Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Dundumio Lako Lina Tatizo?

Je, Dundumio Lako Lina Tatizo?

Je, Dundumio Lako Lina Tatizo?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI

SARA alihuzunika sana kwa kupoteza mimba yake ya miezi mitatu. Mwaka mmoja baadaye akapoteza mimba nyingine. Uchunguzi mbalimbali wa kitiba haukuonyesha kisababishi. Miaka ilipopita, Sara alianza kuongeza uzani, hata ingawa hakuwa akila chakula kingi na alifanya mazoezi kwa ukawaida. Pia, miguu yake ilianza kuuma na akaathiriwa sana na baridi. Mwishowe, uchunguzi wa damu na tezi dundumio lake ulionyesha kwamba Sara alikuwa na ugonjwa unaoitwa Hashimoto thyroiditis, ambao huenda ulisababisha mimba zake kutoka. *

Kama watu wengi, Sara hakuwa na wasiwasi wowote kuhusu dundumio lake. Lakini afya yake ilipozidi kuzorota aligundua kwamba tezi hiyo ni muhimu sana.

Tezi Dundumio

Dundumio ni tezi dogo lenye umbo la kipepeo lililo upande wa mbele wa shingo chini tu ya kongomeo. Dundumio lina sehemu mbili ambazo huzunguka koo na lina uzito usiozidi gramu moja. Tezi hiyo ni kati ya viungo na tishu zinatokeza na kuhifadhi homoni moja kwa moja ndani ya damu.

Dundumio lina vifuko vidogo vilivyojaa umajimaji mzito ulio na homoni za dundumio. Homoni hizo zina iodini nyingi. Kwa kweli, asilimia 80 hivi ya iodini mwilini inapatikana katika dundumio. Mtu anapokosa madini hayo anaweza kupatwa na ugonjwa wa kuvimba kwa tezi dundumio, au rovu. Watoto wachanga wanapokosa iodini wanaweza kushindwa kutokeza homoni na hilo litawafanya wawe mbilikimo, wawe na akili punguani, na kuzuia ukuzi wa viungo vyao vya uzazi.

Homoni za Dundumio Hufanyaje Kazi?

Kuna aina tatu za homoni ya dundumio: T3, RT3 (Reverse T3), na T4. * Homoni ya T3 na RT3 zinatokezwa na homoni ya T4 na mabadiliko hayo hufanyika nje ya dundumio kwenye tishu za mwili. Hivyo, mwili unapohitaji homoni zaidi za dundumio, tezi hiyo huingiza homoni ya T4 ndani ya damu, na kutoka hapo homoni hizo za T4 na homoni zinazofanyizwa kutokana nayo zinaingizwa kwenye chembe zote za mwili.

Kama tu pedali ya mafuta inavyoongoza mwendo wa injini ya gari, homoni za dundumio hudhibiti mwendo wa mwili wa kuyeyusha chakula, yaani, utendaji wa kemikali ndani ya chembe unaotokeza nishati na tishu mpya. Hivyo, homoni za dundumio husaidia katika ukuzi na urekebishaji wa tishu, huongoza mpigo wa moyo, na kudumisha kutokezwa kwa nishati ya misuli na joto mwilini.

Pia, homoni za dundumio hufanya kazi nyingine muhimu. Kwa mfano, zinasaidia maini kuondoa mafuta na kolesteroli isiyofaa kutoka kwenye damu. Kolesteroli hiyo hupelekwa kwenye nyongo na kutoka hapo inakuwa kinyesi. Kwa upande mwingine, kiasi kidogo cha homoni kinaweza kusababisha kuongezeka kwa kolesteroli isiyofaa na kupunguza mafuta, au kolesteroli inayofaa.

Ndani ya tumbo, homoni za dundumio hufanya umajimaji wa kumeng’enya utokezwe kwa wingi na pia huongeza utendaji wa misuli ya tumbo. Hivyo, dundumio linapotokeza homoni nyingi kupita kiasi mtu huenda haja kubwa mara nyingi sana, na linapotokeza kiasi kidogo sana cha homoni mtu hufunga choo.

Ni Nini Kinachodhibiti Dundumio?

Dundumio huanza kudhibitiwa katika eneo la ubongo linaloitwa hypothalamus, au sehemu ya ubongo wa kati. Sehemu hiyo inapotambua kuna uhitaji wa homoni za dundumio, inatuma ujumbe kwenye tezi pituitari iliyo chini ya ubongo kwenye sehemu ya juu ya mdomo. Kisha, tezi pituitari huachilia kwenye damu homoni inayochochea dundumio na hivyo kuifanya itokeze homoni.

