Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuuchunguza Mwili Bila Kufanya Upasuaji

Kuuchunguza Mwili Bila Kufanya Upasuaji

Kuuchunguza Mwili Bila Kufanya Upasuaji

KWA sababu ya maendeleo ya kompyuta, hesabu, na sayansi, kuna mbinu zingine za kutibu magonjwa fulani badala ya kufanya upasuaji. Mbali na eksirei ambayo imetumika kwa zaidi ya miaka 100, sasa kuna tekinolojia nyingine kama vile eksirei ya kompyuta (CT scan), positron-emission tomography (PET scan), kupiga picha kwa nguvu za sumaku (MRI), na kupiga picha kwa kutumia mawimbi ya sauti au sonography. * Mbinu hizo zinafanyaje kazi? Zina madhara gani kwa afya? Na zina faida gani?

Eksirei

Inafanyaje kazi? Eksirei zina mawimbi mafupi kuliko yale ya mwangaza kwa hiyo, zinaweza kupenya tishu za mwili. Sehemu fulani ya mwili inapopigwa eksirei, tishu ngumu, kama vile, mifupa, hufyonza miale na kuwa na rangi nyangavu kwenye eksirei. Tishu nyepesi huonekana zikiwa na rangi ya kijivu. Mara nyingi eksirei hutumiwa kutambua matatizo au magonjwa ya meno, mifupa, matiti, na kifua. Ili kutofautisha kati ya tishu nyepesi zenye upana uleule, daktari anaweza kumdunga mgonjwa sindano yenye umaji-maji wa rangi fulani usiopenya miale ili kuonyesha tofauti. Siku hizi, eksirei huonekana kupitia kompyuta.

Madhara: Kuna uwezekano wa chembe na tishu kuharibiwa, lakini kwa kawaida madhara ni machache yakilinganishwa na faida. * Kabla ya kufanyiwa eksirei, wanawake wanapaswa kuwafahamisha madaktari wao ikiwa wao ni wajawazito. Pia huenda mtu akaathiriwa na rangi za kutofautisha tishu kama vile iodini. Hivyo, mwambie daktari au mtaalamu wako ikiwa unaathiriwa na iodini au chakula cha baharini ambacho huwa na iodini.

Faida: Picha za eksirei zinatokezwa haraka, kwa kawaida hazina maumivu, ni za bei rahisi, na zinapigwa kwa urahisi. Hivyo, zinafaa hasa kutumiwa kuchunguza matiti na matatizo ya dharura. Hakuna mnururisho unaobaki mwilini baada ya eksirei kupigwa, na hivyo kwa kawaida hakuna madhara. *

Eksirei ya Kompyuta

Inafanyaje kazi? CT scan ni eksirei ya hali ya juu zaidi iliyo na vipokezi vya pekee. Mgonjwa analala juu ya meza inayosukumwa ndani ya mashini fulani. Picha hutokezwa kupitia miale myembamba ya mnururisho na vipokezi vinavyomchunguza mgonjwa pande zote. Mbinu hiyo ni sawa na mtu anapokata mkate vipande vyembamba sana na kupiga kila kipande picha. Kompyuta huunganisha picha za “vipande” hivyo, na kumwonyesha daktari sehemu za ndani za mwili. Mashini za hivi karibuni huchunguza kila sehemu za mgonjwa na kupiga picha moja tu ya sehemu hizo zote na hivyo kurahisisha mambo. Kwa sababu CT scan zinachunguza viungo kwa undani, mara nyingi zinatumiwa kuchunguza kifua, tumbo, mifupa yote, na pia kansa mbalimbali na magonjwa mengine.

