Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ Uchunguzi uliofanywa nchini Marekani unasema kwamba “asilimia 29 ya wanaume wamefanya ngono na wanawake 15 au zaidi maishani, wakilinganishwa na asilimia 9 ya wanawake waliosema kuwa wamefanya ngono na wanaume 15 au zaidi maishani.”—VITUO VYA KUDHIBITI NA KUZUIA MAGONJWA, MAREKANI.
▪ Nchini Ugiriki, “asilimia 62 ya watoto wenye umri usiozidi miaka 16 wanasema kwamba wameingiza ponografia (picha au habari za ngono) katika simu zao za mkononi.”—ELEFTHEROTYPIA, UGIRIKI.
▪ Nchini Uingereza, asilimia 82 ya watu waliohojiwa wanasema kwamba “dini ni chanzo cha migawanyiko na mizozo.”—THE GUARDIAN, UINGEREZA.
Maumivu ya Kichwa ya Miaka 64
Mwanamke fulani Mchina ambaye “ameumwa na kichwa kwa kuendelea” kwa zaidi ya miaka 60, hatimaye aligundua kile kilichosababisha tatizo hilo madaktari walipotoa risasi yenye urefu wa sentimita tatu kichwani mwake. Wajapani waliposhambulia kijiji kimoja katika Jimbo la Xinyi mnamo Septemba (Mwezi wa 9) 1943, mwanamke huyo ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 13, alipigwa risasi kichwani. Hakuna mtu ambaye angeweza kuwazia alikuwa na risasi kichwani. Maumivu ya kichwa yalipozidi, picha ya eksirei ilionyesha kwamba alikuwa na risasi, linasema Shirika la Habari la Xinhua. Inasemekana kwamba mwanamke huyo ambaye sasa ana umri wa miaka 77 “yuko katika hali nzuri.”
Nyangumi Aliyeishi Muda Mrefu
Wawindaji huko Alaska walipomuua nyangumi mwenye kichwa kikubwa mnamo 2007, walipata kichwa na mabaki ya chusa cha zamani ndani yake. Chusa hicho kilikuwa “sehemu ya mkuki unaolipuka uliotengenezwa huko New Bedford [Massachusetts, Marekani] katika miaka ya 1800,” linasema gazeti The Boston Globe. Mikuki ya aina hiyo iliacha kutumiwa baada ya muda mfupi, na hilo likawafanya wanahistoria katika Jumba la Makumbusho la Uvuvi wa Nyangumi la New Bedford kukadiria kwamba nyangumi huyo alidungwa kwa chusa hicho “muda fulani kati ya 1885 na 1895.” Kwa hiyo, lazima nyangumi huyo awe alikufa akiwa na umri wa miaka 115 hivi. Gazeti Globe linasema kwamba uchunguzi huo umetoa “uthibitisho zaidi kwa wazo ambalo limeshikiliwa na watu kwa muda mrefu kwamba nyangumi mwenye kichwa kikubwa ni mojawapo ya wanyama wanaonyonyesha wanaoishi muda mrefu zaidi, kwani anaweza kuishi kufikia miaka 150.”
Msitu wa Mvua Uliozikwa
Wanajiolojia wamegundua msitu mkubwa wa mvua uliozikwa ambao una aina nyingi zenye kuvutia za mimea iliyotoweka. Baadhi ya mimea hiyo ilikua kufikia zaidi ya mita 40. Msitu huo wa pekee unapatikana katika vijia vya mgodi wa makaa ya mawe huko Illinois, Marekani. Wanasayansi wanasema kwamba msitu huo ulizama wakati wa tetemeko kubwa la nchi. “Huo ni ugunduzi wenye kusisimua,” anasema Bill DiMichele, mtafiti mkuu wa kikundi kilichoripoti ugunduzi huo. “Tunaweza kuwaeleza kuhusu msitu huo kana kwamba tunauona.”
Kuchimbua Divai Bora
Wageni wengi wanazidi kwenda Makedonia, nchi iliyokuwa sehemu ya jamhuri ya Yugoslavia “ili kuchimbua divai bora iliyoachwa . . . na majeshi ya muungano wakati wa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu,” linasema gazeti Kathimerini—Toleo la Kiingereza. Wakiwa na ramani, wageni hao ambao hasa wanatoka Ufaransa huchimbua maeneo ambayo majeshi yalihifadhi vyombo. Kufikia sasa, divai yoyote inayopatikana imekuwapo kwa angalau miaka 90 na kulingana na gazeti hilo, “kileo kilichohifadhiwa vizuri kinaweza kuuzwa . . . kwa dola 2,675.” Wenyeji ambao wamechimbua divai na brandi wamesema kwamba “hawajawahi kuonja kitu chenye ladha nzuri kama hiyo.”