Hivyo, kwa kupima viwango vya homoni inayochochea dundumio na homoni za dundumio kwenye damu, madaktari wanaweza kujua dundumio liko katika hali gani. Hilo ni muhimu kwa kuwa mtu anaweza kuwa na matatizo ya dundumio.

Dundumio Linapokuwa na Tatizo

Tatizo la dundumio humpata mtu kwa sababu ya kula chakula kisichokuwa na iodini, kufadhaika kimwili au kiakili, kuwa na kasoro katika chembe za urithi, kupatwa na maambukizo, mfumo wa kinga unaposhambulia chembe nzuri, au kupatwa na madhara yanayotokezwa na dawa za kutibu magonjwa mengine. * Dundumio lililovimba, au rovu, linaweza kuonyesha kwamba mtu ni mgonjwa. Uvimbe huo unaweza kuenea katika tezi yote au kutokeza uvimbe mwingine mdogo-mdogo. Ingawa kwa kawaida uvimbe huo si hatari, sikuzote unapaswa kutibiwa kwa kuwa unaweza kuashiria tatizo lingine kubwa, kama vile kansa. *

Kwa kawaida, dundumio lenye tatizo hutokeza homoni nyingi kupita kiasi au chache sana. Kutokezwa kwa homoni nyingi kupita kiasi huitwa hyperthyroidism, kutokezwa kwa homoni chache sana huitwa hypothyroidism. Ugonjwa katika dundumio unaweza kutokea polepole na bila kuonekana, kwa hiyo, mtu anaweza kuwa nao kwa miaka mingi na asitambue. Kama magonjwa mengine, huenda ikawa rahisi kuutibu ukigunduliwa mapema.

Magonjwa ya dundumio yanayowapata watu wengi ni Hashimoto thyroiditis na ugonjwa unaoitwa Graves. Magonjwa yote mawili hufanya mfumo wa kinga ushambulie chembe nzuri ukidhani ni adui. Ugonjwa wa Hashimoto thyroiditis unapatikana mara sita zaidi katika wanawake kuliko katika wanaume, na mara nyingi hufanya dundumio litokeze homoni chache sana. Ugonjwa wa Graves unapatikana mara nane zaidi katika wanawake na kwa kawaida hufanya dundumio litokeze homoni nyingi kupita kiasi.

Kuna maoni mbalimbali kuhusu ni mara ngapi mtu anapaswa kuchunguzwa ikiwa ana ugonjwa katika dundumio, ingawa inasemekana ni muhimu kwa watoto wachanga kufanyiwa uchunguzi kwa ukawaida. (Ona sanduku  “Uchunguzi Muhimu kwa Watoto Wachanga.”) Ikiwa uchunguzi unaonyesha kwamba mtu ana dundumio linalotoa homoni chache, kwa kawaida mtu huchunguzwa ikiwa ana chembe zinazoshambulia tezi hiyo. Kwa upande mwingine, iwapo uchunguzi utaonyesha kuwa mtu ana dundumio linalotoa homoni nyingi kupita kiasi, uchunguzi wa ekisirei hufanywa, maadamu mgonjwa si mjamzito au hanyonyeshi. Ikiwa kuna uvimbe katika dundumio huenda sehemu ya uvimbe huo ikakatwa na kuchunguzwa ikiwa ina kansa.

Mtu Anapohitaji Matibabu

Huenda mtu akapewa dawa za kupunguza dalili za kutokezwa kwa homoni nyingi kupita kiasi, kama vile moyo kupiga kwa kasi, kutetemeka kwa misuli, na wasiwasi. Matibabu mengine yanahusisha kuharibu chembe za dundumio ili tezi hiyo itokeze homoni chache. Na nyakati nyingine tezi hiyo inaweza kutolewa.

Huenda daktari akapendekeza wagonjwa walio na tatizo la kutokezwa kwa homoni chache sana au waliotolewa dundumio watumie dawa zilizo na homoni ya T4 kila siku. Ili wawape kiwango kinachofaa cha homoni hiyo, madaktari huwachunguza wagonjwa hao mara kwa mara. Kansa ya dundumio inaweza kutibiwa kwa njia mbalimbali kutia ndani, kupitia madawa, upasuaji, kuingizwa kwa kemikali mwilini, na kupitia miale yenye iodini.

