Nyavu Zimekauka
Nyavu Zimekauka
“Kuna miaka ambayo tumevua samaki wengi na miaka ambayo tumevua wachache, lakini sijawahi kuona ukosefu mkubwa wa samaki kama ilivyo sasa,” anasema George mwenye umri wa miaka 65 ambaye huvua katika pwani ya kaskazini-mashariki ya Uingereza. “Samaki wote wamekwisha, iwe ni samoni, samaki weupe, chewa, kamba-mti, yaani, hakuna samaki kabisa.”
SI George peke yake anayehangaishwa; ripoti kama hizo zimepokewa kutoka kwa wavuvi sehemu zote duniani. Huko Peru, Agustín ni kapteni wa mashua ya uvuvi yenye uzito wa tani 350. Anasema hivi: “Ukosefu wa dagaa ulianza miaka 12 iliyopita. Nchini Peru kulikuwa na samaki wengi sana mwaka wote, lakini sasa mara nyingi hatuna kazi ya kufanya kwa miezi mingi. Zamani hatukuwa tukisafiri zaidi ya kilomita 25 kutoka ufuoni, lakini sasa tunalazimika kusafiri kilomita 300 hivi ili kuvua.”
Antonio anayeishi huko Galicia, Hispania, anasema: “Nimekuwa nikivua samaki kwa zaidi ya miaka 20. Polepole, nimeona samaki wakipungua baharini. Tunavua samaki wengi kuliko bahari inavyoweza kutokeza.”
Madhara ya bahari zilizovuliwa samaki kupita kiasi hayawezi kuonekana kwenye picha kama madhara ya misitu iliyokatwa. Onyo lililotolewa hivi majuzi na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa kuhusu kuvua samaki kupita kiasi lilisema hivi: “Hali ni mbaya sana, yenye kutisha kwa kuwa asilimia 75 hivi ya maeneo ya uvuvi ulimwenguni tayari yanatumiwa kikamili, au hata yamevuliwa kupita kiasi.”
Asilimia 20 ya watu ulimwenguni hupata protini kutoka kwa samaki. Kwa hiyo, mojawapo ya vyakula muhimu kwa wanadamu vinaelekea kutoweka. Si bahari zote zilizo na samaki wengi. Kwa kweli, bahari nyingi ni kama jangwa. Samaki wengi hupatikana karibu na pwani, na mahali ambapo maji yana virutubisho. Virutubisho hivyo
huliwa na mwani wadogo ambao huliwa na samaki. Ni katika njia gani wavuvi wanaharibu maeneo ya uvuvi ambayo wao hutegemea ili kupata riziki? Historia ya eneo moja la uvuvi itatusaidia kuelewa mambo fulani yanayochangia hali hiyo.Eneo la Grand Banks—Uharibifu Unaanza
Baharia na mvumbuzi aliyeitwa John Cabot * aliyezaliwa nchini Italia alipovuka Bahari ya Atlantiki kutoka Uingereza na kuvumbua eneo la uvuvi la Grand Banks, katika eneo lenye maji yasiyo na kina kwenye pwani ya Kanada, jambo linalofanana na harakati za kutafuta dhahabu lilitukia. Jambo hilo lilitukia miaka mitano baada ya safari ya kihistoria ya Christopher Columbus mnamo 1492. Punde si punde, mamia ya wavuvi walijasiria kuvuka Bahari ya Atlantiki ili wakavue samaki katika eneo la Grand Banks. Hakuna mtu hata mmoja kutoka Ulaya aliyekuwa ameona chewa wengi hivyo.
Samaki aina ya chewa walikuwa na thamani kama dhahabu. Walipendwa kwa sababu ya nyama yao nyeupe iliyo na kiwango kidogo cha mafuta, na bado wanapendwa sana na watu duniani pote. Kwa kawaida, chewa katika Bahari ya Atlantiki huwa na uzani wa kati ya kilogramu 1.4 hadi 9, lakini chewa wa eneo la Grand Banks walikuwa na ukubwa kama wa binadamu. Katika karne zilizofuata, wavuvi waliongeza idadi ya samaki waliovua walipoendelea kujifunza kutumia nyavu za kukokotwa, na nyaya zenye maelfu ya ndoana.
