Kusawazisha Joto Katika Vilima vya Mchwa
Je, Ni Kazi ya Ubuni?
Kusawazisha Joto Katika Vilima vya Mchwa
▪ Kuna sababu nzuri sana kwa nini vilima vya mchwa vimeitwa maajabu ya uhandisi. Vilima hivyo vyenye kustaajabisha vilivyojengwa kwa udongo na mate, vinaweza kufikia kimo cha mita 6. Kuta zake zenye ukubwa wa sentimita 45 huchomwa na jua mpaka zikawa ngumu kama saruji. Vilima vingine vimejengwa kwa usiku mmoja tu.
Malkia huishi karibu katikati ya kilima, naye anaweza kutaga maelfu kadhaa ya mayai kila siku. “Mchwa wafanyakazi” ambao ni vipofu na wasio na mabawa hubeba mayai hayo hadi kwenye vyumba maalumu na kutunza mabuu yanapoanguliwa. Lakini huenda jambo lenye kustaajabisha sana kuhusu vilima hivyo ni mfumo wake wa kusawazisha kiwango cha joto.
Fikiria hili: Licha ya kubadilika-badilika kwa kiwango cha joto nje ya kilima, vishimo na vijia vilivyomo hudumisha kiwango kilekile cha joto ndani ya kilima. Kwa mfano, nchini Zimbabwe, Afrika, kiwango cha joto hupanda kutoka nyuzi 2 Selsiasi hivi usiku na kufikia zaidi ya nyuzi 38 Selsiasi mchana. Hata hivyo, nyakati zote kiwango cha joto ndani ya kilima cha mchwa huwa nyuzi 31 Selsiasi. Kwa nini?
Matundu yaliyo chini ya kilima huingiza hewa baridi, huku hewa yenye joto ikitokea juu ya kilima. Hewa baridi huingia kupitia vishimo vilivyo chini ya ardhi na kusambaa katika vishimo na vijia ndani ya kilima. Ili kusawazisha kiwango cha joto mchwa hufunga na kufungua matundu hayo inapohitajika. Kiwango kilekile cha joto kinahitajika ili kuvu zikue kwani ndicho chakula kikuu cha mchwa.
Muundo wa kilima cha mchwa ni wa kustaajabisha sana hivi kwamba wasanifu-ujenzi waliutumia kujenga jengo fulani huko Zimbabwe. Likilinganishwa na majengo yenye ukubwa kama huo yaliyo na mfumo wa kusawazisha kiwango cha joto, jengo hilo linatumia asilimia 10 tu ya nishati inayohitajika.
Una maoni gani? Je, uwezo wa mchwa wa kusawazisha kiwango cha joto ndani ya kilima chake ulijitokeza wenyewe? Au ni uthibitisho wa kwamba ulibuniwa?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Top: Stockbyte/Getty Images; bottom: Scott Bauer/Agricultural Research Service, USDA