Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪ “Bidhaa 160,000 hivi zimepotea kutoka katika majumba ya makumbusho nchini Urusi.”—RIA NOVOSTI, URUSI.
▪ “Chombo cha Angani kinachoitwa Phoenix Mars cha shirika la NASA, kimegundua kwamba kuna theluji inayoanguka kutoka kwenye mawingu ya Mihiri.”—“NASA MISSION NEWS,” MAREKANI.
▪ “Asilimia 65 ya madereva na abiria wanaokufa katika aksidenti za barabarani nchini Ugiriki hawatumii mikanda ya usalama au kofia za usalama.” —EIKONES, UGIRIKI.
Mizigo Inayopotea
Mara nyingi watu hupoteza mizigo yao wanaposafiri kwa ndege. Gazeti International Herald Tribune linaripoti kwamba mnamo 2007, “mizigo milioni 42 ilipotea, na hiyo ni asilimia 25 zaidi ya mwaka wa 2006.” Watu wengi walirudishiwa mizigo yao katika muda wa saa 48, lakini asilimia 3 kati yao, yaani, “mzigo wa abiria mmoja kati ya 2,000 haukupatikana.” Mizigo iliyopotea iligharimu mashirika ya ndege dola bilioni 3.8 mnamo 2007. Kati ya mambo yanayofanya mizigo ipotee ni “msongamano kwa sababu ya kuongezeka kwa wasafiri, muda mfupi wa kupakua mizigo kutoka kwenye ndege,” kutoshughulikia mizigo vizuri, na kuchanganya vibandiko.
Wakatoliki Wanaishi Pamoja Bila Kuoana
Uchunguzi mmoja huko Ufaransa unaonyesha kwamba “kuzorota kwa dini” ndiko kunawafanya watu wabadili maisha na viwango vyao haidhuru wao ni wa dini gani, linasema gazeti Population & Sociétés. Kwa mfano, asilimia 88 hivi ya vijana walio kati ya umri wa miaka 18 na 24 nchini Ufaransa wanadai kuwa Wakatoliki, lakini asilimia 80 kati yao hawaendi kanisani isipokuwa tu wakati wa arusi, ubatizo, au maziko. Kuzorota kwa viwango vya kitamaduni kunaonekana katika maisha ya familia. Miaka 40 iliyopita idadi ya wenzi wa ndoa walioishi pamoja bila kuoana ilikuwa 1 kati ya 10. Leo idadi hiyo ni 9 kati ya 10. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba “kati ya Wakatoliki wanaoenda kanisani kwa ukawaida, asilimia 75 waliishi pamoja kabla ya kufunga ndoa.”
Wakulima Nchini India Wanajiua
Tangu mwaka wa 2002, zaidi ya wakulima 17,000 wamejiua nchini India, mara nyingi kwa kunywa dawa ya kuua wadudu, linaripoti gazeti The Hindu. Kati ya matatizo ambayo wakulima hupata ni ukame, kuanguka kwa bei ya mazao, kupanda kwa gharama za ukulima, na ugumu wa kupata mkopo wa benki. Kwa sababu hiyo, wengi hukopa pesa kutoka kwa wakopeshaji ambao hutoza riba za juu sana, na hivyo kuwafanya waliokopa wawe na deni kubwa sana. Ili kulipa madeni hayo, baadhi ya wakulima huuza viungo vyao vya mwili. Hata hivyo, wanaposhindwa kulipa madeni, maelfu kati yao huwa na suluhisho moja tu, yaani, kujiua.
Mamba Wanawasiliana Kabla ya Kuangua
“Watoto wa mamba huzungumziana wakiwa ndani ya yai,” na hivyo wanaangua wakati mmoja, linaripoti gazeti The Times la London. Milio ya mamba wa Mto Nile wakiwa ndani ya mayai ilirekodiwa. Milio hiyo ilichezwa karibu na mayai fulani. Mamba waliokuwa ndani ya mayai hayo walijibu milio hiyo na kufanya mayai yao yasonge mara nyingi zaidi kuliko yale ambayo hayakuchezewa milio hiyo. Ripoti hiyo inasema kwamba mamba “waliosikia milio ya mamba wengine ambao hawajaanguliwa waliangua baada ya dakika kumi.” Mayai ambayo yaliwekwa mahali pasipokuwa na milio au yale yaliyochezewa milio mara chache yalishindwa kuangua wakati mmoja na yale mengine.