Madhara ya Biashara ya Uvuvi
Kufikia karne ya 19, baadhi ya watu huko Ulaya walianza kuwa na wasiwasi kuhusu kupungua kwa samaki, hasa heringi. Hata hivyo, Profesa Thomas Huxley, msimamizi wa Shirika la Royal la Uingereza, alitangaza hivi katika Maonyesho ya Kimataifa ya Uvuvi huko London mnamo 1883: “Kuna samaki wengi sana kwa kulinganisha na idadi tunayovua . . . Hivyo, naamini kwamba maeneo ambako chewa wanavuliwa . . . na pengine maeneo mengine makubwa ya uvuvi yana samaki wengi sana.”
Watu wengi walikubaliana na maoni ya Huxley hata baada ya meli za mvuke kuanza kutumiwa na wavuvi katika eneo la Grand Banks. Chewa walinunuliwa kwa wingi hasa baada ya 1925 wakati Clarence Birdseye wa Massachusetts, Marekani, alipogundua mbinu ya kugandisha samaki haraka. Wakitumia nyavu zilizokokotwa na meli za dizeli, wavuvi walitumia mbinu hiyo ya kugandisha samaki haraka na kuvua samaki wengi zaidi. Lakini mambo yalikuwa bado.
Mnamo 1951, meli fulani isiyo ya kawaida kutoka Uingereza ilikuja kuvua samaki kwenye eneo la Grand Banks. Ilikuwa na urefu wa mita 85 na ingeweza kubeba vitu vyenye uzito wa tani 2,600. Hii ilikuwa ndiyo meli ya kwanza ya uvuvi ulimwenguni ambayo iligandisha na kupakia samaki mara tu walipovuliwa. Ilikuwa na sehemu iliyoinuka upande wa nyuma ambako winchi zilivuta wavu mkubwa sana, na kwenye sehemu zake za chini ilikuwa na mashini za kukata na kugandisha samaki. Ikitumia rada na mashini za kunasa sauti, kwa majuma mengi, usiku na mchana, meli hiyo ingeweza kutambua mahali ambapo kulikuwa na samaki wengi sana.
Mataifa mengine yalitambua faida za kifedha ambazo yangeweza kupata, na upesi mamia ya meli kama hiyo zilikuwa zikivua tani 200 hivi za
samaki kwa saa moja. Baadhi ya meli hizo zingeweza kubeba uzito wa tani 8,000 na zilikuwa na nyavu kubwa hivi kwamba zingeweza kufunika ndege kubwa sana ya abiria.Pigo la Mwisho
“Mwishoni mwa miaka ya 1970,” kinasema kitabu Ocean’s End, “watu wengi bado walikuwa wakijipumbaza kwamba samaki hawawezi kwisha baharini.” Idadi iliyokuwa ikiongezeka ya mashua kubwa za kuvulia zilitumiwa huko Grand Banks katika miaka ya 1980. Wanasayansi walionya kwamba chewa walikuwa karibu kutoweka. Lakini maelfu ya watu wakati huo walikuwa wakitegemea uvuvi ili kupata riziki, na wanasiasa waliogopa kufanya uamuzi usiopendwa na wengi. Mwishowe, mnamo 1992, wanasayansi walionyesha kwamba katika miaka 30 idadi ya chewa ilipungua kwa asilimia 98.9. Kuvua chewa huko Grand Banks kulipigwa marufuku. Lakini ilikuwa kuchelewa mno. Miaka 500 baada ya kugunduliwa, karibu samaki wote katika mojawapo ya maeneo yenye samaki wengi zaidi ulimwenguni walikuwa wamevuliwa kabisa.
Wavuvi walitazamia kwamba idadi ya chewa ingeongezeka. Lakini chewa huishi kwa zaidi ya miaka 20 na wanakomaa polepole. Tangu 1992, bado idadi yao haijaongezeka.