Madhara: Kwa kawaida CT scan zina mnururisho mwingi kuliko eksirei za kawaida. Kwa sababu hiyo, kuzitumia kunatokeza hatari zaidi ya kupata kansa, na hivyo mtu anapaswa kufikiria kwa uangalifu kabla ya kuzitumia akilinganisha pia faida yake. Wagonjwa fulani wanaathiriwa na rangi zinazotumiwa kutofautisha tishu ambazo kwa kawaida zinatia ndani iodini. Pia, wagonjwa fulani wanaweza kupata madhara ya figo kwa sababu ya kutumia CT scan. Ikiwa rangi za kutofautisha tishu zinatumiwa, mama anayenyonyesha huenda akahitaji kungoja kwa saa 24 au zaidi kabla ya kuanza kumnyonyesha mtoto.

Faida: CT scan hazina maumivu na ni picha zinazopigwa kutoka nje ya mwili, na zinaweza kuonyesha sehemu za ndani sana za mwili. Picha hizo zinatokezwa haraka na kwa urahisi, zinaweza kuokoa uhai kwa kuonyesha ikiwa viungo vya ndani vimeumia. Haziathiri vifaa vilivyoingizwa ndani ya mwili kwa sababu za kitiba.

Positron-Emission Tomography

Inafanyaje kazi? Ili mtu achunguzwe kupitia PET scan, umaji-maji wenye mnururisho huchanganywa na kemikali inayopatikana mwilini, hasa glukosi na kutiwa mwilini. Positron zinapotokezwa katika tishu picha huweza kupigwa. Chembe zenye kansa hutumia glukosi nyingi kuliko chembe za kawaida, hivyo zinavuta umaji-maji wenye mnururisho. Kwa sababu hiyo, tishu zilizoathiriwa hutokeza positron nyingi zaidi ambazo huonekana kwa rangi mbalimbali katika picha.

Ingawa CT scan na MRI scan huonyesha umbo na muundo wa viungo na tishu, PET scan zinaonyesha jinsi zinavyofanya kazi, na hivyo kuonyesha mabadiliko mapema zaidi. PET scan zinaweza kufanywa pamoja na CT scan, na hivyo kutokeza picha yenye mambo mengi zaidi. Hata hivyo, PET scan zinaweza kutokeza picha zisizo sahihi ikiwa mgonjwa alikula muda fulani kabla ya kupigwa eksirei hiyo au ikiwa kiwango cha sukari kwenye damu kimepanda, pengine kwa sababu ya kisukari. Pia, kwa sababu umaji-maji huo wenye mnururisho unaisha nguvu haraka, ni muhimu picha hiyo ipigwe haraka.

Madhara: Kwa kuwa umaji-maji unaotumiwa una kiasi kidogo cha mnururisho unaoisha nguvu haraka, hauathiri mtu sana. Lakini bado unaweza kuhatarisha kijusi. Kwa sababu hiyo, wanawake ambao ni wajawazito wanapaswa kuwafahamisha madaktari na wale wanaopiga eksirei. Wanawake ambao hawajapita umri wa kuzaa wanaweza kuomba wapimwe damu au mkojo ili kuchunguza ikiwa ni wajawazito. Ikiwa PET scan inatumiwa pamoja na CT scan, mtu anapaswa kufikiria madhara yanayotokana na CT scan.

Faida: Kwa sababu PET scan hazionyeshi tu umbo la viungo na tishu bali pia jinsi zinavyofanya kazi, eksirei hizo zinaweza kutambua matatizo kabla ya mabadiliko katika muundo wa tishu kuonekana kupitia eksirei ya CT au MRI.

Kupiga Picha kwa Nguvu za Sumaku (MRI)

Inafanyaje kazi? MRI hutumia nguvu za sumaku pamoja na mawimbi ya redio (si eksirei) na kompyuta kutokeza picha zenye mambo mengi sana za karibu viungo vyote mwilini. Matokeo huwawezesha madaktari wachunguze sehemu za mwili kwa undani zaidi na kutambua magonjwa kwa njia ambazo haziwezi kugunduliwa kupitia mbinu nyingine. Kwa mfano, MRI ni mojawapo ya vifaa vichache vinavyoweza kupiga picha hata ndani ya mifupa, na hivyo inafaa katika uchunguzi wa ubongo na tishu nyingine nyepesi.

