Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Watafutaji wa Chumvi wa Sahara

Watafutaji wa Chumvi wa Sahara

Watafutaji wa Chumvi wa Sahara

VIGINGI vinaonekana kando ya barabara gari letu linapopita. Vigingi hivyo vinaonyesha njia wakati kuna dhoruba za mchanga. Kwa kweli, dhoruba kama hizo zinatokea mara nyingi katika Jangwa la Sahara.

Barabara tunayofuata ndiyo iliyotumiwa na ngamia zamani na inaunganisha jiji la Agadez lililo katika eneo la kaskazini la Niger na mpaka wa Algeria na mbali zaidi. Tunaelekea kwenye kijiji kidogo cha Teguidda-n-Tessoumt eneo lililo kilomita 200 kaskazini-magharibi ya Agadez. Huko familia 50 zinatumia utamaduni wa muda mrefu wa kutafuta chumvi kutoka kwenye udongo wa Sahara.

Vilima na Vidimbwi vya Chokaa

Mbele yetu tunaona vilima vidogo kwenye jangwa vinavyoonyesha tunakoenda. Mtu anayetuongoza anaegesha gari karibu na kilima chenye urefu wa mita 10 na anatuambia tushuke na kupanda kilima hicho ili tuone kijiji. Tunapokipanda, anatueleza kwamba kilima hicho pamoja na vilima vingine kama hivyo vimetengenezwa na wanadamu na ni mabaki ya miaka mingi ya kutokeza chumvi katika eneo hilo.

Kutoka juu ya kilima hicho, mandhari ni yenye kuvutia sana. Karibu kila kitu katika kijiji kilicho chini kina rangi ya udongo kuanzia chini, kuta, hata paa. Tofauti peke yake ni rangi ya kijani kwenye majani ya miti miwili iliyo kwenye miisho miwili ya mji huo. Ua na nyumba zenyewe zimetengenezwa kwa udongo. Majengo hayo yana rangi moja ambayo ni tofauti sana na rangi ya chokaa katika mamia ya vidimbwi vya chumvi. Eneo hilo lina shughuli nyingi kwa sababu wanaume, wanawake, na watoto wote wanafanya kazi kwa bidii.

Njia ya Pekee ya Kutokeza Chumvi

Tunapoteremka kutoka kilima hicho, mtu anayetutembeza anatueleza njia ya zamani ya kutokeza chumvi iliyotumiwa na wanakijiji. “Kwa kweli, kuna aina mbili za vidimbwi,” anasema. “Vidimbwi vikubwa vyenye mzingo wa mita mbili vinatumiwa kugawa maji kutoka kwa chumvi. Vidimbwi vidogo vinatumiwa kuvukiza. Maji kutoka chemchemi 20 katika eneo hilo yamekolea chumvi. Hata hivyo, chumvi nyingi haitolewi kwenye maji bali kwenye udongo na hilo ndilo jambo la pekee kuhusu njia hii ya kutokeza chumvi.” Chumvi hiyo inatolewa udongoni jinsi gani?

Tunamwona mtu akijaza udongo kwenye kidimbwi kikubwa kilichojaa maji yaliyotoka kwenye chemchemi. Anakanyaga mchanganyiko huo, kana kwamba anakanyaga shinikizo la divai. Anaporidhika na kazi yake, anaacha mchanganyiko huo utulie kwa saa kadhaa. Vidimbwi vikubwa vilivyojaa mchanganyiko huohuo vimemzunguka. Kila kidimbwi kina rangi tofauti ya kahawia kwani rangi inabadilika udongo unapotulia.

Hapo karibu, mwanamume mwingine anateka maji ya chumvi kutoka kwenye kidimbwi akitumia nusu kibuyu na kumwaga mchanganyiko huo ndani ya vidimbwi vidogo. Kwa kawaida wanaume ndio hufanya kazi hiyo. Wanaume pia ndio hutunza vidimbwi hivyo. Vidimbwi fulani ni mashimo yaliyojitokeza yenyewe na vingine vimechimbwa katika mwamba. Wakati hawawezi kuchimba, wanaume hao wanaweka udongo kwa muundo wa mviringo juu ya mwamba. Wanatengeneza ukuta huo wa udongo wakitumia mikono na kuugonga-gonga kwa mti mpaka ukauke. Ni lazima vidimbwi hivyo virekebishwe na kujengwa upya kila mwaka.

