Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wahama-Hamaji wa Asia Waliofanyiza Milki

Wahama-Hamaji wa Asia Waliofanyiza Milki

Wahama-Hamaji wa Asia Waliofanyiza Milki

Urusi ilikumbwa na hofu na wasiwasi. Kama nzige, jeshi la mashujaa wapanda-farasi kutoka mashariki walivamia nchi tambarare wakiua, wakipora, na kuangamiza majeshi yoyote yaliyowapinga. Jimbo la Novgorod ndilo tu lililookoka. Akiwa huko, mwandishi mmoja alisema kwamba uvamizi huo ulifanywa na “makabila yasiyojulikana” yaliyozungumza lugha isiyoeleweka.

WAVAMIZI hao walikuwa Wamongol, watu walioishi katika nchi tambarare ambayo leo inaitwa Mongolia iliyoko katikati na kaskazini-mashariki mwa Asia. Ushindi wao wa haraka ulioanza mapema katika karne ya 13 W.K., ulibadili historia ya Asia na nusu ya Ulaya. Katika miaka 25 tu, Wamongolia walitiisha wakaaji wa maeneo mengi kuliko yale ambayo Waroma walitiisha kwa muda wa karne nne. Katika kilele cha utawala wao, walitawala kutoka Korea hadi Hungaria na kutoka Siberia hadi India. Milki hiyo ndiyo iliyotawala eneo kubwa zaidi lililoshikana kuwahi kurekodiwa katika historia!

Mbali na kutusaidia kuelewa historia ya Asia na Ulaya, maandishi ya kihistoria ya Milki ya Mongol ambayo haikudumu kwa muda mrefu yanaunga mkono mafundisho mengi ya Biblia kuhusu utu wa mwanadamu na utawala wa mwanadamu juu ya mwenzake. Kweli hizo zinatia ndani: Utukufu wa mwanadamu ni ubatili na unatoweka haraka. (Zaburi 62:9; 144:4) “Mwanadamu amemtawala mwanadamu kwa kumuumiza.” (Mhubiri 8:9) Kama zinavyofananishwa katika Biblia, falme za kisiasa zenye nguvu zimetenda kama wanyama-mwitu katika jitihada zao za kutawala mataifa mengine kimabavu. *

Wamongol Walikuwa Nani?

Wamongol walikuwa jamii ya wahama-hamaji na wapanda-farasi stadi waliojiruzuku kwa kufuga wanyama, kufanya biashara, na uwindaji. Tofauti na jamii nyingine nyingi, ambazo asilimia ndogo kati yao walizoezwa na kupewa silaha kwa ajili ya vita, karibu wanaume wote Wamongol walikuwa na farasi na upinde, nao walikuwa mashujaa hodari na wakatili. Na kila kabila lilidumisha ushikamanifu kwa kiongozi wake, aliyeitwa khan.

Baada ya kupingana kwa miaka 20, khan mmoja aliyeitwa Temüjin (karibu 1162-1227), aliunganisha makabila 27 hivi ya Wamongol chini ya uongozi wake. Baadaye, Waislamu wa asili ya Uturuki walioitwa Watatari walijiunga na Wamongol katika mapambano hayo. Kwa kweli, mashujaa wasioshindwa wa Mongol walipoelekea magharibi, wakaaji wa Ulaya waliokuwa na woga waliwaita wavamizi hao Watartari. * Mnamo 1206, Temüjin alipokuwa na umri wa miaka 40 hivi, Wamongol walimweka kuwa Genghis Khan, cheo ambacho huenda kinamaanisha “mtawala mwenye nguvu” au “mtawala wa ulimwengu.” Pia alijulikana kuwa Khan Mkuu.

Wapiga-mishale wa jeshi la Genghis Khan waliokuwa wamepanda farasi walishambulia kwa kasi na hasira, na mara nyingi walipigana vita vingi katika maeneo mengi. Kijeshi, “alitoshana na Aleksanda Mkuu au Napoleon wa Kwanza,” inasema Encarta Encyclopedia. Juzjani, mwanahistoria Mwajemi, aliyeishi wakati mmoja na Genghis Khan, alimfafanua kuwa mtu “mwenye nguvu nyingi, utambuzi, akili, na uelewaji.” Pia alimtaja kuwa “mchinjaji.”

