Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Majitu Yalipokuwa Yamejaa Ulaya

Majitu Yalipokuwa Yamejaa Ulaya

Majitu Yalipokuwa Yamejaa Ulaya

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

MNAMO 1932, wajenzi wa barabara walikuwa wakichimba karibu na uwanja wa Colosseum huko Rome wakati mmoja wao alipogonga kitu fulani kigumu. Kumbe kilikuwa ni pembe na fuvu la tembo. Huo haukuwa ugunduzi wa pekee. Kwa miaka mingi, mabaki ya tembo 140 yamepatikana huko Rome na katika maeneo ya karibu. Mabaki ya kwanza yalipatikana katika karne ya 17.

Watu walifikiri kwamba mifupa hiyo ilikuwa ya tembo waliosafirishwa hadi Roma ya kale kutoka nchi nyingine au wale walioletwa Italia na Jenerali Hanibali Mkarthage. Kasisi wa karne ya 19 G. B. Pianciani ambaye pia alikuwa profesa wa Sayansi ya Asili huko Viterbo, alipinga madai hayo. Kwa kuwa mifupa hiyo iligunduliwa hasa katika maeneo yenye mchanga ulioachwa na maji, alifikia mkataa kwamba ilikuwa ya wanyama waliokufa mahali pengine na kuletwa hapo na maji ya mafuriko.

Mabaki au visikuku vya tembo vilivyochimbuliwa huko Italia havifanani na ya tembo wa leo. Badala yake, mabaki hayo ni ya jamii ya tembo iliyotoweka inayoitwa Elephas antiquus, au tembo wa kale. (Ona ukurasa wa 15.) Tembo huyo alikuwa na pembe zilizonyooka na alikua kufikia kimo cha mita 5 kwenye mabega, kimo kinachozidi tembo wa leo kwa mita 2 hivi.

Majitu hayo yalikuwa mengi kadiri gani? Rekodi ya vitu vya kale vilivyochimbuliwa inaonyesha kwamba wakati mmoja tembo hao walipatikana katika sehemu zote za Ulaya na Uingereza, kama tu tembo wengine wa jamii yao wanaoitwa mammoth. Isitoshe, mabaki ya tembo hao hayapatikani mbali na yale ya wanyama wengine, bali yanapatikana katika matabaka ya udongo ambapo mabaki ya jamii nyingine nyingi za wanyama yanapatikana, na baadhi ya wanyama hao waliwawinda tembo hao.

Fisi na Viboko

Mabaki yaliyochimbuliwa huko Lazio, eneo la Italia ya kati linalotia ndani Rome, yanadokeza kwamba wakati mmoja eneo hilo lilikuwa na hali ya hewa kama ile ya Afrika, kwa kuwa viboko, swala, na hata wanyama wakubwa wa jamii ya paka walipatikana katika eneo hilo. Kwa kweli, mabaki ya paka mmoja, anayeitwa chui wa Monte Sacro, yalipatikana katikati ya Rome. Katika kijiji cha Polledrara kilicho nje ya jiji la Rome, zaidi ya mabaki ya wanyama 9,000 yamechimbuliwa, yakionyesha wanyama mbalimbali waliokuwapo katika eneo hilo kama vile: tembo wa kale, nyati, mbawala, nyani wa Barbary, vifaru, na fahali-mwitu waliotoweka karne nne hivi zilizopita. Jumba la Makumbusho katika eneo hilo lina njia iliyoinuliwa ili wageni waweze kuona mahali mabaki hayo yalipochimbuliwa.—Ona ukurasa wa 16.

Pango moja karibu na Palermo, Sicily, lilikuwa limejaa mabaki mengi sana kutia ndani mabaki ya mifupa ya mbawala, fahali, tembo, na viboko wa umri mbalimbali, na hata kulikuwa na kijusi. Kwa kweli, tani 20 za mabaki ya kale yalikuwa yakiuzwa katika miezi sita ya kwanza baada ya eneo hilo kugunduliwa!

Katika Uingereza Kusini, mtaalamu wa mabaki ya kale ya wanyama na mimea, J. Manson Valentine, aligundua matabaka ya mchanga yaliyo na mifupa mingi iliyovunjika ya wanyama waliopatikana huko Palermo, kutia ndani fisi na dubu barafu. Kwa nini kuna matabaka hayo makubwa ya mabaki ya wanyama katika maeneo tofauti-tofauti?

Wanasayansi fulani wanaamini kwamba hali ambayo wanyama hao walipatikana zinaonyesha kwamba walikufa kutokana na msiba wa asili. Hata iwe wanyama hao walikufa kwa sababu gani, kutoweka kwao kulionekana katika maeneo mbalimbali kutia ndani Ulaya, Visiwa vya Uingereza, Siberia, na Alaska.

Rekodi za mabaki ya wanyama zinatusaidia kuwazia ulimwengu tofauti na ule tunaojua leo. Kwa kweli, zamani za kale, Italia ilifanana na pori za Afrika.

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

MABAKI YA KALE HUTAMBULIWAJE?

Huenda mabaki ya kale la mnyama yakaonekana tu kama mfupa wa kawaida. Kwa kweli, hilo husababishwa na mabadiliko katika kemikali ambayo hufanya mabaki ya mnyama yawe magumu kama mwamba kabla hayajaoza.

Njia moja ya kufanya mabaki ya mnyama yawe magumu ni wakati maji yenye madini yanapopenya kwenye mabaki hayo. Katika hatua hii mifupa yake hubadilika kabisa au kidogo, na kuwa madini yanayopatikana katika matope. Hivyo, ili mabadiliko hayo yatukie, lazima kuwe na hali fulani katika mazingira. Hali hizo zinatia ndani wingi wa matope na kuzikwa haraka kwa mabaki na pia uwezo wake wa kutooza haraka. Katika hali za kawaida, mabaki ya wanyama yasipoliwa na wanyama wengine huliwa na bakteria na vilevile huoza kwa sababu ya kemikali fulani au kwa sababu ya upepo na maji. Kwa hiyo, si jambo la kawaida kwa mifupa kubadilika kuwa madini.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

MAMOTHI KATIKA KIZIO CHA KASKAZINI

Rekodi ya mabaki ya wanyama wa kale inaonyesha kwamba mamothi wenye manyoya walipatikana katika maeneo mengi sana, kutia ndani Asia, Amerika Kaskazini, na Ulaya. Huko Ulaya, inaonekana kwamba eneo la mbali zaidi upande wa kusini ambalo wanyama hao walifika ni Italia.

Mamothi, ambao walikuwa na ukubwa kama wa tembo wa leo wa Asia, walikuwa na manyoya yaliyokua kufikia sentimita 50, na mamothi wa kiume walikuwa na pembe ndefu zilizojipinda zilizokuwa na urefu wa mita 5 hivi. Pembe nyingi sana za mamothi zimepatikana huko Siberia. Pembe hizo ni nyingi sana hivi kwamba zimekuwa zikisafirishwa hadi China na Ulaya tangu enzi za kati.

[Hisani]

Photo courtesy of the Royal BC Museum

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Eneo la Polledrara lenye mabaki ya wanyama

[Hisani]

Soprintendenza Archeologica di Roma

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Top: Museo di Paleontologia dell’Università degli Studi “La Sapienza” di Roma; bottom: © Comune di Roma - Sovraintendenza Beni Culturali (SBCAS; fald. 90, fasc. 4, n. inv. 19249)