Wagonjwa wanapaswa kutulia wanapochunguzwa kupitia MRI. Na kwa sababu picha inapigwa wakati mgonjwa anapoingizwa ndani ya mashini, watu fulani huwa na woga wa kuwa katika sehemu ndogo zilizofungwa. Hata hivyo, hivi karibuni MRI zilizo wazi zimebuniwa kwa ajili ya wagonjwa walio na woga wa aina hiyo au wanene. Kwa kawaida, vifaa vyenye chuma kama vile kalamu, saa, vito, pini za nywele, na zipu pia kadi za mkopo na vifaa vingine vinavyoweza kumuumiza mgonjwa au kuharibiwa na sumaku haviruhusiwi kwenye chumba cha kupigia MRI.

Madhara: Ikiwa rangi ya kutofautisha tishu inatumiwa, wagonjwa fulani wanaweza kuathiriwa, lakini rangi hiyo haina madhara mengi kama ile ya iodini inayotumiwa katika eksirei na CT scan. Mbali na hilo, MRI haina madhara mengine yanayojulikana. Hata hivyo, kwa sababu MRI ina sumaku zenye nguvu sana, wagonjwa wenye vifaa fulani vyenye chuma mwilini au waliojeruhiwa na visehemu vya chuma vikabaki mwilini hawawezi kupigwa picha hiyo. Hivyo, ikiwa daktari anapendekeza ufanyiwe MRI, unahitaji kumwambia daktari wako au mtaalamu wa MRI ikiwa una chuma chochote mwilini.

Faida: MRI haina mnururisho hatari, na ni nzuri katika kutambua magonjwa katika tishu, hasa zile ambazo zinaweza kufichwa na mfupa.

Sonography

Inafanyaje kazi? Kupiga picha kwa kutumia mawimbi ya sauti au sonography ni tekinolojia ya kupiga picha kwa kutumia mawimbi ya sauti yasiyoweza kusikiwa na wanadamu. Mawimbi yanapofika mahali kuna badiliko katika tishu, kwa mfano, mahali kuna kiungo, mawimbi huongezeka. Kompyuta hupima mawimbi na kuonyesha muundo wa kiungo, kama vile kina, ukubwa, na umbo lake. Mawimbi yenye sauti za chini husaidia kuchunguza sehemu za ndani kabisa za mwili; mawimbi yenye sauti za juu sana husaidia kuchunguza sehemu za juu za viungo kama vile macho na ngozi, labda hata kusaidia kutambua kansa ya ngozi.

Katika visa vingi, mtaalamu hutumia kifaa kinachoitwa transducer. Anapopaka mafuta juu ya ngozi, anasugua kifaa hicho juu ya eneo linalochunguzwa, na picha hutokea mara moja kwenye kompyuta. Inapohitajika transducer ndogo inaweza kuunganishwa na kifaa fulani na kuingizwa mwilini ili kuchunguza sehemu fulani za mwili.

Tekinolojia inayoitwa Doppler ultrasound hutambua kitu kinachosonga na inatumiwa kuchunguza jinsi damu inavyosonga. Hilo linaweza kusaidia kutambua magonjwa yanayohusiana na viungo na uvimbe ambao kwa kawaida huwa na mishipa mingi sana ya damu.

Mbinu hii ya kutumia mawimbi ya sauti husaidia madaktari kutambua magonjwa mbalimbali na kisababishi cha matatizo mbalimbali kama vile, magonjwa ya moyo, uvimbe katika matiti, au afya ya mtoto tumboni. Kwa upande mwingine, kwa kuwa mawimbi ya sauti hayawezi kupenya gesi, mbinu hiyo haifanyi kazi vizuri inapotumiwa katika sehemu fulani za tumbo. Pia, huenda picha isiwe wazi kama ile inayotolewa kupitia njia nyingine.

