Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mifereji ya Uingereza—Bado Unavutia

Mifereji ya Uingereza—Bado Unavutia

Mifereji ya Uingereza—Bado Unavutia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

Mwanzoni mwa karne ya 19 huko Uingereza, Scotland, na Wales kulikuwa na mifereji yenye urefu wa kilomita 6,000 hivi. Kwa nini mifereji hiyo ilijengwa, na ni nani wanaoitumia katika karne ya 21?

BAADA ya mvuvumko wa kiviwanda huko Uingereza katika karne ya 18, mfumo wa usafiri wa bei rahisi na wa haraka ulihitajiwa ili kusafirisha mali ghafi na bidhaa nyingine. Kabla ya kipindi hicho, farasi kadhaa walitumiwa kubeba mizigo au kuvuta mabehewa katika barabara. Katika majira ya baridi kali barabara hizo ziliharibika sana na kujaa matope hivi kwamba hazingepitika. Kwa upande mwingine, farasi mmoja tu angeweza kuvuta kwa urahisi na haraka mashua iliyobeba mizigo yenye uzito wa kufikia tani 30.

Mnamo 1761, Dyuki wa Bridgewater alijenga mfereji wa kusafirishia makaa ya mawe kutoka kwa migodi yake hadi kwa wateja huko Manchester, jiji lililokuwa umbali wa kilomita 16. Hilo lilimletea dyuki huyo pesa nyingi na likapunguza gharama ya makaa mawe huko Manchester kwa asilimia 50. Hatimaye kufikia 1790, mfumo wa mfereji wa Grand Cross uliokuwa mradi mkubwa zaidi, uliunganisha mito minne muhimu na hivyo kuunganisha eneo la viwandani la Uingereza na miji iliyo kwenye bandari. Enzi ya kutumia mifereji kwa usafiri ikaanza huko Uingereza.

Ujenzi na Matumizi ya Mifereji

Wahandisi stadi walibuni mbinu za hali ya juu za ujenzi wa mifereji yenye urefu wa kilomita kadhaa ili kupitisha maji katika maeneo yenye milima, mabonde, na tambarare. Mmoja wa wahandisi hao alikuwa James Brindley, aliyejifundisha uhandisi na alifanya kazi zake zote bila kufuata hesabu zilizoandikwa au michoro. Mifereji, vijia vya chini ya ardhi, sehemu za kuinulia mashua, na madaraja yaliyojengwa na wafanyakazi bado huonwa kuwa uthibitisho wa mafanikio ya mradi huo.

Mashua zenye urefu wa mita 20 hivi na upana wa mita 2 hivi ambazo hazikuwa na paa ziliundwa ili kubeba mizigo mikubwa. Mizigo hiyo ilitia ndani makaa ya mawe, chokaa, mawe ya chokaa, udongo mweupe, mawe yenye madini ya chuma, matofali, na unga. Mashua hizo zilikokotwa na farasi waliotembea kwenye njia za kuvutia mashua kandokando ya mifereji. Mashua nyingine zilizoenda kwa kasi zilibeba bidhaa zilizohitajiwa haraka au zile zinazoharibika haraka, nazo zilisafiri bila kusimama njiani, huku mabaharia wakifanya kazi usiku kucha.

Katika mifereji fulani, vikundi vya farasi vilivyobadilishwa kwa zamu, vilivuta mashua zilizobeba kufikia abiria 120 kwa mwendo wa wastani wa kilomita 15 kwa saa. Kama mashua zilizoenda kwa kasi sana, mashua hizo za abiria zilipewa nafasi ya kwanza. Zile zilizosafiri kwenye Mfereji wa Bridgewater, zilikuwa na upanga mkubwa kwenye omo ili kukata kamba ya kuvutia ya mashua yoyote iliyokuwa mbele yake! Ujenzi wa mifereji uliwawezesha kwa mara ya kwanza watu wa kawaida kufunga safari ndefu kwa bei nafuu na kwa starehe.

Maisha Ndani ya Mashua

Maisha ya watu katika mashua hizo yalikuwa magumu. Kazi yao ilikuwa ngumu na mara nyingi hatari. Kwa kuwa walisafiri kila wakati, hawakuwa na nafasi ya kutosha ya kupata elimu na hawangeweza kutangamana na watu waliowazunguka.