Wanawake hufanya kazi gani? Wao ndio wanaobeba vitu vizito, wakihakikisha kwamba nyakati zote kuna udongo wenye chumvi karibu na vidimbwi. Pia wanatoa chembechembe za chumvi kutoka kwenye vidimbwi vya kuvukizia. Kisha wao husafisha vidimbwi kabisa na kuvitayarisha kwa ajili ya kazi tena.

Wakati huo, watoto hukimbia kandokando ya vidimbwi vidogo. Kazi yao ni kuchunguza jinsi chembechembe hizo zinavyokauka. Maji yanapovukizwa kutoka kwenye vidimbwi, chembechembe hujitokeza juu yake. Zikiachiliwa zitazuia uvukizaji zaidi. Kwa hiyo, watoto hunyunyiza matone ya maji ili kuvunja tabaka hilo na kufanya chembechembe hizo hushuka na kutulia kwenye sakafu ya kidimbwi. Uvukizaji huendelea hadi mwishowe ni chumvi peke yake inayobaki.

Kwa nini vidimbwi huwa na rangi nyingi maridadi? Mtu anayetutembeza anaeleza: “Kuna aina tatu za matope katika eneo hili, na kila aina hufanya maji yawe na rangi ya pekee. Isitoshe, rangi hutofautiana kwa kutegemea kiasi cha chumvi majini. Pia, mwani unakua katika baadhi ya vidimbwi hivyo na kuongeza rangi.” Tunagundua kwamba vidimbwi hivyo vinageuka rangi jua linaposonga.

Chumvi Inatumiwa Kama Pesa

Huko kijijini, wanawake wanatengeneza chembechembe za chumvi kwa muundo wa mkate au keki na kuziacha zikauke kwenye jua. Keki hizo zinabaki na rangi ya kahawia. Tunawaona wanawake wakitengeneza keki kwa muundo wa pia, mviringo, na pembetatu. Mwanamke mmoja anatueleza kwamba keki zenye muundo wa pia na mviringo zinauzwa, na zile zenye muundo wa pembetatu zinatumiwa kama zawadi.

Ni nani wanaonunua chumvi? Wahama-hamaji na wafanyabiashara wa chumvi. Wao hupitia Teguidda-n-Tessoumt wakibadilishana chakula na bidhaa nyingine ili wapate chumvi. Chumvi nyingi huuzwa kwenye soko za miji mikubwa kandokando ya jangwa. Chumvi kutoka kijiji hicho haitumiwi na wanadamu. Badala yake, inaongezewa kwa chakula cha wanyama.

Tunaporudi kwenye gari letu, tunamwona mwanamume akichimba matope yaliyobaki kwenye kidimbwi cha kutenganisha maji na chumvi. Anamwaga matope hayo kwenye eneo fulani na kuongeza ukubwa wa kilima kimoja. Tunapoondoka tunafikiri kuhusu vilima hivyo ambavyo vinaonyesha vizazi vingi vya watafutaji wa chumvi ambao wameishi, wakafanya kazi, na kufa katika eneo la Teguidda-n-Tessoumt.—Tumetumiwa makala hii.

[Blabu katika ukurasa wa 22]

“Chumvi nyingi haitolewi kwenye maji bali kwenye udongo na hilo ndilo jambo la pekee kuhusu njia hii ya kutokeza chumvi”

[Ramani katika ukurasa wa 21]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

SAHARA

NIGER

Agadez

Teguidda-n-Tessoumt

Picha zimeandaliwa na]

Based on NASA/Visible Earth imagery

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kutokeza chumvi kutoka kwenye udongo wa Sahara

[Hisani ya Picha]

© Victor Englebert

[Picha katika ukurasa wa 23]

Vidimbwi vya uvukizaji huwa na rangi nyingi

[Hisani ya Picha]

© Ioseba Egibar/age fotostock

[Picha katika ukurasa wa 23]

Vipande vya chumvi vikikaushwa katika jua