Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Roboti Zimepiga Hatua Kubwa

Roboti Zimepiga Hatua Kubwa

Roboti Zimepiga Hatua Kubwa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI JAPANI

ROBOTI. Neno hilo huleta wazo gani akilini mwako? Watu fulani huona roboti kuwa zenye faida na vitu vinavyoweza kusaidia kazi. Wengine huziona kuwa tisho, yaani, mashine zenye uwezo mkubwa wa akili ambazo siku moja zitachukua kazi zinazofanywa na wanadamu. Hata hivyo, wengine huziona kuwa ubuni tu wa kisayansi.

Namna gani leo? Kulingana na kadirio la uchunguzi mmoja lililotolewa 2006 na Shirikisho la Kimataifa la Utengenezaji wa Roboti, kuna roboti karibu milioni moja zinazofanya kazi viwandani ulimwenguni pote, na karibu nusu ziko barani Asia. Kwa nini kuna uhitaji mkubwa hivyo wa roboti?

Kazi Zinazofanywa na Roboti

Wazia mfanyakazi ambaye haachi kufanya kazi, halalamiki, na anafanya kazi bila kuchoka kwa saa 24 kila siku, siku saba kwa juma. Hiyo ndiyo kazi inayofanywa na roboti katika viwanda vya kutokeza bidhaa mbalimbali kama vile magari, vifaa vya umeme, na vifaa vya nyumbani. Jina lao, roboti, linawafaa sana kwa kuwa linatokana na neno la Kicheki, robota, linalomaanisha “kazi ya kulazimishwa.” Inakadiriwa kwamba katika mwaka wa 2005, kulikuwa na roboti 1 kwa kila wafanyakazi 10 katika viwanda vya kutengeneza magari!

Hata hivyo, siku hizi roboti hazitumiki kwenye viwanda peke yake. Roboti za kisasa zina vifaa vya kutambua sauti, zinaweza kutembea, zina mfumo wa mawasiliano usiounganishwa kwa nyaya, zina Mfumo wa Kupokea Habari Kutoka kwa Setilaiti (GPS), na vifaa vya kupima joto, nguvu, sauti zisizoweza kusikiwa na wanadamu, kemikali, na mnururisho. Kwa kuwa sasa roboti zina nguvu zaidi na uwezo mwingi kuliko zamani, zinafanya kazi ambazo miaka michache iliyopita ilionekana kwamba haziwezi kufanya. Fikiria mifano ifuatayo.

Huduma. Katika hospitali moja huko Uingereza, roboti inayofanya kazi katika chumba cha dawa, inapokea na kuwapa wagonjwa dawa kwa sekunde chache. Shirika la Posta la Marekani lina roboti ambazo zinatumiwa kukagua, kuinua na kupanga masanduku yenye barua. Roboti nyingine pia hutumiwa kufikia maeneo yenye nafasi ndogo, kama vile ndani ya mbawa za ndege, ili kufanya uchunguzi au marekebisho.

Mwandamani. Katika makao ya kuwatunzia wazee huko Japani, wagonjwa waliozeeka kwa zamu wanapapasa roboti ndogo yenye umbo la sili iliyo na manyoya. Roboti hiyo inaweza kutambua na kuitikia inapoguswa, kunapokuwa na mwangaza, inaposikia sauti, joto linapobadilika, na kulingana na inavyoshikwa. Inaweza kuiga tabia za mnyama kwa kupiga kelele kwa uchangamfu, kufumba na kufumbua macho, na kuchezesha mapezi yake. Inasemekana kwamba roboti hiyo inatimiza uhitaji wa msingi wa mwanadamu wa kuwa na mwandamani na inatumiwa katika matibabu.

Matibabu. Roboti yenye mikono mitatu inasimama kando ya mgonjwa. Daktari anasimama kando na kuangalia kupitia kiwambo kikubwa kinachoonyesha moyo wa mgonjwa. Daktari huyo anaongoza mikono ya roboti hiyo inapofanya upasuaji wa kurekebisha mshipa wa moyo. Njia hiyo huwezesha kufanya upasuaji bila kugusa viungo vingine kwa sababu roboti inaweza kufikia sehemu hususa, hilo linapunguza mshtuko wa mwili, uvujaji wa damu, na kumsaidia mgonjwa kupona haraka.

Nyumbani. Unahitaji tu kubonyeza swichi kwenye roboti yenye umbo la mviringo ili kufyonza uchafu kwenye sakafu. Roboti hiyo huondoa uchafu kwenye maeneo yasiyo na vifaa ikizunguka na kusonga kandokando ya ukuta, na hivyo kutambua mpangilio wa nyumba. Inatambua mahali ngazi zilipo na kuziepuka. Roboti hiyo huacha kusafisha inapomaliza na kurudi mahali inapoongezwa nguvu. Kuna roboti zaidi ya milioni mbili kama hizo zinazotumika.