Tatizo la Ulimwenguni Pote la Uvuvi
Jambo lililotukia huko Grand Banks ni tatizo linaloipata biashara ya uvuvi ulimwenguni pote. Mnamo 2002, waziri wa mazingira wa Uingereza alisema kwamba “asilimia 60 ya samaki ulimwenguni wanakaribia kumalizwa.” Baadhi ya samaki wanaokabili hatari ya kutoweka ni tuna, chuchunge, papa, na rockfish.
Tayari nchi nyingi zilizoendelea zimevua samaki kupita kiasi katika maeneo yao ya uvuvi na sasa wanajaribu kuvua katika maeneo mengine. Kwa mfano, pwani ya Afrika ni mojawapo ya maeneo yenye samaki wengi sana duniani. Watawala wengi wa nchi za Afrika hawawezi kukataa kuyapa mataifa ya kigeni leseni za uvuvi kwa sababu biashara hiyo ni chanzo cha pesa za kigeni kwa serikali za Afrika. Haishangazi kwamba wenyeji wanachukizwa na tendo hilo ambalo linamaliza samaki wao.
Kwa Nini Samaki Wanavuliwa Kupita Kiasi?
Kwa mtu asiyehusika, huenda suluhisho likawa kuzuia watu wasivue kupita kiasi. Lakini jambo hilo si rahisi. Wavuvi huwa na vifaa vya bei ghali. Hivyo, kila mvuvi anatumaini kwamba wengine wataacha kuvua ili yeye aendelee. Kwa sababu hiyo, uvuvi unaendelea. Isitoshe, serikali zinajihusisha sana katika uvuvi, na hivyo wanachangia tatizo hilo. Gazeti Issues in Science and Technology linasema: “Kwa kawaida mataifa yaliona miradi [ya UM] ya kuhifadhi samaki kuwa kanuni za kufuatwa na mataifa mengine lakini mataifa hayo yenyewe hayakuona umuhimu wa kuzifuata.”
Pia, wavuvi wanaovua ili kujifurahisha hushiriki katika kuangamiza samaki. Likiripoti kuhusu uchunguzi uliofanywa Marekani, jarida New Scientist lilisema hivi: “Uvuvi wa kujifurahisha unachangia asilimia 64 ya samaki waliovuliwa kupita kiasi katika Ghuba ya Mexico.” Kwa kuwa watu wanaovua ili wajifurahishe au kwa ajili ya biashara wana uvutano wenye nguvu, wanasiasa hufanya jambo linalowafanya wapendwe na watu kuliko kufanya jambo linalosaidia kuhifadhi samaki.
Je, samaki wanaweza kuhifadhiwa? Boyce Thorne-Miller anasema hivi katika kitabu chake The Living Ocean: “Hakuna kitu hususa kinachoweza kuhifadhi viumbe baharini ikiwa mitazamo ya wanadamu haibadiliki.” Inafurahisha kwamba Muumba wetu, Yehova Mungu, amesimamisha Ufalme ambao utahakikisha usalama wa wakati ujao wa dunia yote.—Danieli 2:44; Mathayo 6:10.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 8 John Cabot alizaliwa huko Italia, ambako aliitwa Giovanni Caboto. Alihamia Bristol, Uingereza, katika miaka ya 1480, na akiwa huko alifunga safari yake ya mwaka wa 1497.
[Blabu katika ukurasa wa 21]
Kama misitu iliyokatwa, bahari zilizovuliwa kupita kiasi zimeharibiwa
[Blabu katika ukurasa wa 22]
“Asilimia 75 hivi ya maeneo ya uvuvi ulimwenguni tayari yanatumiwa kikamili, au hata yamevuliwa kupita kiasi.”—Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa
[Blabu katika ukurasa wa 23]
Asilimia 20 ya watu ulimwenguni hupata protini hasa kutoka kwa samaki
[Picha katika ukurasa wa 23]
Kambodia
[Picha katika ukurasa wa 23]
Biashara ya uvuvi huko Alaska
[Picha katika ukurasa wa 23]
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]
© Janis Miglavs/DanitaDelimont.com
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]
Top: © Mikkel Ostergaard/Panos Pictures; middle: © Steven Kazlowski/SeaPics.com; bottom: © Tim Dirven/Panos Pictures