Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

‘Kupita Katika Tundu la Sindano’

‘Kupita Katika Tundu la Sindano’

‘Kupita Katika Tundu la Sindano’

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

WAGUNDUZI Waingereza walipogundua Mlango-Bahari wa Bass mnamo 1798, maofisa wa jeshi la majini walifurahi sana. Ikitenganisha kisiwa cha Tasmania na nchi kavu ya Australia, njia hiyo ya baharini ilipunguza safari ya kutoka Uingereza hadi Sydney kwa kilomita 1,100.

Hata hivyo, Mlango-Bahari wa Bass umethibitika kuwa mojawapo wa njia hatari zaidi baharini kupitia. Njia hiyo ina pepo zenye nguvu, mikondo yenye nguvu, na kina kifupi sana cha maji cha mita 50 hadi 70 hivi, mambo ambayo huchangia kutokeza mawimbi makubwa sana yanayofanya njia hiyo isipitike kwa urahisi. Pia, matumbawe yaliyochongoka ya Kisiwa cha King, kilicho katikati ya mlango-bahari huo upande wa magharibi, ni hatari sana.

Siku hizi si vigumu kupitia Mlango-Bahari wa Bass. Lakini haikuwa hivyo zamani wakati ambapo kulikuwa tu na meli zilizoendeshwa kwa matanga na vifaa duni vya kuziongoza. Lilikuwa jambo lenye kuogopesha kupitia upande wa magharibi wa mlango huo, na safari kama hiyo ililinganishwa na ‘kupita katika tundu la sindano.’

Kusafiri Kupitia Njia Fupi

Katika miaka ya mapema ya karne ya 19, meli zilichukua miezi mitano hivi kusafiri umbali wa kilomita 19,000 kutoka Uingereza hadi Australia mashariki, na safari hiyo ilikuwa na matatizo mengi. Kwa kawaida, mamia ya wasafiri ambao wengi wao walikuwa wahamaji na wafungwa, walijazwa kwenye sehemu ya chini ya meli ambako hali zilikuwa mbaya sana. Watu wengi walipatwa na kichefuchefu, utapia-mlo, na magonjwa mengine, na kulikuwa na wanyama wengi waharibifu. Mara nyingi watu walikufa. * Lakini wasafiri walipata nguvu za kuvumilia kwa sababu ya kutarajia maisha mazuri.

Mnamo 1852, safari hiyo ilianza kuwa rahisi wakati Kapteni James (Bully) Forbes aligundua njia fupi. Akiamua kutofuata njia iliyoitwa 39th parallel ambayo ilionekana kuwa ndiyo njia fupi zaidi kupitia kusini mwa Bahari ya Hindi hadi Australia, Forbes alifuata njia fupi kutoka Uingereza hadi kusini-mashariki ya Australia, na njia hiyo ikamwongoza upande wa kusini zaidi kuelekea Antaktika. * Licha ya kwamba kulikuwa na miamba ya barafu na mawimbi makubwa, meli ya Forbes, iliyoitwa Marco Polo, ikiwa imebeba wahamaji 701, ilitia nanga huko Melbourne, Victoria, baada ya siku 68 tu, ikitumia karibu nusu ya muda uliohitajika kusafiri kufika huko. Ugunduzi huo ulitukia wakati unaofaa sana, kwa kuwa harakati za kutafuta dhahabu huko Victoria zilikuwa zimepamba moto. Habari kuhusu njia hiyo fupi ziliwafanya maelfu ya wachimba-migodi wasafiri kwenda Australia.

Meli zilipoondoka Uingereza zilitia nanga huko Cape Otway, umbali wa kilomita 16,000 hivi. Mabaharia walitumia chombo cha kupima pembe na chati za kufanya hesabu za latitudo, na walitumia saa ya meli, iliyosawazishwa na saa ya ulimwengu, ili kutambua longitudo. Wakati wa mahali ulipimwa kulingana na mahali jua lilikuwa. Tofauti ya saa moja kati ya mahali meli ilipokuwa na saa ya ulimwengu iliwakilisha nyuzi 15 za longitudo. Vipimo vya latitudo na longitudo vilimwezesha baharia kujua mahali alipo kwa usahihi wa kadiri fulani.

Lakini mambo yanaweza kuharibika. Huenda mawingu yakalifunika jua siku nyingi. Na saa za zamani hazikuwa sahihi siku zote. Kupoteza au kuongeza sekunde moja kila siku kwa miezi mitatu kungefanya meli ipotee njia kwa kilomita 50. Kulipokuwa na mvua, ukungu, au giza, meli zilizopotea njia zingeweza kukosa mwingilio wa Mlango-Bahari wa Bass na kupata matatizo kwenye pwani yenye mawe-mawe ya Kisiwa cha King au Victoria. Basi haishangazi kwa nini wasafiri wengi walirudia maneno ya kapteni ambaye alipoona Cape Otway kwa umbali alisema hivi kwa sauti: “Asante Mungu! Hatujakosea.” Ni uthibitisho wa ustadi wa wanabaharia wa karne ya 19 uliowawezesha ‘kupita katika tundu la sindano.’ Hata hivyo, si meli zote zilizofanikiwa kupita.

Kaburi la Meli

Kabla ya alfajiri ya Juni 1, 1878 (1/6/1878), meli ya matanga iliyoitwa Loch Ard ilisafiri kwenye ukungu kuelekea pwani ya Victoria. Ukungu huo ulioanza siku iliyotangulia ulimzuia nahodha kujua mahali hususa ambapo meli yake ilikuwa. Kwa sababu hiyo alikuwa karibu na pwani ya Australia kuliko alivyodhani. Kwa ghafula, ukungu uliondoka na akaona miamba yenye urefu wa mita 90 kilomita mbili hivi mbele yake. Mabaharia walijitahidi kuigeuza meli hiyo lakini upepo na mkondo wa bahari ukawazuia. Katika muda wa saa moja hivi, meli hiyo iligonga tumbawe kwa kishindo kikubwa na ikazama dakika 15 baadaye.