Sara anatibiwa kwa kutumia dawa zilizo na homoni ya T4 na mtaalamu wa lishe amemsaidia kula vyakula vyenye lishe. Amepata matokeo mazuri. Kama Sara alivyojifunza, dundumio linaweza kuwa kiungo kidogo sana, lakini ni muhimu sana. Kwa hiyo, tunza dundumio lako, kula chakula kinachofaa kilicho na iodini ya kutosha, epuka mfadhaiko wa daima, na jitahidi kuwa na afya nzuri.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Ingawa dundumio linalotoa homoni chache sana linaweza kuhatarisha mimba, wanawake wengi wenye ugonjwa katika dundumio huzaa watoto wenye afya. Hata hivyo, ni muhimu sana kwa mama kupata matibabu ya kuongeza homoni mwilini, kwa kuwa mwanzoni yeye ndiye humpa mtoto wake ambaye hajazaliwa homoni za dundumio.

^ fu. 9 T3 ni homoni inayoitwa triiodothyronine na T4 inaitwa thyroxine. Nambari 3 na 4 zinaonyesha idadi ya atomu za iodini zilizo katika homoni hizo. Pia, dundumio hutokeza kalistonini, homoni inayosaidia kudumisha kiwango cha kalisi ndani ya damu.

^ fu. 17 Amkeni! halipendekezi matibabu yoyote hususa. Ukishuku kwamba una tatizo na dundumio lako, mwone daktari aliye na ujuzi wa kuzuia na kutibu ugonjwa katika dundumio.

^ fu. 17 Watu ambao wamepata matibabu ya kichwa na shingo kwa kutumia miale au ambao wamewahi kupata kansa au wenye watu wa ukoo wenye kansa ya dundumio wako katika hatari kubwa zaidi ya kupatwa na kansa.

[Blabu katika ukurasa wa 27]

Kama tu pedali ya mafuta inavyoongoza mwendo wa injini ya gari, homoni za dundumio hudhibiti mwendo wa mwili wa kuyeyusha chakula

[Blabu katika ukurasa wa 29]

Ugonjwa katika dundumio unaweza kutokea polepole na bila kuonekana, kwa hiyo, mtu anaweza kuwa nao kwa miaka mingi na asitambue

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 28]

DALILI ZA KAWAIDA

Hyperthyroidism: Kuudhika sana, kupoteza uzito bila sababu, moyo kupiga kwa kasi, kwenda haja kubwa mara nyingi zaidi, kutopata hedhi kwa ukawaida, kukasirika-kasirika, kuwa na wasiwasi, kubadilika- badilika kwa hisia, kutokeza sana kwa mboni za macho, udhaifu wa misuli, kutopata usingizi, na kuwa na nywele nyembamba zinazokatika haraka. *

Hypothyroidism: Kuwa mvivu na kukosa kuwa makini, kuongeza uzito bila sababu, kukatika kwa nywele, kufunga choo, kuathiriwa sana na baridi, kutopata hedhi kwa ukawaida, kushuka moyo, kubadilika kwa sauti (sauti nzito), kusahau mambo, na uchovu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 36 Huenda dalili nyingine zikasababishwa na magonjwa mengine, kwa hiyo hakikisha unamwona daktari ukijihisi mgonjwa.

[Sanduku katika ukurasa wa 28]

 UCHUNGUZI MUHIMU KWA WATOTO WACHANGA

Matone machache ya damu yaliyotolewa kwa mtoto mchanga yanaweza kuonyesha ikiwa ana tatizo katika dundumio. Uchunguzi unapoonyesha kuna tatizo, madaktari wanaweza kumtibu. Mtoto anapokosa homoni za kutosha za dundumio anaweza kuwa mbilikimo na akili punguani. Kwa hiyo, watoto hufanyiwa uchunguzi siku chache tu baada ya kuzaliwa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 29]

JE, UNAKULA VYAKULA VINAVYOFAA?

Kula chakula chenye lishe kunaweza kuzuia matatizo katika dundumio. Kwa mfano, je, unakula chakula chenye iodini ya kutosha ambayo ni muhimu katika kutokeza homoni za dundumio? Unaweza kupata madini hayo kwa kula samaki wa baharini na chakula kingine cha baharini. Kiasi cha iodini katika mboga na nyama hutofautiana kulingana na kemikali zilizo katika udongo wa eneo fulani. Serikali fulani huamuru kwamba chumvi iongezwe iodini ikiwa chakula kinachokuzwa nchini humo kimekosa madini hayo.

Madini ya seleni ni muhimu pia kwa dundumio. Madini haya ni sehemu ya kimeng’enya ambacho hubadili homoni ya T4 kuwa T3. Kiwango cha madini ya seleni katika mboga, nyama, na maziwa hutegemea udongo wa eneo. Unaweza kupata seleni nyingi katika vyakula vya baharini, mayai, na kabeji. Bila shaka, ukifikiri kwamba una tatizo katika dundumio, mwone daktari; usijaribu kujitibu.

[Mchoro katika ukurasa wa 28]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Koo

Koromeo (Kongomeo)

Dundumio

Koo