Madhara: Kwa kawaida mawimbi ya sauti yanapotumiwa vizuri hayana madhara, hata hivyo, yanaweza kudhuru tishu kutia ndani zile za kijusi. Kwa hiyo, huenda mawimbi ya sauti yakamdhuru mama mjamzito.

Faida: Tekinolojia hii inatumiwa katika sehemu nyingi, si lazima mgonjwa afanyiwe upasuaji, na ni mbinu isiyogharimu sana. Pia, picha hutokezwa mara moja.

Tekinolojia za Wakati Ujao

Kwa sasa, inaonekana kwamba uchunguzi mwingi unaofanywa unakazia fikira kuboresha tekinolojia zilizopo. Kwa mfano, watafiti wanajaribu kubuni MRI ambayo haitumii nguvu nyingi za sumaku na hivyo kupunguza gharama sana. Tekinolojia mpya ambayo sasa inabuniwa inaitwa molecular imaging (MI). Imekusudiwa kutambua mabadiliko mwilini katika molekuli, MI inatarajiwa kugundua magonjwa mapema sana.

Tekinolojia ya kutumia eksirei imepunguza uhitaji wa kufanyiwa upasuaji mwingi ulio hatari, na usiohitajika. Na eksirei inaposaidia kutambua na kutibu magonjwa mapema, matokeo huwa bora. Hata hivyo, vifaa vinavyotumiwa ni vya bei ghali sana, hata mashini nyingine zinagharimu mamilioni ya dola.

Bila shaka, ni jambo bora kuzuia magonjwa badala ya kuyatibu. Hivyo, jaribu kudumisha afya nzuri kupitia lishe bora, mazoezi ya kawaida, mapumziko ya kutosha, na mtazamo unaofaa wa akili. “Moyo wenye shangwe ni dawa nzuri,” inasema Methali 17:22.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Mbinu zote zilizotajwa zinahusisha kupiga picha viungo vya ndani vya mwili.

^ fu. 5 Ili ulinganishe vipimo vya mnururisho, ona sanduku  “Unapatwa na Mnururisho Kadiri Gani?”

^ fu. 6 Makala hii inataja tu kijuujuu mbinu mbalimbali, madhara, na faida. Kwa habari zaidi, tafadhali chunguza vichapo vya wataalamu au uzungumze na mpiga-picha za eksirei.

[Sanduku katika ukurasa wa 13]

 UNAPATWA NA MNURURISHO KADIRI GANI?

Kila siku tunapatwa na kiwango fulani cha mnururisho iwe kinatoka kwa miale inayotoka angani au kutoka kwa vitu vya asili vinavyotoa mnururisho kama vile gesi ya radoni. Vipimo vilivyo hapa chini vitakusaidia kuona hatari zinazohusianishwa na uchunguzi mbalimbali wa kitiba. Viwango vya mnururisho hupimwa kwa millisievert (mSv).

Kusafiri kwa saa tano kwa ndege: 0.03 mSv

Kukaa mahali penye mnururisho wa asili kwa siku kumi: 0.1 mSv

Eksirei moja ya meno: 0.04-0.15 mSv

Eksirei moja ya kawaida ya kifua: 0.1 mSv

Eksirei ya matiti: 0.7 mSv

CT scan ya kifua: 8.0 mSv

Ukihitaji kufanyiwa uchunguzi, usisite kumwuliza daktari wako au mtaalamu wa kupiga eksirei akupe habari hususa kuhusu kiwango cha mnururisho utakachopata au maswali mengine ambayo huenda ukataka kujibiwa.

[Picha katika ukurasa wa 11]

Eksirei

[Picha katika ukurasa wa 12]

CT

[Hisani]

© Philips

[Picha katika ukurasa wa 12]

PET

[Hisani]

Courtesy Alzheimer’s Disease Education and Referral Center, a service of the National Institute on Aging

[Picha katika ukurasa wa 13]

MRI

[Picha katika ukurasa wa 14]

Sonography