Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Kuna uthibitisho mwingi wa kisayansi unaounga mkono mageuzi unaoonekana kuwa mambo halisi tunayoona na ambayo yanaongeza ujuzi wetu kuhusu uhai.”—PAPA BENEDICT WA 16.

“Baada ya daraja la miaka 40 katika barabara kuu huko Minneapolis [Minnesota] kuanguka ghafula mita 18 ndani ya Mto Mississippi wakati wa msongamano na kuua [watu 13], maofisa walifanya hima . . . kupata pesa za kukagua na kurekebisha madaraja 74,000 hivi ‘yaliyokuwa na kasoro’ huko Marekani.”—THE WEEK, MAREKANI.

Watu Wengi Wanavunja Sheria

“Wazo la kwamba ‘watu wengi hutii sheria’ ni dhana tu tunayotaka kuamini,” lasema gazeti Times la London. “Waingereza wengi wanakiri kwamba wanatii tu sheria wanazotaka, wakati tu wanapotaka.” Kituo cha Utafiti cha Masomo ya Uhalifu na Haki katika Chuo cha King, huko London, kimefunua kwamba watu wengi wanaovunja sheria ni watu “wanaoheshimiwa” katika jamii. Asilimia 33 hivi ya watu waliohojiwa walisema kwamba hulipa pesa ili kuepuka kutozwa kodi, asilimia nyingine 33 hivi hawarudishi pesa wakipewa fedha zaidi, na asilimia 20 walikiri kwamba wanaiba kazini. Watafiti wamekata kauli kwamba tabia hiyo “inafunua hali ya kiadili ya jamii—huenda hata zaidi kuliko uhalifu wenye jeuri mitaani.”

Je, Silaha za Nyuklia Ziko “Mikononi mwa Mungu”?

Kanisa Othodoksi la Urusi limebariki kazi inayofanywa na wanaume na wanawake wanaohifadhi na kudumisha silaha za nyuklia za Urusi. Katika ujumbe uliosomwa wakati wa sherehe katika Kanisa la Christ the Savior, huko Moscow, na kuripotiwa na gazeti Krasnaya Zvezda, Alexis II, mkuu wa Kanisa Othodoksi, alisema: “Ninasali kwa Mungu . . . kwamba silaha za nyuklia mlizounda na mkakabidhiwa zitabaki nyakati zote mikononi mwa Mungu na kutumiwa kuzuia vita na kulipiza kisasi.”

Asali Katika Israeli la Kale

“Uthibitisho wa kiakiolojia unaounga mkono ufafanuzi wa Biblia kuhusu Israeli . . . kuwa ‘nchi ya maziwa na asali’ (au angalau nchi ya asali) umepatikana,” chasema Chuo Kikuu cha Hebrew cha Taasisi ya Akiolojia ya Jerusalem. Uvumbuzi huo uliofanywa huko Tel Rehov katika Bonde la Beth Shean huko Israel, unahusisha safu tatu za mizinga ya nyuki ya udongo iliyopangwa kwenye matabaka matatu hivi. Safu hizo ni za “kuanzia karne ya 10 mpaka mwanzoni mwa karne ya 9 K.W.K.” na “zingekuwa na mizinga 100 hivi,” yasema ripoti hiyo. Wafugaji wa nyuki wanakadiria kwamba huenda eneo hilo lilitokeza “hata kufikia nusu tani ya asali” kila mwaka.

Wanyama-Vipenzi Hutangulizwa

Kulingana na uchunguzi fulani wa Intaneti, “Mwaustralia mmoja kati ya wanne anasema kwamba mnyama-kipenzi ndiye mshiriki muhimu zaidi katika familia, hata kuliko mwenzi au wazazi” laripoti gazeti The Sydney Morning Herald kwenye mtandao. Mtu mmoja kati ya watu watatu waliohojiwa na kampuni ya huduma za kiuchumi ya Australia alitumia “wakati na pesa zaidi kwa ajili ya wanyama-vipenzi kuliko kwa matibabu yao wenyewe.” Matibabu ya wanyama-vipenzi yanatia ndani kuchunguza utendaji wa ubongo, mbinu za hali ya juu ya upasuaji, kupandikizwa mifupa, nyonga, au viungo vingine, matibabu ya kansa, na hata upasuaji wa ubongo.