Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maji Yanaendeleza Uhai

Maji Yanaendeleza Uhai

Maji Yanaendeleza Uhai

MAJI ni fumbo. Maji yamefanyizwa kwa njia rahisi na pia iliyo tata. Kila molekuli ina atomu tatu peke yake, mbili za hidrojeni na moja ya oksijeni. Hata hivyo, bado wanasayansi hawaelewi kabisa jinsi molekuli za maji zinavyofanya kazi. Jambo ambalo sote tunajua ni kwamba maji ni muhimu kwa uhai na yanafanyiza asilimia 80 hivi ya uzito wa vitu vyote vilivyo hai. Fikiria mambo matano kuhusu kitu hicho cha ajabu.

1. Maji yanaweza kuhifadhi kiasi kikubwa cha joto bila kiwango cha joto kuongezeka na hivyo yanasaidia kusawazisha hali ya hewa.

2. Maji yanapoganda, huwa yanapanuka na hivyo kufanya barafu ielee na kufanyiza tabaka linalozuia joto lisitoke. Ikiwa maji yangekuwa kama vitu vingine vinavyoongezeka uzito kadiri vinavyoganda, basi maziwa, mito, na bahari zingeganda kutoka chini hadi juu na hivyo kuangamiza kila kitu kwa barafu!

3. Mwangaza hupenya katika maji kwa urahisi na hivyo kuwezesha viumbe wanaotegemea mwangaza waendelee kuishi hata wakiwa chini sana majini.

4. Molekuli za maji hutokeza nguvu fulani. Nguvu hiyo inawezesha wadudu kukimbia juu ya kidimbwi, inasaidia kufanyiza matone, na kuchangia kupitisha maji hadi kwenye mimea mirefu zaidi.

5. Maji yanaweza kuyeyusha vitu vingi zaidi. Yanaweza kuyeyusha oksijeni, kaboni-dioksidi, chumvi, madini, na vitu vingine muhimu.

Muhimu Katika Kusawazisha Joto Duniani

Asilimia 70 hivi ya dunia imefunikwa na bahari na hivyo bahari hutimiza fungu muhimu katika kudhibiti hali ya hewa. Kwa kweli, bahari na angahewa zinafanya kazi pamoja, zikibadilishana joto, maji, gesi, na kuathiri kufanyizwa kwa upepo na mawimbi. Pia zinafanya kazi pamoja ya kuondoa joto kutoka maeneo ya Tropiki kuelekea ncha na hivyo kusawazisha joto duniani. Ili viumbe wengi waendelee kuwa hai, joto linahitaji kuwa katika kiwango kinachoruhusu maji yabaki yakiwa katika hali ya umajimaji. “Inaonekana kwamba hali za Dunia ni sawa kabisa,” kinasema kitabu Rare Earth—Why Complex Life Is Uncommon in the Universe.

Bila shaka, dunia ilibuniwa na haikujitokeza. Lakini je, ilijitokeza kwa nasibu, au je, ilitokezwa na Muumba mwenye upendo? Biblia inasema kwamba ilitokezwa na Muumba. (Matendo 14:15-17) Katika makala inayofuata, tutaona jinsi mifumo ya ajabu inayofanya sayari yetu iwe safi na yenye afya na hivyo kuunga mkono maoni ya Biblia.

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

BIBLIA NI SAHIHI KISAYANSI

Dunia inaelea angani. “Anaitandaza kaskazini juu ya mahali pasipo na kitu, akiitundika dunia pasipo na kitu.”—Ayubu 26:7, iliandikwa karibu 1613 K.W.K.

Dunia ni duara. “Kuna Yeye anayekaa juu ya mviringo wa dunia.” —Isaya 40:22, iliandikwa karibu 732 K.W.K.

Maji hufuata mzunguko. “Mito yote ya wakati wa majira ya baridi kali inaenda baharini . . . Mahali inapoenda mito hiyo ya majira ya baridi kali, hapo ndipo inarudi ili iende tena.”—Mhubiri 1:7, iliandikwa kabla ya 1,000 K.W.K.

Ulimwengu unaongozwa kwa sheria. “Mimi [Yehova] niliweka . . . sheria za mbingu na dunia.”—Yeremia 33:25, Biblia Habari Njema. Maneno hayo yaliandikwa kabla ya 580 K.W.K.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 7]

Magnetosphere: NASA/Steele Hill; aurora: Collection of Dr. Herbert Kroehl, NGDC; reef: Stockbyte/Getty Images