Ng’ambo ya Mongolia

Eneo la kaskazini mwa China lilikaliwa na Manchu, ambao waliita milki yao Jin, au “Ya Kidhahabu.” Ili kufika katika maeneo ya Manchu, Wamongol walivuka Jangwa la Gobi linalotisha, lakini hilo halikuwa tatizo kubwa kwa wahama-hamaji ambao, ikiwa lazima, wangeweza kuishi kwa kunywa tu maziwa na damu ya farasi. Ijapokuwa Genghis Khan alipanua utawala wake utie ndani China na Manchuria, vita viliendelea kwa miaka 20 hivi. Alichagua baadhi ya Wachina waliokuwa wasomi, wasanii, wafanyabiashara, na pia wahandisi ambao wangeweza kujenga kuta za mazingiwa, manati, na mabomu ya unga wa risasi.

Baada ya kudhibiti njia za biashara kati ya China na Bahari ya Mediterania kuelekea pande za mbali za magharibi, Genghis Khan alijaribu kufanya mapatano ya kibiashara pamoja na Sultani Muhammad wa Uturuki. Sultani huyo alitawala milki kubwa katika eneo ambalo leo linatia ndani Afghanistan, Tajikistan, Turkmenistan, Uzibekistani, na sehemu kubwa ya Iran.

Katika 1218 wajumbe Wamongol, ambao inaelekea walitaka kufanya biashara, walifika katika mpaka wa eneo la sultani huyo. Lakini gavana wa eneo hilo aliwaua, na hivyo akaanzisha matukio ambayo yaliwafanya Wamongol wavamie kwa mara ya kwanza nchi ya Kiislamu. Katika miaka mitatu iliyofuata, Wamongol, waliosemekana kuwa wengi kuliko chungu, walipora, wakateketeza majiji na mashamba, na kuwaua raia wengi wa Sultani Muhammad, isipokuwa wale waliokuwa na ustadi ambao Wamongol walitaka.

Kisha, jeshi la Mongol lililokadiriwa kuwa na askari 20,000 hivi likapita maeneo ya Azerbaijan na Georgia kuelekea nchi tambarare iliyo kaskazini ya Caucasia likishinda majeshi yote waliyokutana nayo, kutia ndani jeshi la Urusi lenye askari 80,000. Katika safari ya kilomita 13,000 hivi, Wamongol walizunguka Bahari ya Kaspiani katika kile kinachoonwa na watu fulani kuwa mojawapo ya uvamizi mkubwa zaidi wa jeshi la wapanda-farasi katika historia. Mfululizo wao wa ushindi uliweka kielelezo cha uvamizi ambao ungefuata wa Ulaya Mashariki na watawala wa baadaye wa Mongol.

Warithi wa Genghis Khan

Ögödei, mwana wa tatu kati ya wana wanne wa Genghis Khan waliozaliwa na mke wake wa kwanza ndiye aliwekwa kuwa Khan Mkuu baada yake. Ögödei alidhibiti tena maeneo yaliyokuwa yametiishwa, akapokea ushuru kutoka kwa vibaraka, na kumaliza milki ya Jin huko kaskazini mwa China.

Ili kuendeleza milki na mtindo wa starehe wa maisha ambao Wamongol walikuwa wamezoea, hatimaye Ögödei kwenda vitani tena—lakini wakati huu alitaka kupigana na nchi ambazo hawakuwa wamezitiisha. Alishambulia maeneo mawili tofauti—nchi za Ulaya upande wa magharibi na milki ya Sung kusini mwa China. Kampeni ya Ulaya ilifanikiwa, lakini ya China haikufanikiwa. Ijapokuwa walipata mafanikio fulani, Wamongol hawakufaulu kutiisha eneo kuu la Sung.

