Nimejionea Mabadiliko Makubwa Nchini Korea
Nimejionea Mabadiliko Makubwa Nchini Korea
Limesimuliwa na Chong-il Park
“Mwoga! Unaogopa kufa vitani. Unajaribu kuepuka kuingia jeshini kwa kudai kwamba una sababu za kidini.” Hivyo ndivyo kapteni wa Shirika la Upelelezi la CIC alivyoniambia nilipokuwa mbele yake mnamo Juni (Mwezi wa 6) 1953, zaidi ya miaka 55 iliyopita.
HILO lilitokea wakati wa Vita vya Korea. Kisha kapteni huyo akatoa bastola na kuiweka juu ya dawati. “Sasa, utakufa papa hapa badala ya kule vitani,” akasema. “Ungependa kubadilisha mawazo yako?”
“Hapana,” nilijibu kwa uthabiti. Kwa hiyo, kapteni akamwamuru ofisa mmoja ajitayarishe kuniua.
Nilijikuta katika hali hiyo kwa sababu nilikuwa nimeamriwa nitumike jeshini, lakini nikakataa. Tulipokuwa tukisubiri nilimwambia kapteni kwamba tayari nilikuwa nimeweka maisha yangu wakfu kwa Mungu, hivyo niliamini kwamba haingekuwa sawa kudhabihu maisha yangu kwa sababu nyingine yoyote isipokuwa kwa utumishi wa Mungu. Kisha dakika kadhaa zilipita huku tukiwa tumenyamaza. Muda mfupi baadaye, ofisa huyo alirudi na kusema kwamba kila kitu kilikuwa tayari kwa ajili ya kuuawa kwangu.
Wakati huo, watu wengi huko Korea Kusini hawakujua mengi kuhusu Mashahidi wa Yehova. Pia hawakujua chochote kuhusu kukataa kwetu kushiriki katika mambo ya kijeshi ya serikali yoyote kwa sababu za kidini. Kabla ya kueleza kilichotukia baadaye, acheni nieleze jinsi nilivyofikia uamuzi niliomwambia kapteni.
Maisha Yangu ya Mapema
Nilizaliwa Oktoba (Mwezi wa 10) 1930, katika mji ulio karibu na Seoul, uliokuwa mji mkuu wa Korea nikiwa mwana wa kwanza wa familia yetu. Babu yangu alikuwa mfuasi shupavu wa Confucius, na alinizoeza katika dini hiyo. Alipinga nisiende shule, hivyo sikuhudhuria shule mpaka alipokufa nikiwa na umri wa miaka kumi. Kisha mnamo 1941, Japani na Marekani zilipigana katika Vita vya Pili vya Ulimwengu zikiwa katika pande tofauti.
Kwa kuwa Korea ilikuwa chini ya utawala wa Japani, kila asubuhi tukiwa shuleni tulishiriki katika sherehe ya kumtukuza maliki Mjapani. Shangazi na mjomba wangu walikuwa Mashahidi wa Yehova na walifungwa nchini Korea wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu kwa sababu, kwa msingi wa mafundisho ya kidini, walikataa kujihusisha na vita. Mashahidi waliteswa na Wajapani sana hivi kwamba baadhi yao walikufa, kutia ndani mjomba wangu. Baadaye, shangazi yangu aliishi pamoja na familia yetu.
Korea ilipata uhuru kutoka kwa Japani mnamo 1945. Nikisaidiwa na shangazi yangu na Mashahidi wengine walioachiliwa, nilianza kujifunza Biblia na nikabatizwa na kuwa mmoja wa
Mashahidi wa Yehova katika mwaka wa 1947. Mnamo Agosti (Mwezi wa 8) 1949, Don na Earlene Steele, wamishonari wa kwanza waliozoezwa katika Shule ya Gileadi (Watchtower Bible School of Gilead) kutumwa nchini Korea waliwasili Seoul. Baada ya miezi kadhaa, wamishonari wengine walitumwa.Januari 1, 1950 (1/1/1950), mimi na Wakorea wengine watatu tulianza kutumika kama mapainia, kama wahudumu wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova wanavyoitwa. Tulikuwa wa kwanza kuwa mapainia nchini Korea baada ya Vita vya Pili vya Ulimwengu.
Maisha Wakati wa Vita vya Korea
Jumapili (Siku ya Yenga) Juni 25, vita vilianza kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini. Wakati huo, nchi yote ya Korea ilikuwa na kutaniko moja tu la Mashahidi huko Seoul, likiwa na wahudhuriaji 61. Ubalozi wa Marekani uliwaagiza wamishonari wote watoke nchini humo kwa sababu ya usalama wao. Pia, Mashahidi wengi Wakorea walihama Seoul na wakasambaa kotekote katika sehemu ya kusini ya nchi.
