Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Bucharest Jiji Lenye Majengo ya Kale na ya Kisasa

Bucharest Jiji Lenye Majengo ya Kale na ya Kisasa

Bucharest Jiji Lenye Majengo ya Kale na ya Kisasa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI RUMANIA

UNAPOTAZAMA jiji la Bucharest kutoka mbali unaona jengo moja linalotokeza—Kasri la Bunge (1), ambalo katika nyakati za Ukomunisti liliitwa Nyumba ya Watu. Watalii hupenda sana kutembelea jengo hilo ambalo ni kati ya majengo makubwa zaidi ulimwenguni.

Kwa njia fulani kasri hilo linawakilisha Bucharest ya kisasa. Lakini wenyeji wa Bucharest wana maoni yanayotofautiana kuhusu jengo hilo kubwa. Wakazi wanatumaini kwamba wageni watapendezwa na mambo mengine ya jiji hilo, yaani, majengo yake ya kale.

Mji Mkuu wa Kale

Mnamo 1862, Bucharest iliwekwa kuwa mji mkuu wa Rumania. Katika kipindi cha pili cha karne ya 19, jiji hilo lilisitawi upesi. Majengo mengi makubwa na yenye kuvutia yaliyobuniwa na wachoraji wa ramani za ujenzi Wafaransa yalianza kujengwa katika barabara zenye miti. Kwa kuwa Bucharest lina bustani nyingi, lilikuja kuitwa jiji la bustani. Pia Bucharest lilikuwa miongoni mwa majiji ya kwanza ulimwenguni kuwa na taa za barabarani zilizotumia mafuta. Mnamo 1935 Tao la Ushindi (2), lililoiga Arch de Triomphe kwenye barabara ya Champs-Élysée huko Paris lilijengwa kwenye barabara maridadi ya Kiseleff Avenue. Jiji hilo maridadi lilifanana na Paris. Bucharest hata liliitwa kwa utani Paris Ndogo ya Mashariki.

Baada ya Vita vya Pili vya Ulimwengu, Bucharest, lilibadilika sana chini ya utawala wa Kikomunisti. Karibu asilimia 33 ya sehemu ya mji ambayo ilikuwa na majengo mengi ya kale ilibomolewa ili kuwe na nafasi ya kujenga majengo ya ghorofa. Kati ya mwaka wa 1960 na 1961 peke yake, nyumba zenye ghorofa 23,000 hivi zilijengwa. Mnamo 1980, mipango ilianza kufanya ili kujenga lile jengo linaloitwa Nyumba ya Watu. Jengo hilo baadaye lilikuja kuwa na mashada mengi ya taa na chumba kilicho mita 90 chini ya ardhi cha kujikinga na mabomu. Jengo hilo lenye ukubwa wa mita 360,000 za mraba, lina ghorofa 12, na vyumba 1,100, na lina ukubwa mara tatu wa Kasri la Versailles huko Ufaransa. Nyumba nyingi zilihitaji kubomolewa katika eneo la zamani la mji ili kujenga Kasri la Bunge pamoja na barabara yake yenye upana mkubwa sana unaofika kwenye mwingilio wa kasri hilo. Barabara hiyo ni pana kuliko ile ya Champs-Élysées iliyoko Ufaransa. Wale waliojua jiji la Bucharest hapo awali, hawangeweza kulitambua baadaye.

Kwa wenyeji wengi, kasri hilo kubwa huwakumbusha kwa majonzi mjenzi wake, Nicolae Ceauşescu mtawala wa kimabavu aliyekufa. Akiongozwa na tamaa ya kujisimamishia mnara wa makumbusho, aliwakusanya wachoraji 700 hivi wa ramani za ujenzi na wafanyakazi wengi sana ambao walifanya kazi kwa bidii katika zamu tatu usiku na mchana. Utawala wake ulipoanguka mnamo 1989, jengo hilo halikuwa limekamilika ingawa kufikia wakati huo lilikuwa limetumia zaidi ya dola bilioni moja.

Jengo Lingine

Sehemu ya kale iliyobaki ya jiji hilo inaonekana kuwa tofauti sana. Katika eneo hilo unaweza kuona ubuni wenye kupendeza wa majengo ya kale ya Bucharest. Na kwenye Jumba la Makumbusho la Kijijini (3)—ambalo ni moja kati ya majumba mengi ya makumbusho katika jiji hilo—unaweza kuona utamaduni wenye unamna-namna wa maeneo ya vijijini ya Rumania. Katika bustani yenye utulivu iliyo ng’ambo ya ziwa, zaidi ya nyumba 50 za wakulima na majengo mengine kutoka sehemu zote za Rumania zilijengwa tena kwa uangalifu na kutokeza eneo lenye kupendeza. Kila nyumba ni kama jumba la makumbusho kwani zote zinaonyesha vifaa vya kazi, biashara, na mazingira ya nyumbani ya Warumania ambayo ni tofauti sana na Bucharest ya leo.

Katika jiji hilo, hakuna mpaka kati ya sehemu ya kale na ya kisasa. Si ajabu kuona jengo lililojengwa nyakati za kale likiwa limesimama kando ya jengo la kisasa (4). Hivyo, jiji la Bucharest lina majengo ya kale na ya kisasa yakiwa karibu-karibu.

[Picha katika ukurasa wa 10]

1 Kasri la Bunge

2 Tao la Ushindi

3 Jumba la Makumbusho la Kijijini

4 Jengo lililojengwa nyakati za kale likiwa limesimama kando ya jengo la kisasa

[Picha zimeandaliwa]

© Sari Gustafsson/hehkuva/age fotostock