Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Baiskeli Inayonoa Visu

Baiskeli Inayonoa Visu

Baiskeli Inayonoa Visu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI TANZANIA

▪ Ikiwa ungemwona mwanamume ameketi juu ya baiskeli akitazama kuelekea upande wa nyuma, akizungusha pedali kwa nguvu lakini hasongi hata kidogo, ungefikiria nini? Katika sehemu fulani za dunia, kama Afrika Mashariki, huenda ukawa unamtazama mnoa-visu ambaye anatimiza huduma muhimu.

Baiskeli ya mtu huyo ni ya kawaida lakini imekarabatiwa kwa njia mbalimbali. Jiwe la kusagia la mviringo linawekwa kwenye sehemu ya kubeba mizigo. Mshipi unaozungusha jiwe la kusagia uliotengenezwa kwa nailoni umefungwa kwenye kiunzi cha gurudumu la ziada la baiskeli ambalo limegawanywa mara mbili na kuchomelewa kwenye gurudumu la nyuma la baiskeli.

Haijulikani jinsi kifaa hicho kilivyofika barani Afrika. “Nimeambiwa kwamba baiskeli hizi zilitumika Dar es Salaam, kabla ya wazo hili kufika mji wa Moshi ninakoishi,” anasema Andrea ambaye amenoa visu kwa njia hiyo tangu 1985. “Wazo hilo lilianza kutumika huku katika mwaka wa 1982,” anasema.

Mtu anaweza kupata baiskeli ya kunoa visu jinsi gani? Andrea anaeleza, “Tunakwenda kwa fundi . . . na kumwomba abadilishe baiskeli ya kawaida kuwa ya kunolea kulingana na maelekezo na vipimo vyetu.” Baiskeli itakuwa tayari baada ya siku moja au mbili.

Cheche na Jasho!

Andrea huanza kazi yake asubuhi saa moja hivi anapopanda baiskeli yake na kuelekea eneo lenye watu wengi. Anapofika, anapaaza sauti na kusema: “Kunoa! Kunoa!” Pia yeye hupiga kengele ya baiskeli yake. Muda si muda, mama mmoja anaonekana dirishani. Anamwita Andrea na kumpa visu kadhaa butu. Jirani yake analeta upanga, na kinyozi analeta makasi yake. Pia Andrea hunoa majembe, kekee, na kitu chochote kilicho na makali.

Andrea hutafuta mahali tambarare na kutumia kifaa cha kusimamisha baiskeli yake na hivyo kuinua gurudumu la nyuma. Kisha anaunganisha mshipi wa nailoni, anaketi kwenye kiti kilichoelekezwa upande wa nyuma, na anaanza kuzungusha pedali. Cheche zinaruka na anatokwa na jasho anaponoa vitu mbalimbali. Jioni saa kumi na mbili hivi, Andrea anafunga kazi yake.

Mfano huo wa kunoa visu kwa kutumia baiskeli ni njia moja tu inayoonyesha jinsi watu “wenye bidii” wanavyoweza kutumia maarifa ili kujipatia riziki kwa njia halali hata chini ya hali ngumu za kiuchumi.—Methali 13:4.