Hata hivyo, serikali ya Korea Kusini iliwazuia vijana kama mimi wanaopaswa kuandikishwa jeshini kuhama Seoul. Ghafula, majeshi ya Wakomunisti yaliingia jijini na Seoul ikawa chini ya majeshi hayo. Hata katika kipindi hicho iliponibidi kujificha katika chumba kidogo kwa miezi mitatu, niliweza kuwahubiria watu kuhusu Ufalme wa Mungu. Kwa mfano, nilikutana na mwalimu aliyekuwa akijificha kutoka kwa Wakomunisti. Hatimaye, tulianza kuishi pamoja na nilijifunza naye Biblia kila siku. Baadaye alibatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova.
Mwishowe, maofisa Wakomunisti kutoka Korea Kaskazini walipata mahali tulipokuwa tumejificha. Tulijitambulisha kuwa wanafunzi wa Biblia na tukawafafanulia fundisho la Biblia kuhusu Ufalme wa Mungu. Kwa kushangaza, hawakutukamata na badala yake walipendezwa na ujumbe wa Biblia. Kwa kweli, baadhi yao walirudi tena mara kadhaa na walitaka kusikia mengi zaidi kuhusu Ufalme wa Mungu. Kisa hicho kiliimarisha imani yetu katika nguvu za Yehova za kulinda.
Majeshi ya Umoja wa Mataifa yalipodhibiti Seoul kwa mara nyingine, nilipewa ruhusa ya pekee ya kusafiri hadi jiji la Taegu mnamo Machi (Mwezi wa 3) 1951. Nikiwa huko, nilifurahia kuhubiri pamoja na Mashahidi wenzangu kwa miezi kadhaa. Kisha mnamo Novemba (Mwezi wa 11) 1951, kabla ya vita kwisha, Don Steele alirudi Korea.
Nilimsaidia kupanga tena kazi yetu ya kuhubiri. Mnara wa Mlinzi na Informant, zilizotoa mwongozo kwa Mashahidi kuhusu kazi ya kuhubiri, zilihitaji kutafsiriwa katika Kikorea, kupigwa chapa, na kutolewa nakala. Vichapo hivyo vilitumwa katika makutaniko yaliyokuwa katika majiji kadhaa. Mara kwa mara, mimi na Don tulisafiri pamoja kuyatembelea makutaniko ili kuyatia moyo.
Mnamo Januari 1953, nilifurahi kupokea barua iliyonialika kwenda kwenye Shule ya Gileadi huko New York ili nizoezwe kuwa mmishonari. Hata hivyo, baada ya kukata tikiti ya ndege, nilipata ujumbe kutoka kwa serikali ya Korea uliosema nijiunge na jeshi.
Hali ya Kufa na Kupona
Kwenye kituo cha kujiandikisha nilimweleza ofisa msimamo wangu wa kutounga mkono upande wowote katika mambo ya kisiasa na uamuzi wangu wa kutojiunga na jeshi. Kwa sababu hiyo, alinipeleka kwenye Shirika la Upelelezi la CIC ili wachunguze ikiwa mimi ni Mkomunisti. Hapo ndipo nilikabili hali ya kufa na kupona
niliyotaja awali. Lakini badala ya kunipiga risasi, kapteni huyo alisimama ghafula, akampa ofisa mmoja ubao mnene, na akamwamuru anipige. Ingawa nilihisi uchungu mwingi, nilifurahi kwamba nilifaulu kuvumilia.Maofisa wa CIC walinirudisha kwenye kituo cha kujiandikisha ambako maofisa, wakipuuza imani yangu, walinipa namba ya utambulisho wa kijeshi bila kujali, na wakanipeleka kwenye kituo cha kijeshi kwenye kisiwa cha Cheju, karibu na Korea bara. Asubuhi iliyofuata, wote waliokuwa wametoka tu kuandikishwa kutia ndani mimi, walipaswa kula kiapo ili wawe wanajeshi. Nilikataa kufanya hivyo. Kwa sababu hiyo, nilishtakiwa katika mahakama ya kijeshi na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani.
Maelfu Wadumisha Utimilifu
Siku niliyopaswa kuondoka kwa ajili ya shule ya wamishonari, niliona ndege ikipaa angani. Ilikuwa ndege niliyostahili kusafiri nayo. Badala ya kuvunjika moyo kwa sababu singeweza kwenda Gileadi, niliridhika sana kwani nilikuwa nikidumisha utimilifu wangu kwa Yehova. Mimi si Shahidi pekee aliyekataa kutumika jeshini nchini Korea. Kwa kweli, Mashahidi zaidi ya 13,000 wamefanya vivyo hivyo katika miaka iliyofuata. Wametumika kwa jumla ya miaka zaidi ya 26,000 katika magereza nchini Korea.
