Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ghuba Maridadi

Ghuba Maridadi

Ghuba Maridadi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

GHUBA maridadi yenye rangi ya bluu-kijani ya California (iliyoonyeshwa chini), ambayo mwanzoni iliitwa Bahari ya Cortés, iko katikati ya Mexico na rasi ya Baja ya California. Sehemu kubwa ya ukanda wa jangwa hilo la pwani na kisiwa imetangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni kuwa Eneo Linalostahili Kuhifadhiwa Ulimwenguni. Kwa nini eneo hilo ni la pekee sana?

Ghuba ya California iliyo na urefu wa zaidi ya kilomita 1,000 na upana wa kilomita 153, na pia maeneo yanayozunguka ghuba hiyo ni maridadi na yenye viumbe vingi. Duniani pote, ghuba hiyo ni mojawapo ya maeneo ambako wakati wa kujaa na kupwa, maji yanaenea sehemu kubwa zaidi ya pwani, nyakati nyingine yakienea kufikia umbali wa mita 9 katika ncha yake ya kaskazini. Kwa sababu ya mwangaza wa kutosha wa jua na pia maji yaliyo na chakula kingi, kuna mimea na viumbe vingi vya baharini katika eneo hilo. Kwa sababu hizo, na pia kwa kuwa sehemu kubwa ya eneo hilo ina maji safi sana, mvumbuzi wa baharini Jacques-Yves Cousteau, aliita ghuba hiyo “hifadhi ya ulimwengu ya viumbe wa baharini.”

Ghuba hiyo iliyo na zaidi ya jamii 890 za samaki, jamii 90 kati yake zikipatikana katika eneo hilo tu, imekuwa maabara ya kiasili ya uchunguzi wa viumbe wa baharini. Hata hivyo, inasikitisha kwamba jamii nyingi zimepungua, kutia ndani pomboo wasioonekana sana wanaoitwa vaquita, neno la Kihispania linalomaanisha “ng’ombe mdogo.”

Kiumbe huyo ni mdogo zaidi katika jamii ya pomboo, hukua kufikia urefu wa sentimita 150 hivi. Ngozi yake huwa na rangi ya kijivu au kahawia, na ana mabaka meusi kuzunguka macho yake. Mnyama huyo mdogo anayepatikana tu katika eneo lenye maji yasiyo na kina ya ghuba hiyo karibu na mdomo wa Mto Colorado, ni mwoga, naye haonekani kwa urahisi wala hatujui mengi kumhusu. Kwa kweli, hakuvumbuliwa mpaka 1958 mafuvu matatu ya vaquita yalipopatikana katika ufuo wa Baja huko California.

Idadi ya vaquita ni mamia kadhaa, nao wameorodheshwa kati ya viumbe walio hatarini zaidi. Licha ya jitihada za kuwalinda, kila mwaka makumi ya viumbe hao wananaswa katika nyavu za wavuvi. Ili kusaidia kuwalinda mamalia hao wasiopatikana katika maeneo mengi, Mexico imeanzisha hifadhi ya kiasili ambayo inatia ndani makao ya vaquita. Wakaaji wa ghuba hiyo na wageni wenye kuhama wanatia ndani nyangumi, manta ray wakubwa, kasa wenye ngozi laini mgongoni, sili, marlin, samaki wanaoitwa sailfish, na idadi kubwa ya tuna.

Upande wa kusini wa ghuba hiyo, chini zaidi, wanasayansi wamepata viumbe wenye kupendeza ambao wameonekana na watu wachache sana. Hawajaonekana na wengi kwa sababu wanaishi katika bonde la Guaymas, ambalo lina kina cha mita 2,000 hivi. Bonde hilo lenye kina kirefu lina chemchemi za maji moto ambazo hutegemeza jamii mbalimbali za viumbe ambavyo havipati nishati kutokana na jua bali kutokana na kemikali inayoitwa hidrojeni-salfaidi. Kiumbe mmoja anayeishi karibu na chemchemi hizo ni tube worm. Huyo ni mnyoo ambaye hana mdomo wala tumbo. Ana manyoya mekundu naye huishi pamoja na minyoo wengine wa jamii yake. Yeye husimama wima akijishikilia kwenye sakafu ya bahari, na kama uzi anayumba-yumba kati ya maji baridi ya bahari na ya moto yanayotoka kwenye chemchemi hizo. Kila mnyoo hujitegemeza kwa kushirikiana na bakteria zinazoishi ndani yake. Manyoya yake mekundu ndiyo viungo vyake vya kupumulia.

Ijapokuwa viumbe vingi vya ghuba hiyo vimo hatarini, kuna matumaini mazuri ya wakati ujao. Kwa nini? Kwa sababu Muumba anajali. Kwa kweli, anaijali sana dunia yote hivi kwamba muda si mrefu, ataingilia kati ili kuilinda isiendelee kuharibiwa, kisha ataifanya iwe sawa na alivyokusudia mwanzoni. (Mwanzo 1:26-28; Ufunuo 11:18) Ni vigumu kuwazia jinsi Ghuba ya California itakavyopendeza wakati huo. Bila shaka, neno “maridadi” halitatosha kufafanua uzuri wake.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Nyangumi-pezi

[Picha katika ukurasa wa 25]

Minyoo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Satellite view: NASA/The Visible Earth (http://visibleearth.nasa.gov/); reef: © Dirscherl Reinhard/age fotostock

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Beach: Mexico Tourism Board; whale: © Mark Jones/age fotostock; tube worms: © Woods Hole Oceanographic Institution