Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nchi Yenye Bafu za Pekee za Maji Moto

Nchi Yenye Bafu za Pekee za Maji Moto

Nchi Yenye Bafu za Pekee za Maji Moto

ZAIDI ya miaka 2,000 iliyopita, Waselti walianzisha kijiji karibu na chemchemi kadhaa za maji yenye madini na wakakiita Ak-Ink, jina ambalo linamaanisha “Maji Mengi.” Leo, Ak-Ink ni Budapest, mji mkuu wa Hungaria na mojawapo wa miji ya kale zaidi huko Ulaya. Wahamiaji wa mapema walifurahia kuogelea katika chemchemi hizo za maji moto, ambazo ziliburudisha na kupunguza maumivu.

Katika karne ya kwanza W.K., eneo hilo la Ulaya lilikuja kuwa chini ya utawala wa Waroma. Waroma walipanua kijiji hicho na kujenga kambi ya kijeshi ambayo waliita Aquincum. Inaaminika kwamba jina hilo lilitokana na neno la Kiselti la maji au msemo wa Kilatini aqua quinque, unaomaanisha “chemchemi tano.” Waroma walijenga mifereji, mifumo ya kuondoa maji-taka, na bafu za kibinafsi na za umma. Kwa hiyo bafu zilizoko Budapest ni za zamani.

Karne kadhaa baada ya Milki ya Roma kuporomoka bafu hizo zilianza kuwa maarufu tena. Katika karne ya 15, waandishi walisifu bafu za maji moto zilizokuwa karibu na mji mkuu wa Hungaria na hivyo kufanya jiji hilo liwe maarufu. Inasemekana kwamba Mfalme Matthias Corvinus, aliyetawala Hungaria kutoka 1458 mpaka 1490, alijenga kijia chenye paa ili kuunganisha jumba lake la kifalme na Bafu ya Rácz. Kwa hiyo, ilikuwa rahisi kufika huko hata hali ya hewa ilipokuwa mbaya.

Katika karne za 16 na 17, Waturuki walimiliki sehemu kubwa ya Hungaria kutia ndani mji wake mkuu. Walijenga bafu za mvuke na za maji moto, ambazo Waislamu hutumia kujitakasa na ambazo ni muhimu katika maisha ya kijamii ya Waturuki. Bafu zenye kupendeza za Waturuki zilikuwa vidimbwi vyenye ngazi vilivyofunikwa kwa paa. Maji yake yalimfikia mtu mabegani. Vidimbwi hivyo vilizungukwa na mabeseni na mahali pa kupumzikia na zilitumiwa kwa zamu na wanaume na wanawake. Baadhi ya bafu hizo bado zinatumiwa leo.

Mnamo 1673, kitabu fulani cha watalii kilifafanua bafu katika eneo ambalo sasa linaitwa Budapest kuwa bafu bora zaidi Ulaya kwa sababu ya “chemchemi zake nyingi za maji moto na nguvu zake za kuponya, kutia ndani ukubwa wa majengo ya kuogea na umaridadi wake.” Katika karne ya 19, bafu za mvuke zilikuwa maarufu zaidi wakati Wafini walipoanzisha sauna. Baada ya muda, bafu za mvuke, sauna, na vidimbwi vya maji baridi vilijengwa katika bafu za Budapest.

Muundo wa Eneo Hilo

Kila siku, lita milioni 70 hivi za maji hutoka katika chemchemi 123 za maji moto na chemchemi 400 za maji machungu huko Budapest. Maji hayo yote hutoka wapi? Kuchunguza muundo wa nchi hiyo kutatupa jibu.

Mto Danube, ambao hupitia Budapest, hugawanya milima ya Buda iliyo ukingo wake wa magharibi na nyanda za chini za Pest zilizo kwenye ukingo wake wa mashariki. Zamani sana, bahari ilifunika eneo hilo na iliacha mabaki ya chokaa na marumaru. Miamba hiyo ilifunikwa kwa matabaka ya matope, udongo wenye chokaa, mchanga, na makaa ya mawe.

Mianya iliyo juu ya nchi inaruhusu maji ya mvua yapenye hadi kwenye miamba moto yenye madini mengi iliyo chini kabisa ya ardhi ambayo ilichemsha maji hayo. Maji hayo moto hupanda juu kwa nguvu kupitia mianya au visima.

Muundo huo wa nchi unapatikana kotekote Hungaria. Kwa sababu hiyo, sehemu nyingi za nchi hiyo zina maji yenye madini mengi na bafu maridadi, na watu fulani huamini kwamba zina faida za kitiba na zinaweza kuponya. *

Chemchemi za maji moto zinapendwa katika sehemu nyingi ulimwenguni. Biblia inataja kugunduliwa kwa chemchemi hizo kwenye jangwa la Seiri, kati ya Bahari ya Chumvi na Ghuba ya Aqaba wakati wa enzi za wazee wa ukoo.—Mwanzo 36:24.

Wanadamu bado wana mengi ya kujifunza kuhusu mambo yenye kutatanisha katika sayari yetu. Mungu aliwekaje misingi dunia na kuumba vitu vyote vya ajabu vilivyomo? Kutafakari maswali hayo kunafanya watu wanaomhofu Mungu wastaajabie hekima nyingi ya Muumba.—Ayubu 38:4-6; Waroma 1:20.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Amkeni! halipendekezi tiba yoyote hususa.

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Bafu ya maji moto katika Hoteli ya Gellért

[Picha katika ukurasa wa 24]

Bafu za Rudas zilizojengwa na Waturuki

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Bafu za Széchenyi wakati wa majira ya baridi kali

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

All photos: Courtesy of Tourism Office of Budapest