na mateso niliyo nayo. Kila siku ninakuwa na wakati mgumu kwa sababu ya kushindwa kulala usiku na kumbukumbu mbaya zinanisumbua mara nyingi. Lakini nimechukua msimamo thabiti dhidi ya Shetani.

B. R., Marekani

Kwa Nini Mimi Huzimia? (Aprili 2007) Nilitiwa moyo kujua kwamba si mimi tu ambaye huzimia. Makala hii imenifanya nihisi ni kana kwamba Yehova anazungumza nami moja kwa moja, akisema, “Ninaona kinachokupata na sasa ninakupa kitia-moyo.”

I. R., Madagaska

Kitu Ambacho Kinadumu Kuliko Sanaa (Aprili 2007) Maneno hayatoshi kueleza jinsi ninavyothamini makala hii. Kwa miaka sita nilisimamia studio mbili za kupiga picha zilizoleta faida. Nilipenda kazi yangu kwa kuwa iliniwezesha kutumia ustadi wangu. Lakini nilikuja kutambua kwamba kadiri nilivyofanikiwa na kuwa mashuhuri kazini ndivyo utumishi wangu kwa Yehova ulivyopungua. Nilijihusisha sana katika kazi yangu ya kupiga picha hivi kwamba sikuwa na wakati wa kufanya mambo mengine. Nilitambua kwamba nilihitaji kubadili mambo. Kwa hiyo niliacha kazi yangu na kujihusisha zaidi katika ibada. Uradhi na furaha niliyopata kutokana na kupiga picha maridadi hauwezi kulingana na furaha ninayopata katika huduma ya Kikristo.

A. P., Marekani

Vijana Huuliza . . . Je, Mtu Huyu Ananifaa? (Mei 2007) Hivi karibuni nilianza kumpenda mtu ambaye nilifikiri ananifaa. Lakini baada ya kusoma makala hiyo, niligundua kwamba sifa zake zilizonivutia hazikuwa sifa muhimu. Makala hiyo ilinisaidia kutambua kwamba mambo muhimu zaidi ya kuchunguza ni sifa za kiroho na jinsi anavyoshughulika na watu wengine. Ninamshukuru Yehova kwa kutupa sisi vijana makala kama hiyo, ambazo zinatulinda na kutuongoza.

E. P., Marekani

Wajue Watu wa Timor Mashariki (Mei 2007) Nilipendezwa sana na makala hiyo. Nilisikia kuhusu nchi hiyo kulipokuwa na ripoti za ghasia zilizofanyika. Tangu wakati huo nimetaka kujua jinsi watu wa Timor Mashariki walivyokabiliana na hali na jinsi kazi ya kuhubiri ya Mashahidi wa Yehova inavyoendelea nchini humo. Nilishangazwa na roho ya watu hao na jinsi ambavyo hawalemazwi na hali zao mbaya, badala yake wanaendelea na maisha yao ya kila siku. Nitakumbuka mtazamo mzuri ya watu wa Timor Mashariki na tabasamu changamfu za Jacob na familia yake.

Y. M., Japani