Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ Ni asilimia 8 tu ya idadi ya watu nchini Ujerumani wanaofikiri kwamba ile sehemu muhimu zaidi ya usiku wa kuamkia Krismasi ni ya kidini. Mnamo 1980, idadi hiyo ilikuwa asilimia 47.—KITUO CHA HABARI CHA TV N24, UJERUMANI.
▪ “Kwa mara ya kwanza katika historia ya [Marekani], zaidi ya mtu mmoja kati ya Wamarekani 100 yuko gerezani . . . Nchini kote, idadi ya watu walio gerezani ni karibu milioni 1.6.”—THE NEW YORK TIMES, MAREKANI.
▪ Uchunguzi mmoja umeonyesha kwamba “asilimia 100 ya Wahispania waliochunguzwa” walikuwa na angalau aina moja ya kemikali za kuua wadudu mwilini, yaani, “vitu ambavyo vinatambulika ulimwenguni pote kuwa hatari kwa afya ya binadamu.”—CHUO KIKUU CHA GRANADA, HISPANIA.
▪ “Katika nchi zinazoweka rekodi, mapato ya kodi kutoka kwa tumbaku ni zaidi ya mara 500 pesa zinazotumiwa kuzuia matumizi ya tumbaku.”—SHIRIKA LA AFYA ULIMWENGUNI, USWISI.
▪ Idadi ya Waislamu imezidi ile ya Wakatoliki. Mnamo 2006, ulimwenguni pote kulikuwa na asilimia 19.2 ya Waislamu na asilimia 17.4 ya Wakatoliki.—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, UINGEREZA.
Tiara Yasaidia Kuvuta Meli
Kwa sababu ya kuongezeka kwa bei ya mafuta na athari kwa mazingira, wamiliki wa meli wanatafuta njia za kupunguza matumizi ya mafuta na moshi unaosababishwa na mafuta hayo. Na wanatumia njia ya zamani, yaani, upepo. Njia moja ambayo imejaribiwa ni ile ya kutumia tiara kuvuta meli, linaripoti gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung. Tiara hiyo iliyo umbali wa mita 300 angani, inasukumwa na upepo na hivyo kumsaidia kapteni apunguze matumizi ya injini. Hivi karibuni, tiara moja yenye ukubwa wa mita 160 za mraba ilitumiwa kuvuta meli ya mizigo iliyokuwa ikivuka Bahari ya Atlantiki.
Kustahimili Ukame
“Kiwavi wa mdudu fulani anayepatikana Afrika hustahimili ukame kwa kujigeuza kuwa na ugumu kama wa peremende,” linasema gazeti Science News. Anapoishiwa kabisa na maji, kiwavi wa mdudu Polypedilum vanderplanki hugeuza maji yaliyo katika chembe zake kuwa kitu fulani kinachofanana na sukari iliyoyeyushwa inapogandamana. Akiwa katika hali hiyo, mfumo wa kumeng’enya wa kiwavi huyo huacha kufanya kazi kabisa. Anaweza kukaa katika “hali ya kutotenda” kwa muda mrefu hata kufikia miaka 17, hadi mvua inayofuata itakaponyesha na kumfanya aanze kutenda tena.
Mahali Bora pa Kuchunguza Nyota
Kikundi fulani cha kimataifa kimeanzisha kituo cha kuchunguza nyota kinachoendeshwa na roboti huko Dome Argus. Kituo hicho kiko mita 4,000 juu ya usawa wa bahari na ndilo eneo lililoinuka zaidi kwenye nyanda za Mashariki ya Antaktiki. Kikiwa umbali wa kilomita 1,000 hivi kutoka Ncha ya Kusini, kituo hicho kina baridi sana na giza sana. Kina hewa kavu, iliyotulia na mwangaza wa jua unaweza kukosa kuonekana kwa miezi minne mfululizo. Inasemekana kuwa Dome Argus ndipo mahali bora zaidi duniani pa kuchunguza nyota. Kwa kutumia darubini, anasema Lifan Wang, msimamizi wa Kituo cha Wachina cha Antaktiki cha Kuchunguza Nyota, “inawezekana kupata picha kama zile zinazopigiwa angani bila kutumia pesa nyingi kama zile za kupeleka darubini angani.”