Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mnamo 2007 Wachina milioni 47 hivi walikumbwa na ukosefu wa maji ya kunywa kwa sababu ya ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miaka kumi. Wakati huohuo, Wachina milioni 42 waliathiriwa na tufani, huku milioni 180 wakiathiriwa na mafuriko.—SHIRIKA LA HABARI LA XINHUA, CHINA.

“Mnamo 2003, inakadiriwa kwamba mimba moja kati ya tano ulimwenguni pote zilitolewa. Huko Ulaya, takwimu hizo zilikuwa mimba moja kati ya tatu . . . [Katika] nchi zilizokuwa chini ya Muungano wa Sovieti, . . . inakadiriwa kwamba katika mwaka wa 2003 asilimia 45 ya mimba zilitolewa.”—BRITISH MEDICAL JOURNAL, UINGEREZA.

Michezo ya Video Yenye Jeuri Kanisani

“Mamia ya wahudumu na makasisi wanaojaribu kuwavutia vijana waje kanisani wamechambuliwa vikali kwa sababu ya kutumia njia isiyo ya kawaida kutekeleza lengo lao.” Wametumia “mchezo wa video wenye jeuri” ambao “unapendwa sana,” linasema gazeti The New York Times. Mchezo huo umekusudiwa uchezwe hasa na watu wazima. Mchezaji ambaye hucheza kama askari, anahitaji kutumia njia mbalimbali kuua. Hilo halijawazuia wasimamizi wa vikundi mbalimbali vya vijana Waprotestanti na wa kievanjeli “kujaza vituo vyao na mashini nyingi za kucheza video ili vijana wengi waje kucheza mchezo huo,” linasema gazeti hilo.

Utambulisho wa Watoto Unaibwa

Idadi inayoongezeka ya utambulisho wa watoto unaibwa, na hilo linaweza kuathiri sana uwezekano wao wa kupewa mikopo na uhusiano wao na watu walioiba utambulisho wao, linasema jarida The Wall Street Journal. Uhalifu huo ambao kwa kawaida unafanywa na mtu wa familia, unaweza kuendelea kwa miaka mingi bila kugunduliwa. “Watu wengi hawatambui kwamba mtu amekuwa akitumia utambulisho wao kinyume cha sheria . . . hadi wanapotafuta kazi kwa mara ya kwanza, leseni ya kuendesha gari, mkopo wa wanafunzi au wa kununua nyumba,” linaeleza jarida hilo. Wengine hugundua mapema kwamba utambulisho wao unatumiwa shirika la mkopo linapojaribu kudai deni ambalo limerundamana katika jina la mwathiriwa.

Makombora ya Nyuklia “Yalipotea”

Agosti 30, 2007 (30/8/2007), ndege ya Jeshi la Angani la Marekani aina ya B-52 bomber iliruka juu ya anga la Marekani kwa saa tatu na nusu ikiwa imebeba makombora sita ya nyuklia ambayo yalikuwa “yamewekwa kimakosa kwenye bawa la ndege hiyo,” linaripoti gazeti The Washington Post. Marubani wa ndege hiyo na wafanyakazi walioweka makombora hayo hawakugundua kosa hilo, ambalo “kwa kustaajabisha halikugunduliwa kwa saa 36,” linasema gazeti hilo. Kulingana ripoti fulani, “maofisa wa Jeshi la Angani walisema kwamba makombora hayo hayakuwa tayari kutumiwa na hakuna wakati yalipokuwa tisho kwa raia.” Hata hivyo, mtangazaji mmoja aliuliza: “Tukio hilo litutie wasiwasi kadiri gani?”

Njiwa Wanatumiwa Kupima Uchafuzi

Uchunguzi uliofanyiwa njiwa katika jiji la Jaipur unaonyesha kwamba ndege hao wanaweza kutumiwa kupima kiwango cha uchafuzi katika jiji, wanasema wachunguzi katika Chuo Kikuu cha Rajasthan, kaskazini mwa India. “Vyuma vinavyopatikana katika mazingira wanamoishi huingia katika manyoya yao, na kubaki hata baada ya [manyoya] kunyonyoka,” linaeleza gazeti la New Delhi Gobar Times, ambalo ni nyongeza ya gazeti Down to Earth. Kwa kuwa njiwa huishi katika eneo moja, viwango vya kadimiamu, kromiamu, shaba, na risasi vinavyopatikana katika manyoya vinaweza kuwa vipimo sahihi vya uchafuzi katika eneo fulani.