Watu hao walianzisha utamaduni wa sanaa ya kipekee kwa kupamba mashua wakitumia michoro yenye rangi za kupendeza ya mandhari mbalimbali za nchi, maumbo ya maua, na jiometria. Upande wote wa nje wa mashua na pia vyumba vilivyokuwa katika tezi vilikuwa na michoro hiyo. Mwendeshaji wa mashua, mke wake, na watoto wao waliishi katika vyumba hivyo vilivyokuwa na urefu wa mita tatu na upana wa mita mbili tu. Kwa kuwa vyumba hivyo vilikuwa na nafasi ndogo, watu walioishi katika mashua hizo walikuwa na vitanda na makabati yanayoweza kukunjwa. Vitambaa vilivyofumwa vyenye lesi vilifunika rafu, na mapambo maridadi ya kauri na shaba nyeupe kuzunguka jiko yaling’aa. Yote hayo yalifanya chumba kionekane kuwa chenye joto na starehe. Mke mwenye bidii wa mwendeshaji mashua alikuwa na majukumu mengi na mara nyingi mizigo ilileta uchafu, hata hivyo alidumisha usafi wa familia yake na wa mashua. Hata alisafisha kamba inayozungushwa kwenye usukani wa chombo hadi ikawa nyeupe pe pe pe!

Mifereji Yatoweka na Kutokea

Mwaka wa 1825, mfumo wa mifereji ulipokuwa ukielekea kukamilishwa, George Stephenson, alifungua reli katika miji ya Stockton na Darlington. Hiyo ilikuwa mojawapo ya reli za umma za kwanza zilizotumiwa na magari-moshi yaliyoendeshwa kwa mvuke. Katika kipindi cha miaka 20, reli zilianza kutumiwa kusafirisha bidhaa ambazo hapo awali zilisafirishwa kupitia mifereji. Hilo lilifanya mifereji iache kutumiwa na hivyo ikaanza kuharibika. Ili kuzuia ushindani makampuni ya reli yalinunua mifereji fulani. Baada ya Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, matumizi ya mifereji yalizidi kupungua wakati barabara mpya na nzuri zilijengwa. Hata watu wanaotazamia mema hawakufikiri kwamba mifereji ingeendelea kutumiwa kwa muda mrefu.

Lakini kwa sababu ya jitihada za watu mmoja-mmoja na vikundi vya watu, kwa miaka 50 iliyopita mifereji hiyo imeendelea kutumiwa. Ingawa mashua fulani zinazosafiri kwenye mifereji bado hubeba mizigo, nyingine zimegeuzwa kuwa nyumba au mashua za kutalii. Sasa inawezekana kusafiri kwenye mifereji yenye urefu wa zaidi ya kilomita 3,000 na kuona baadhi ya mandhari maridadi zaidi za asili za Uingereza. Ili kuwajulisha watu wengi zaidi sherehe za zamani, watu wanaopenda mashua wameanza kuzifanya tena kwa ukawaida. Kwa sababu ya umaarufu wa mashua hizo za starehe zilizopambwa kwa rangi nyingi, sasa kuna mashua nyingi zaidi kuliko wakati zilipotumiwa kusafirisha bidhaa. Mifereji inarekebishwa haraka kama vile ilivyokuwa ikijengwa miaka 200 iliyopita.

Hata hivyo, kati ya wale wanaotumia mifereji hiyo leo, waendeshaji wa mashua ni wachache sana. Kwa nini? Kurekebishwa kwa mifereji hiyo kumetokeza bustani nyingi kando ya mifereji hiyo. Bustani hizo zimewapa watu fursa ya kuona mandhari ya maeneo yasiyojulikana sana ya mijini na mashambani wanapotumia njia za kuvutia mashua iwe wanatembea kwa miguu, wanaendesha baiskeli, au ni wavuvi. Mabwawa ambayo yamejengwa ili kusawazisha kiwango cha maji katika mifereji yamekuwa makao muhimu ya viumbe, na mifereji yenyewe hutegemeza aina mbalimbali za mimea, ndege, na wanyama.

Ujenzi wa mifereji ya Uingereza ulileta mabadiliko makubwa ambayo hayakutazamiwa. Sasa mifereji hiyohiyo imekuwa mahali pa kukimbilia ili kuepuka mikazo inayosababishwa na ulimwengu wa leo, uliotokezwa na mifereji hiyo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]

KUSAFIRI NDANI YA MIFEREJI ILIYO CHINI YA ARDHI

Ni mifereji michache sana iliyo chini ya ardhi yenye njia za kuvutia mashua. Hivyo, kabla ya kubuniwa kwa mashua zenye mtambo wa kuendesha, njia hatari ilitumiwa kupitisha mashua kwenye maeneo hayo. Vipande viwili virefu vya mbao vilifungwa kwenye pande mbili za mbele za mashua. Waendeshaji mashua walilala chali juu ya mbao hizo walizozishika kwa mikono na kusukuma mashua kwa kusogeza miguu yao ukutani. Kwenye giza hilo kukiwa tu na mwangaza wa mshumaa, ilikuwa rahisi kwa mwendeshaji kuteleza na kuanguka majini, nyakati nyingine akibanwa hadi kufa kati ya ubavu wa mashua na ukuta wa mfereji. Wakati mmoja, mfumo wa mifereji huko Uingereza ulikuwa na mifereji ya chini ardhi yenye urefu wa kilomita 68, na waendeshaji mashua stadi waliajiriwa kusafiri katika mifereji ya chini mirefu zaidi. Mfereji mrefu zaidi wa chini ya ardhi ambao umefunguliwa tena Standedge, huko Yorkshire, una urefu wa kilomita tano.