Kampeni ya Magharibi

Mnamo 1236, jeshi lenye mashujaa 150,000 hivi, lilielekea magharibi huko Ulaya. Kwanza, walishambulia maeneo ya kando-kando ya Mto Volga; kisha wakashambulia majiji ya Urusi, na kuteketeza kabisa jiji la Kiev. Wamongol waliahidi kuyahifadhi majiji ikiwa watu wangewapa sehemu ya kumi ya kila kitu. Lakini Warusi waliamua kupigana. Wakitumia manati, Wamongol waliwapiga maadui wao kwa kutumia mawe makubwa, mafuta yanayowaka, na baruti. Kuta za majiji zilipoangushwa, wavamizi walimiminika ndani, na kuwachinja watu wengi sana hivi kwamba, kama mwanahistoria mmoja alivyoandika, “Hakuna jicho lililobaki wazi ili kuwaombolezea wafu.”

Majeshi ya Mongol yalivamia Poland na Hungaria, walifika karibu na mpaka wa Ujerumani leo. Ulaya magharibi lilijitayarisha kwa ajili ya uvamizi, lakini halikuvamiwa. Mnamo Desemba (Mwezi wa 12) 1241, Ögödei Khan alikufa, inaelekea akiwa amelewa chakari. Hivyo, makamanda Wamongol walirudi haraka kwenye jiji lao kuu, Karakorum, lililokuwa umbali wa kilomita 6,000, ili kumchagua mtawala mpya.

Güyük, mwana wa Ögödei, akamrithi baba yake. Mmoja wa watu walioshuhudia kutawazwa kwa Güyük ni kasisi Mwitaliano ambaye alifunga safari ya miezi 15 kupitia eneo lililodhibitiwa na Wamongol ili kumpelekea barua kutoka kwa Papa Innocent wa Nne. Papa huyo alitaka uhakikisho wa kwamba Ulaya halingeshambuliwa tena, na aliwahimiza Wamongol wakubali Ukristo. Güyük hakutoa ahadi yoyote. Badala yake, alimwambia papa aje pamoja na wafalme kumpa Khan heshima kuu!

Mashambulio Mengine Katika Maeneo Mawili

Khan Mkuu aliyefuata alikuwa Mongke, ambaye alitawazwa mnamo 1251. Yeye na nduguye Kublai walishambulia milki ya Sung kusini mwa China, huku jeshi lingine likishambulia maeneo ya magharibi. Jeshi lililoelekea magharibi liliharibu Baghdad na likalazimisha Damasko lisalimu amri. Watu waliodai kuwa Wakristo waliokuwa wakipambana na Waislamu walifurahi sana, na “Wakristo” walioishi Baghdad walipora na kuwaua majirani wao Waislamu.

Wakati huo muhimu sana—Wamongol walipokuwa tu tayari kumaliza jamii ya Waislamu—historia ilijirudia. Walipata ujumbe kwamba Mongke amekufa. Kwa mara nyingine tena, wavamizi hao walirudi nyumbani, wakati huu wakiwaacha wanaume 10,000 waulinde mpaka. Muda mfupi baada ya hapo, jeshi hilo lenye watu wachache liliangamizwa na jeshi la Wamisri.

Mashambulizi yaliyofanywa kusini mwa China dhidi ya milki tajiri ya Sung yalifanikiwa. Kublai Khan alijitangaza kuwa mwanzilishi wa milki mpya ya China, na kuiita Yuan. Jiji kuu la milki hiyo leo linaitwa Beijing. Baada ya kuwashinda wale ambao bado walikuwa wakiunga mkono milki ya Sung mwishoni mwa miaka ya 1270, Kublai alitawala China iliyounganishwa kwa mara ya kwanza tangu kuanguka kwa milki ya Tang mnamo 907.

Kuvunjika na Kuanguka

Karibu mwanzoni mwa karne ya 14, milki kubwa ya Mongol ilianza kuporomoka. Hilo lilisababishwa na mambo mengi. Kwanza, kwa sababu wazao wa Genghis Khan walishindania mamlaka, milki hiyo ilivunjika na kuwa milki kadhaa ndogo. Pia, Wamongol walichangamana na jamii za maeneo waliyotiisha. Huko China, mapambano ya kushindania utawala yalipunguza mamlaka ya wazao wa Kublai. Katika 1368 Wachina, waliochoshwa na utawala mbaya, ufisadi, na kodi kubwa, waliwapindua mabwana wao wa milki ya Yuan, na kuwafurusha warudi Mongolia.

