Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mnamo 2007, kiwango cha barafu katika bahari ya Aktiki kilipungua “kufikia kiwango cha chini zaidi tangu satelaiti zilipoanza kutumiwa kupima.” Barafu hiyo ilienea kilomita 4,280,000 za mraba, hiyo ikiwa asilimia 23 chini ya kiwango cha chini kilichorekodiwa mwaka wa 2005.—KITUO CHA KITAIFA CHA TAKWIMU ZA BARAFU NA THELUJI, MAREKANI.

Kwa kuwa kuna bunduki 90 kwa kila raia 100 nchini Marekani, nchi hiyo ndiyo iliyo na bunduki nyingi zaidi ulimwenguni. Nchi “ya pili iliyo na idadi kubwa ya bunduki miongoni mwa raia” ni India, iliyo na “bunduki 4 tu kwa kila watu 100.”—TIME, MAREKANI.

Inaelekea kwamba msichana aliyezaliwa huko Miami, Florida, Marekani, baada ya majuma 21 na siku 6, akiwa na uzito wa chini ya gramu 283.5, “huenda ndiye mtoto aliye hai kuwahi kurekodiwa kuwa alizaliwa muda mrefu zaidi kabla ya wakati.” “Inaaminika kwamba watoto wanaozaliwa chini ya majuma 23 wakiwa na uzito wa gramu 400 hawawezi kuishi.”—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, MAREKANI.

Maji ya Bahari Yasiyo na Chumvi

Katika jitihada za kukabiliana na upungufu wa maji katika visiwa vya Bahari ya Aegea, wanasayansi Wagiriki wameunda “mfumo wa kwanza unaojiendesha na unaoelea wa kuondoa chumvi katika maji yenye chumvi bila kudhuru mazingira,” laripoti Shirika la Habari la Athens. Mfumo huo unaoendeshwa na tabo za upepo na betri zinazotumia nguvu za jua, unatokeza maji ya kutosha kwa matumizi ya kila siku ya watu 300 hivi. Mfumo huo unafanya kazi vizuri kabisa hata chini ya hali mbaya za hewa, unaweza kuongozwa na kuendeshwa kutoka mbali, na unaweza kuhamishiwa popote unapohitajiwa.

Mifupa ya Kale Yafunuliwa

“Katika sehemu za kaskazini zaidi za Siberia . . . , kiwango cha joto kinachobadilika kinasababisha barafu kuyeyuka na hivyo kufunua mifupa ya wanyama wa kale kama vile wanyama wanaofanana sana na tembo, vifaru wenye manyoya mengi na simba,” yasema ripoti ya Reuters kutoka Cherskiy, Sakha, Urusi. Wakusanyaji na taasisi za kisayansi ziko tayari kulipa pesa nyingi ili kupata mifupa mizuri, hivyo watafutaji, wakisaidiwa na wenyeji, wanajitahidi sana kupata mifupa yenye thamani katika eneo hilo. Ripoti hiyo inasema: “Barafu inayeyuka na kuvunjika haraka sana hivi kwamba katika sehemu fulani . . . baada ya kila mita chache mifupa inaonekana juu ya ardhi.”

Vileo Vilivyonaswa Vyatumiwa Vizuri

Mpaka miaka ya hivi majuzi, maofisa wa forodha wa Sweden walikuwa wakimwaga vileo vyote vilivyonaswa kutoka kwa wafanyabiashara wa magendo. Sasa vileo hivyo “vinatumiwa kutokeza nishati kwa ajili magari ya umma nchini humo,” inasema ripoti ya Shirika la Habari la Associated Press la Stockholm. Karibu lita 700,000 za vileo vilivyonaswa katika 2006 vilitumiwa kutengeneza gesi, chanzo badala cha nishati, na gesi hiyo “ikatumiwa katika mabasi, malori, na magari-moshi.” Biashara ya nishati hiyo “ni biashara nzuri,” yaeleza ripoti hiyo, “kwa sababu vitu vinavyotumiwa kuitengeneza vinapatikana bure.” Pia ni nzuri kwa sababu kuitumia kunapunguza kutokezwa kwa gesi zinazoongeza kiwango cha joto nchini Sweden.

“Wengi Wanakumbwa na Haya”

“Kwa sababu ya kutumia barua pepe, ujumbe fupi, na iPod wengi wanakumbwa na haya duniani,” laripoti gazeti Sunday Telegraph la Australia. Kulingana na Robin Abrahams, mtafiti na mwanasaikolojia, tatizo la kuona haya unapokuwa miongoni mwa watu linakabili nusu ya watu, na hilo linaonyesha kwamba idadi ya watu wenye haya inazidi kuongezeka. “Teknolojia inatuwezesha kujiondoa katika hali ngumu na kuwafanya watu wajitenge zaidi na zaidi,” anasema Abrahams. “Watu . . . wanawasiliana kupitia barua pepe na ujumbe mfupi badala ya kuzumgumza.”