Angani. Roboti yenye magurudumu sita inayoitwa Spirit inachunguza sayari Mihiri. Ikiwa na vifaa vya kisayansi kwenye mikono yake, roboti hiyo inachunguza udongo na mawe. Kwa kutumia kamera, roboti hiyo imepiga picha zaidi ya 88,500 kwenye sayari hiyo, zikitia ndani mchanga, mabonde, mawingu, dhoruba za mchanga, na machweo. Ni mojawapo ya roboti mbili zenye magurudumu zinazotumika kwenye sayari Mihiri.

Kazi ya Kutafuta na Kuokoa Watu. Chini ya vifusi vya chuma moto zilizopindika na zege za majengo yaliyoanguka ya World Trade Towers, roboti 17 zinazotoshana na mpira wa vikapu zilitumiwa kutafuta watu waliokwama. Tangu wakati huo, roboti za hali ya juu zaidi zimetengenezwa kama ile inayoonyeshwa hapa chini.

Chini ya Maji. Roboti zinazojiendesha chini ya maji zinatumiwa na wanasayansi kuchunguza eneo la dunia ambalo halijavumbuliwa, yaani, bahari. Roboti hizo hazina dereva. Matumizi mengine ya roboti chini ya maji yanatia ndani kutafuta na kuokoa watu, kukagua nyaya za mawasiliano, kufuata nyangumi, na kuondoa mabomu yaliyotegwa baharini.

Roboti Zinafanana na Wanadamu Kadiri Gani?

Kwa karne nyingi, mwanadamu ametamani kujenga roboti zinazofanana na mwanadamu. Lakini hilo limekuwa jambo gumu sana kufanya. “Ni jambo rahisi zaidi kujenga kompyuta za hali ya juu, majengo marefu sana, au hata kuchora ramani ya majiji mazima kuliko kuiwezesha mashine iwe na uwezo wa kusonga kama mwanadamu, kuona, kunusa, kusikia, na kugusa, pia uwezo wa akili unaokaribia ule wa mwanadamu,” likasema jarida Business Week.

Kwa mfano, fikiria jambo linaloonekana kuwa rahisi kama kutengeneza roboti inayoweza kutembea. Baada ya miaka 11 ya utafiti wenye kina na kutumia mamilioni ya dola, wataalamu Wajapani walitimiza jambo hilo la kustaajabisha mnamo Septemba 1997. Tangu wakati huo, wataalamu wametengeneza roboti zinazoweza kupanda ngazi, kukimbia, kucheza dansi, kubeba vitu kwenye sinia, kusukuma mkokoteni, na hata kujiinua baada ya kuanguka!

Wakati Ujao wa Roboti

Roboti zitatumiwaje wakati ujao? Kwa sasa, shirika la NASA la Marekani linabuni roboti inayoweza kufanya kazi hatari angani. Bill Gates alisema inawezekana kwamba “roboti zitatimiza fungu muhimu katika kuwasaidia watu na zitakuwa waandamani kwa wazee.”

Vivyo hivyo, katika ripoti iliyotolewa na serikali ya Japani, inatarajiwa kwamba kufikia 2025 roboti zitashirikiana na wanadamu kutunza wagonjwa, kulea watoto, na kufanya kazi za nyumbani. Kufikia 2050, watafiti wanatarajia kwamba kutakuwa na timu ya mpira ya roboti itakayoshinda timu ya wanadamu. Pia, inatarajiwa kwamba baada ya makumi ya miaka, mashine zenye uwezo wa akili unaopita ule wa wanadamu zitatokezwa.

Ingawa watu fulani wana matarajio hayo mazuri, si kila mtu anayekubaliana nao. Kuhusu matatizo ya kiufundi wanayokabili, Jordan B. Pollack, mtafiti wa uwezo wa akili wa roboti alisema hivi: “Tumepuuza sana uwezo wa kujiratibu wa hali ya juu wa viumbe hai.”

Hatujui roboti zitafanyiwa maendeleo kadiri gani wakati ujao. Hata hivyo, tuna uhakika huu: Ni wanadamu tu ambao sikuzote watakuwa na uwezo wa kuonyesha upendo, kutenda kwa hekima, haki, na nguvu. Kwa nini? Biblia inasema wazi kwamba tofauti na viumbe wengine, ni mwanadamu peke yake aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu. (Mwanzo 1:27) Wanadamu si mashine zisizo na hisia zinazoongozwa na programu fulani. Ni viumbe walio na uwezo wa kuchagua, wenye ufahamu na uwezo wa kumwabudu Mungu. Jambo hilo na lituchochee kumkaribia Muumba wetu, Yehova Mungu!—Yakobo 4:8.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Courtesy Aaron Edsinger

Courtesy OC Robotics

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Courtesy AIST

© 2008 Intuitive Surgical, Inc.

Courtesy iRobot Corp.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Top: NASA/JPL-Solar System Visualization Team; left: NASA/JPL/Cornell University

© The RoboCup Federation

Greg McFall/NOAA/Gray’s Reef National Marine Sanctuary

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]

© 2007 American Honda Motor Co., Inc.