Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Katika miaka sita iliyopita, “karibu watu 100,000 . . . wameuawa kimakusudi nchini Marekani.”—THE NEW YORK TIMES, MAREKANI.

Tovuti fulani imefuta rekodi za utambulisho za watu 29,000 waliokuwa wakiitumia ambao wameshtakiwa kwa makosa ya kingono. “Idadi inayoongezeka haraka ya rekodi za watu wanaofanya makosa ya kingono kwenye [tovuti hiyo] inadai hatua ichukuliwe,” asema Richard Blumenthal, Mkuu wa Sheria wa Connecticut.—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, MAREKANI.

“China inakumbwa na ukosefu wa majina. . . . Uchunguzi uliofanywa kotekote nchini katika 2006 ulionyesha [kwamba] majina 100 ya pili yanatumiwa na asilimia 85 hivi . . . ya Wachina bilioni 1.4.”—CHINA DAILY, CHINA.

Kwa kila kilomita moja ya usafiri, “waendeshaji wa pikipiki wanakabili hatari mara 32 ya kufa” katika misiba ya barabarani kuliko watu walio ndani ya magari.—UC BERKELEY WELLNESS LETTER, MAREKANI.

Mashahidi wa Yehova Waandikishwa Nchini Uturuki

Julai 31, 2007 (31/7/2007), Mashahidi wa Yehova nchini Uturuki walipokea taarifa rasmi ya kuandikishwa kama shirika la kidini. Hilo linawawezesha kununua na kumiliki ardhi, kukodi mahali pa kukutania, kupokea michango, na kutetea haki zao za kisheria mahakamani inapohitajiwa.

Intaneti ‘Inafanya Watu Wasiwe na Woga’

Ripoti ya tovuti (kituo cha Intaneti) moja nchini Ujerumani ambayo ilibuniwa ili kuwasaidia watu kupata wenzi wa kufanya uzinzi nao, inasema kwamba ilitembelewa na watu 310,000 na wengine 1,000 wanajiandikisha kila siku. Wabuni wa kituo hicho walijisifu kwa kuwapa watu wenzi wa kufanya uzinzi nao ‘kwa siri kabisa.’ Msimamizi mmoja alisema: “Uhakika wa kwamba watu wanaweza kuwasiliana kwa siri kwenye Intaneti unafanya wasiwe na woga sana” na hivyo kufanya iwe “rahisi zaidi kuanzisha mahusiano ya wazi.” Msimamizi mwingine alisema kwamba Intaneti itafanya uzinzi uenee.

Mabaki Yatokeza Utata

Mara nyingi wanasayansi wanasema kwamba katika “hatua” za mwisho za “mageuzi ya mwanadamu,” aligeuka kutoka jamii ya Homo habilis kisha akawa Homo erectus, na mwishowe akawa “mwanadamu wa kawaida,” yaani, Homo sapiens. Hata hivyo, nchini Kenya mabaki ya kale ya Homo habilis na Homo erectus yalipatikana karibu-karibu na sasa inaaminika kwamba hilo linadokeza kuwa jamii hizo mbili ambazo inasemekana kuwa wanadamu walitokana nazo, ziliishi wakati mmoja. “Uhakika wa kwamba jamii hizo ziliishi wakati mmoja unafanya isiwezekane kuwa jamii ya Homo erectus ilitokana na ile ya Homo habilis,” anasema Meave Leakey, mmoja wa watungaji wa ripoti hiyo.

Je, Miisho-Juma Ina Hali Mbaya Zaidi ya Hewa?

Wajerumani wengi wanadhania kwamba hali ya hewa huwa mbaya katika miisho-juma kuliko siku za kazi. Uchunguzi wa miaka 15 wa takwimu za hali ya hewa katika maeneo mbalimbali nchini Ujerumani huenda ukathibitisha maoni yao kuwa ya kweli, laripoti Der Spiegel. Jumatano (Siku ya 3) ndiyo siku yenye joto zaidi, na Jumamosi (Siku ya Posho) ndiyo yenye baridi zaidi. Jumamosi kiasi cha mvua kinaongezeka kwa asilimia 15 na kinazidi kwa asilimia 10 kile cha Jumatatu (Siku ya 1), ambayo ndiyo siku kavu zaidi. Kwa wastani Jumanne (Siku ya 2) jua linawaka kwa dakika 15 zaidi ya Jumamosi. Watafiti wanakisia kwamba uchafuzi unaosababishwa na wanadamu katikati ya juma unaongezeka hatua kwa hatua kufikia mwisho-juma. Hilo hufanya kiwango cha joto kiongezeke nalo linachangia kukusanyika kwa mawingu.