Kama dhoruba kubwa, tufani ya Wamongol ilikuja haraka, ikadumu kwa muda mfupi, kisha ikapita. Lakini bado iliacha alama katika historia ya Ulaya na Asia, kutia ndani kuunganisha Mongolia na kuunganisha China. Bila shaka, Wamongolia wanamwona khan mkuu wa kwanza, Genghis Khan, kuwa baba wa taifa lao.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Ona marejeo yanayotaja wanyama-mwitu na tawala za kisiasa, au serikali katika mistari ifuatayo ya Biblia: Danieli 7:6, 12, 17, 23; 8:20-22; Ufunuo 16:10; 17:3, 9-12.

^ fu. 7 Wakaaji wa Ulaya walifikiri kwamba Watatari walikuwa mashetani waliotoka “Tartaro.” (2 Petro 2:4) Hivyo, waliwaita wavamizi hao Watartari.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 13]

Kutoka ushindi mpaka biashara

Katika kilele chake, milki ya Yuan iliyoanzishwa na Kublai Khan, ilichochea biashara na usafiri, na hivyo kutokeza kile ambacho kimeitwa “upanuzi mkubwa zaidi wa biashara katika historia ya Ulaya na Asia.” Hiyo ilikuwa enzi ya msafiri mkuu wa Venice aitwaye Marco Polo (1254-1324). * Wakisafiri kupitia nchi kavu au kwa kutumia meli, wafanyabiashara kutoka Arabia, Uajemi, India, na Ulaya walikuwa na farasi, mazulia, vito, na vikolezo, na walibadilisha vitu hivyo ili wapate vyombo vya udongo, vanishi, na hariri.

Mnamo 1492, Christopher Columbus, akiwa amebeba simulizi la safari za Marco Polo, alisafiri kwa meli upande wa magharibi kutoka Ulaya, akitumaini kusitawisha biashara na Wamongol. Hata hivyo, hakujua kwamba milki ilikuwa imeporomoka zaidi ya karne moja kabla! Kuvunjika kwa milki hiyo kulikatiza mawasiliano, na Waislamu walifunga njia ya kutoka Ulaya kuelekea Mashariki.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 33 Ukitaka kusoma kuhusu safari ya Marco Polo kuelekea China, ona makala ya Amkeni! Juni 8, 2004 (8/6/2004).

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]

Walijulikana kwa uhuru wa kidini

Ingawa waliabudu wanyama, Wamongol wa zamani waliruhusu imani nyingine. Kitabu The Devil’s Horsemen kinaeleza kwamba watu kutoka nchi za Magharibi walipoingia kwenye mji mkuu wa Mongol, Karakorum, walishangazwa na utajiri wake na pia uhuru wa kidini—makanisa, misikiti, na mahekalu yalikuwa karibu-karibu.

Ukristo uliwafikia Wamongol kupitia Wanestoria, waliokuwa wameacha Kanisa la Bizantiamu au Mashariki. Wanestoria waliwageuza imani watu wengi kati ya jamii za Waturuki wa Asia ambao walikutana na Wamongol. Baadhi ya wanawake waliogeuzwa imani hata waliolewa katika familia ya kifalme ya Mongol.

Wamongolia wa siku hizi wana dini mbalimbali. Idadi ya wanaodai kuabudu wanyama ni asilimia 30 hivi; Walama (Watibet) Wabudha, asilimia 23; na Waislamu, asilimia 5. Wengi kati ya hao wengine hawafuati dini yoyote.

[Ramani katika ukurasa wa 15]

 

Maeneo yaliyotawaliwa na Wamongol

HUNGARIA

URUSI

Kiev

Mto Volga

SIBERIA

Bahari ya Kaspiani

Damasko

IRAN

Baghdad

UZIBEKISTANI

MONGOLIA

Karakorum

Jangwa la Gobi

KOREA

CHINA

Beijing

INDIA

Novgorod

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kundi la farasi, Mongolia

[Picha katika ukurasa wa 15]

Genghis Khan

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

Bildarchiv Preussischer Kulturbesitz/Art Resource, NY

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Scenic: © Bruno Morandi/age fotostock; Genghis Khan: ©The Stapleton Collection/The Bridgeman Art Library