Mdomo wa Ngisi
Je, Ni Kazi ya Ubuni?
Mdomo wa Ngisi
▪ Wanasayansi wanastaajabishwa na mdomo wa ngisi. Wao hujiuliza: ‘Kitu kigumu sana hivyo kinaweza kuunganishwa kwa mwili usio na mifupa jinsi gani? Je, kuunganisha kitu kigumu na kitu chepesi hakuwezi kumchubua na kumuumiza ngisi?’
Fikiria hili: Ncha ya mdomo wa ngisi ni ngumu lakini sehemu ya chini ni laini. Mdomo huo umetengenezwa kwa mchanganyiko wa protini, maji, na kitu kigumu kinachoitwa chitin. Ugumu wa mchanganyiko huo hubadilika polepole kutoka kuwa laini hadi kuwa mgumu na hivyo ngisi anaweza kutumia mdomo wake bila kujichubua.
Profesa Frank Zok wa Chuo Kikuu cha California anasema kwamba kuchunguza mdomo wa ngisi kunaweza “kubadili sana maoni ya wahandisi kuhusu jinsi ya kuunganisha vitu mbalimbali.” Ujuzi huo unaweza kutumiwa kutengeneza viungo bandia. Ali Miserez, mchunguzi katika chuo hicho, anafikiria jinsi ya “kubuni kiungo bandia kinachoiga mchanganyiko wa mdomo huo, ili upande mmoja wa kiungo hicho uwe laini kama gegedu na upande mwingine” uwe umetengenezwa “kwa kitu kigumu.”
Una maoni gani? Je, mdomo wa ngisi wenye ncha ngumu na sehemu laini ya chini ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]
© Bob Cranston/SeaPics.com
© Richard Herrmann/SeaPics.com