Baada ya kufungwa kwa miaka miwili ya kifungo changu cha miaka mitatu, nilisamehewa mnamo 1955 kwa sababu ya mwenendo wangu mzuri nikiwa mfungwa na nikaachiliwa. Nilirudia utumishi wangu wa wakati wote. Baadaye, mnamo Oktoba 1956, nilipata mgawo wa kutumika katika ofisi za Mashahidi wa Yehova huko Korea Kusini. Kisha, katika mwaka wa 1958, nilialikwa tena Gileadi. Baada ya kuhitimu, nilipewa mgawo nchini Korea.
Muda fulani baada ya kurudi Korea, nilikutana na In-hyun Sung, Shahidi mwaminifu, na tulioana Mei (Mwezi wa 5) 1962. Alikuwa amelelewa na wazazi Wabudha na alijifunza kuhusu Mashahidi kutoka kwa mwanafunzi mwenzake. Kwa miaka mitatu baada ya kuoana, tulitembelea kutaniko tofauti kila juma nchini Korea tukiwa na mradi wa kuwaimarisha washiriki wake kiroho. Tangu 1965, tumetumika katika ofisi ya tawi ya Mashahidi iliyoko kilomita 60 hivi kutoka Seoul.
Kukumbuka Mabadiliko
Nikitazama nyuma, ninashangaa kuona mabadiliko mengi ambayo yametokea katika nchi hii. Vita vya Pili vya Ulimwengu na vile vita dhidi ya Korea Kaskazini, vilisababisha uharibifu wa kiwango kikubwa nchini Korea Kusini. Barabara na majiji yaliachwa yakiwa magofu. Umeme haukupatikana kwa vipindi virefu. Na hali ya uchumi ilikuwa mbaya sana. Kwa miaka 50 iliyofuata, Korea Kusini imefanya maendeleo yenye kustaajabisha.
Leo, Korea Kusini ndiyo nchi ya 11 tajiri zaidi ulimwenguni. Inajulikana kwa majiji yake ya kisasa, magari-moshi ya kasi sana, vifaa vya elektroniki, na ujuzi wa kutengeneza magari. Sasa, Korea Kusini inaorodheshwa kuwa nchi ya tano inayotengeneza magari kwa wingi zaidi. Lakini jambo muhimu zaidi kwangu ni maendeleo ambayo yametukia nchini Korea Kusini kuhusu kuheshimu haki za raia.
Mnamo 1953, niliposimamishwa mbele ya mahakama ya kijeshi, serikali ya Korea haikuelewa kwa nini mtu angekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Baadhi yetu tulishtakiwa kuwa Wakomunisti, na Mashahidi wachache walipigwa mpaka wakafa. Wengi ambao walifungwa kwa sababu ya kukataa kuingia jeshini walipokuwa vijana wamewaona wana wao, na hata wajukuu wao, wakifungwa kwa sababu hiyohiyo.
Kwa miaka michache iliyopita, vyombo vya habari vimeangazia visa vya Mashahidi wa
Yehova wanaokataa kujiunga na jeshi la nchi yoyote kwa sababu ya dhamiri zao. Wakili mmoja aliyekuwa amemshtaki Shahidi fulani aliyekataa kujiunga na jeshi, aliandika barua ya kuomba msamaha ambayo ilichapishwa katika gazeti moja maarufu.Ninatumaini kwamba haki yetu ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri itaheshimiwa nchini Korea Kusini kama inavyoheshimiwa katika nchi nyingine nyingi. Ninasali kwamba serikali ya Korea Kusini haitawasumbua watu walio na imani kama yangu na kukomesha zoea la kuwafunga vijana wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, “ili tuendelee kuishi maisha shwari na matulivu.”—1 Timotheo 2:1, 2.
Tukiwa watumishi wa Mungu wetu, Yehova, tunathamini nafasi za kutetea haki yake ya kuwa Mtawala wetu. (Matendo 5:29) Tamaa yetu ya kutoka moyoni ni kuufurahisha moyo wake kwa kuwa waaminifu kwake. (Methali 27:11) Ninafurahia kuwa miongoni mwa mamilioni ambao wamechagua ‘kumtegemea Yehova kwa moyo wao wote na kutotegemea uelewaji wao wenyewe.’—Methali 3:5, 6.
[Blabu katika ukurasa wa 13]
“Kwa kushangaza, hawakutukamata na badala yake walipendezwa na ujumbe wa Biblia”
[Blabu katika ukurasa wa 14]
Mashahidi Wakorea wamefungwa kwa jumla ya miaka 26,000 kwa kukataa kuingia jeshini
[Picha katika ukurasa wa 12]
Nikiwa katika gereza la jeshi, 1953
[Picha katika ukurasa wa 15]
Kutembelea makutaniko pamoja na Don Steele wakati wa vita, 1952
[Picha katika ukurasa wa 15]
Kabla ya arusi yetu, 1961
[Picha katika ukurasa wa 15]
Nilimsaidia mwangalizi anayesafiri kwa kumtafsiria, 1956
[Picha katika ukurasa wa 15]
Nikiwa na In-hyun Sung leo