[Hisani]

Courtesy of British Waterways

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

MBINU ZA KUINUA MASHUA

Kwa kuwa maji hayawezi kupanda, inakuwaje mfereji unapofika mahali palipoinuka? Ili kusafiri kwenye maji yenye kiwango kilekile, mfereji unaweza kujengwa kuzunguka mahali hapo, lakini hilo litarefusha njia. Au unaweza kupitia chini ya ardhi ndani ya kizuizi hicho. Njia ya tatu ni kuinua kiwango cha maji kwa kujenga sehemu za kuinulia mashua. Sehemu hizo za kuinulia mashua zinaunganisha maeneo yaliyo na viwango tofauti vya maji, na zina lango la kuingilia na la kutokea. Mashua inapoingia katika sehemu hiyo, malango yote mawili yanafungwa. Kisha, ikitegemea kiwango cha maji kilicho katika sehemu inayofuata, maji hupunguzwa au kuongezwa ili kuwe na kiwango sawa, kisha mashua huendelea na safari.

Vipi ikiwa sehemu hizo za kuinulia mashua haziwezi kukarabatiwa? Hilo ndilo tatizo walilokabili wajenzi huko Scotland katika mradi wa kukarabati mifereji miwili iliyounganisha Glasgow na Edinburgh. Haingewezekana kukarabati sehemu 11 za kuinulia mashua zilizo huko Falkirk ambazo ziliunganisha Mfereji wa Union na ule wa Forth na Clyde ambao ndio mfereji wa kale zaidi ulimwenguni unaounganisha bahari mbili. Suluhisho lilikuwa kujengwa kwa Gurudumu la Falkirk ambalo lilikuwa na muundo wa kipekee sana. Gurudumu hilo la kuinulia mashua lina kipenyo cha mita 35. Gurudumu hilo linaweza kuinua mashua nane, nne kila upande, kutoka kiwango moja cha maji hadi kingine kwa dakika 15 tu.

Gazeti The Times la London linafafanua gurudumu hilo kuwa “uhandisi wa kustaajabisha,” na kivuli chake huonekana katika kidimbwi kikubwa cha duara kilicho na nanga za mashua zaidi ya 20.

[Hisani]

Top right: Courtesy of British Waterways

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16, 17]

SABABU INAYOFANYA TUFURAHIE KUSAFIRI KATIKA MIFEREJI

Katika miaka ya karibuni mimi na mke wangu tumefurahia likizo tulivu kwa kusafiri kwa mashua katika mifereji hata kama tumezeeka. Kwa nini tunasema likizo tulivu? Kwanza, tuko mbali na kelele za magari na wale wanaopenda kuendesha gari kwa kasi. Ukiwa katika mashua, unaweza kusafiri taratibu kwa mwendo usiozidi kilomita 5 kwa saa. Kwa nini tusafiri kwa mwendo wa kinyonga? Ili kuepuka kufanyiza mawimbi yanayoweza kuharibu kingo za mfereji. Hivyo, hata watu wanaowatembeza mbwa wao huwa wanaenda haraka kuliko sisi.

Pia tunasafiri kwa mwendo huo ili kufurahia mandhari na kuwasalimu wapita-njia. Mandhari hiyo huwa maridadi sana. Kwa kawaida sisi hukodisha mashua zilizo katika Mfereji wa Monmouthshire na Brecon huko South Wales. Mfereji huo una urefu wa kilomita 50 hivi kutoka mpaka wa Wales hadi kwenye milima ya Brecon iliyo na mwinuko wa mita 886. Sisi husisimuka tunapofikia sehemu ambapo mashua huinuliwa au kushushwa.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 15.

Mashua hizo zina kila kitu tunachohitaji na ni starehe sana. Nyingine hata zina vyumba viwili vya kulala vya watu wawili, kila chumba kikiwa na bafu na choo. Zina mfumo wa kupasha joto ikiwa kuna baridi usiku. Kwa kawaida tunajipikia, lakini ikiwa hatutaki kupika, tunaweza kutia nanga na kula chakula kitamu katika mojawapo ya mikahawa iliyo kando ya mfereji.

Kuna utulivu mwingi, hasa alfajiri wakati unapoweza kuona majini miti na vilima vilivyo kando ya mfereji. Kuna kimya chenye mshindo hivi kwamba mtu anaweza kusikia vizuri ndege wakiimba. Kwenye kingo za mfereji, korongo hutembea polepole na kwa utulivu mbele yetu.—Tumetumiwa makala hii.

[Hisani]

Courtesy of British Waterways

Top right: By kind permission of Chris & Stelle on Belle (www.railwaybraking.com/belle)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

Courtesy of British Waterways