Kati ya watu 54 waliokuwa kwenye meli hiyo, ni wawili tu waliookoka, mfanyakazi wa meli Tom Pearce, na abiria Eva Carmichael. Wote walikuwa na umri usiozidi miaka 20. Kwa muda wa saa nyingi, Tom alishikilia mashua ya kuokoa uhai akiwa ndani ya maji baridi sana. Hatimaye alichukuliwa na mkondo wa maji hadi kwenye korongo lililokuwa katikati ya miamba mikubwa. Alipoona ufuo mdogo uliojaa vipande vya meli, aliogelea hadi ufuoni. Eva hangeweza kuogelea kwa hiyo alishikilia mabaki ya meli kwa saa nne hivi kabla ya kuchukuliwa na mkondo hadi kwenye korongo hilo. Alipomwona Tom ufuoni, alipaaza sauti akiomba msaada. Tom aliruka ndani ya mawimbi makubwa na baada ya kujitahidi kwa saa moja alimburuta Eva aliyekuwa amepoteza fahamu hadi ufuoni. Eva alisimulia hivi: “Alinipeleka ndani ya pango lililokuwa zaidi ya mita 50 kutoka ufuoni na akapata kasha lililokuwa na mvinyo akafungua chupa moja, akaninywesha, na hilo likanifanya nipate fahamu. Alitandika nyasi ndefu na majani fulani ili nilalie. Nilipoteza fahamu kwa saa kadhaa.” Wakati huo, Tom alipanda mwamba huo mkubwa na kwenda kutafuta msaada. Muda usiozidi saa 24 baada ya meli ya Loch Ard kuzama, Tom na Eva walipelekwa katika nyumba iliyokuwa karibu. Wazazi wa Eva, ndugu zake watatu, na dada zake wawili walikufa katika msiba huo.

Siku hizi, maelfu ya meli kubwa na ndogo hupitia Mlango-Bahari wa Bass kila mwaka. Njiani wao hupita sehemu mbalimbali ambapo meli zaidi ya 100 zilizama. Watalii hutembelea sehemu hizo, kama vile Loch Ard Gorge katika Mbuga ya Taifa ya Port Campbell, huko Victoria. Sehemu hizo ni vikumbusho vyenye kuhuzunisha vya ujasiri wa watu walioishi katika karne ya 19 ambao baada ya kusafiri kutoka mbali sana, walijasiria kupitia njia hiyo hatari, “tundu la sindano,” wakitafuta maisha bora.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Mnamo 1852, mtoto 1 kati ya 5 mwenye umri wa miezi isiyozidi 12 alikufa safarini kutoka Uingereza kwenda Australia.

^ fu. 8 Kamba inapovutwa kwa nguvu kati ya sehemu mbili kwenye duara, itapitia njia fupi zaidi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

NI NINI KILICHOWAPATA TOM NA EVA?

Tom Pearce na Eva Carmichael, waokokaji pekee wa msiba wa meli iliyoitwa Loch Ard, walikuwa maarufu upesi huko Australia. Kitabu Cape Otway—Coast of Secrets kinasema: “Magazeti yalitangaza sana kuhusu msiba huo, Pearce alisifiwa kuwa shujaa, Eva Carmichael akasemwa kuwa mrembo na yakasisitiza kwamba wanapaswa kuoana.” Ingawa Tom aliomba kumwoa, Eva alikataa na kurudi Ireland baada ya miezi mitatu. Akiwa huko aliolewa na kuanzisha familia. Eva alikufa mnamo 1934 akiwa na umri wa miaka 73. Tom alirudi kuabiri baharini na upesi akavunjikiwa na meli kwa mara ya pili. Kwa mara nyingine tena aliokoka. Baada ya kuwa nahodha wa meli zinazoendeshwa kwa mvuke kwa miaka mingi, Tom alikufa mnamo 1909 akiwa na umri wa miaka 50.

[Hisani]

Both photos: Flagstaff Hill Maritime Village, Warrnambool

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Forbes alisafiri kutoka Uingereza hadi Australia kwa kutumia meli iliyoitwa “Marco Polo” (juu) kupitia njia fupi

[Mchoro]

NJIA YA ZAMANI

39th parallel

NJIA FUPI

Mzingo wa Antaktiki

[Ramani]

BAHARI YA ATLANTIKI

BAHARI YA HINDI

ANTAKTIKA

[Hisani]

From the newspaper The Illustrated London News, February 19, 1853

[Mchoro/Ramani katika ukurasa wa 16, 17]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kusafiri kupitia mwingilio wa magharibi wa Mlango-Bahari wa Bass kulisemwa ni ‘kupita katika tundu la sindano’

[Ramani]

AUSTRALIA

VICTORIA

MELBOURNE

Mbuga ya Taifa ya Port Campbell

Cape Otway

Mlango-Bahari wa Bass

Kisiwa cha King

TASMANIA

[Picha katika ukurasa wa 16]

Baada ya kugonga tumbawe, meli inayoitwa “Loch Ard” ilizama baada ya dakika 15

[Hisani]

La Trobe Picture Collection, State Library of Victoria

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mbuga ya Taifa ya Port Cambell mahali ambapo (1) meli inayoitwa “Loch Ard” iligonga tumbawe na (2) pango la Tom Pearce

[Picha zimeandaliea na]

Photography Scancolor Australia