Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Matumizi Mazuri na Mabaya ya Dawa za Kitiba

Matumizi Mazuri na Mabaya ya Dawa za Kitiba

Matumizi Mazuri na Mabaya ya Dawa za Kitiba

MSICHANA anayeitwa Angie aliwasikia wazazi wake wakisema kwamba dawa za ndugu yake zilisaidia kupunguza hamu yake ya kula. Kwa sababu Angie alihangaika sana kuhusu uzito wake, alianza kutumia dawa za ndugu yake, akimeza tembe moja baada ya siku chache. Ili wazazi wake wasigundue, alimwomba rafiki yake aliyekuwa akitumia dawa hizohizo ampe tembe kadhaa. *

Kwa nini watu wengi hutumia dawa vibaya? Sababu moja ni kwamba zinapatikana kwa urahisi nyumbani. Pili, vijana wengi hujidanganya kwamba hawavunji sheria yoyote kwa kutumia dawa bila maagizo ya daktari. Na tatu, inaonekana kwamba dawa zinazopendekezwa na daktari hazina madhara sana kama dawa za kulevya. Vijana fulani hujiambia, ‘Ikiwa mtoto anaweza kunywa dawa fulani, basi bila shaka ni salama kuitumia.’

Ni kweli kwamba zinapotumiwa vizuri, dawa zinazopendekezwa na daktari zinaweza kuboresha afya na hata kuokoa uhai. Lakini zinapotumiwa vibaya zinaweza kuwa hatari kama dawa za kulevya. Kwa mfano, mtu anapotumia vibaya dawa fulani za kuchochea utendaji wa mwili, anaweza kufanya moyo uache kupiga au kupatwa na kifafa. Dawa nyingine zinaweza kupunguza mwendo wa kupumua na mwishowe kusababisha kifo. Pia dawa inaweza kuwa na madhara ikitumiwa na dawa nyingine au kileo. Mapema mnamo 2008, mwigizaji mmoja maarufu alikufa “kwa sababu ya kuchanganya dawa sita za kumtuliza mtu akili, za kulala, na za kutuliza maumivu,” lilisema gazeti Arizona Republic.

Hatari nyingine ni kwamba mtu anaweza kuwa mraibu. Dawa nyingine huwa kama dawa za kulevya kwani zinapotumiwa kupita kiasi au kwa sababu isiyofaa, zinachochea sehemu za ubongo zinazoufanya mwili usisimke na hivyo kufanya mtu awe na hamu yenye kuendelea ya dawa hizo. Lakini badala ya kutokeza msisimko unaoendelea au kuwasaidia watu wakabiliane na matatizo maishani, kutumia dawa vibaya hutokeza matatizo zaidi. Dawa hizo zinaweza kuongeza mfadhaiko na kushuka moyo, kuharibu afya na uwezo wa mwili wa kufanya kazi kwa njia ya kawaida, zinaweza kumfanya mtu awe mraibu, au kusababisha mambo haya yote. Mambo hayo humfanya mtu awe na matatizo nyumbani, shuleni, au kazini. Kwa hiyo, tutatofautisha jinsi gani ikiwa dawa zilizopendekezwa na daktari zinatumiwa vizuri au vibaya?

Matumizi Mazuri na Mabaya

Unatumia dawa vizuri ikiwa unazimeza kulingana na maagizo ya daktari ambaye anajua ugonjwa wako. Hilo linatia ndani kumeza kiasi cha dawa ulichoambiwa, wakati unaofaa, kwa njia inayofaa, na kwa sababu zinazofaa za kitiba. Hata hivyo, unaweza kupatwa na matatizo mengine yasiyofaa au yaisiyotazamiwa. Hilo likitukia, mwone daktari mara moja. Anaweza kukubadilishia dawa au kukuambia uache kutumia dawa hiyo. Unaweza kufuata mwongozo huo unapotumia dawa unazoweza kununua bila maagizo ya daktari: Zitumie tu ikiwa una sababu nzuri ya kufanya hivyo na ufuate kwa uangalifu maagizo yaliyo kwenye kibandiko.

Watu hujihatarisha wanapotumia dawa kwa sababu zisizofaa, wasipomeza kiwango walichopendekezewa na daktari, wanapotumia dawa za mtu mwingine, au kutumia dawa kwa njia isiyofaa. Kwa mfano, tembe fulani zinapaswa kumezwa zikiwa nzima ili ziweze kufanya kazi polepole mwilini. Mara nyingi watu hutumia dawa hizo vibaya kwa kuzipondaponda au kuzitafuna, kuzisaga na kuzinusa, au kuziyeyusha ndani ya maji na kujidunga mwilini kwa kutumia sindano. Kufanya hivyo kunaweza kumlewesha mtu, lakini hiyo inaweza kuwa hatua ya kwanza ya kumfanya mtu awe mraibu. Isitoshe, kufanya hivyo kunaweza kusababisha kifo.

Kwa upande mwingine, ikiwa mtu anatumia dawa kwa njia inayofaa lakini anashuku kwamba huenda inamfanya awe mraibu, anapaswa kumjulisha daktari bila kukawia. Daktari atajua jinsi ya kurekebisha hali hiyo bila kupuuza ugonjwa wa mtu huyo.

Kuenea sana kwa matumizi mabaya ya dawa, kunaonyesha jinsi hali ilivyo katika nyakati zetu. Mpango wa familia, mahali ambapo mtu angetazamia kupata upendo na kimbilio kutokana na matatizo ya kila siku, unakumbwa na hali ngumu. Viwango vya maadili na vya kiroho vinapotea, na watu pia hawaheshimu uhai. (2 Timotheo 3:1-5) Sababu nyingine ni kwamba watu hawana tumaini la kuwa na wakati ujao mzuri. Watu wengi wanatazamia tu mabaya. Hivyo, wanafanya mambo bila kufikiria madhara na wanafuatilia anasa bila kujali. Biblia inasema: “Mahali pasipo na maono watu hujiachilia.”—Methali 29:18.

Ikiwa wewe ni mzazi, bila shaka unataka kuilinda familia yako kutokana na upotovu wa maadili wa ulimwengu na ufuatiliaji wa mambo yasiyo muhimu. Lakini unaweza kufanya hivyo jinsi gani? Na unaweza kupata wapi mwongozo unaofaa na tumaini linalotegemeka la wakati ujao mzuri? Makala zinazofuata zitajibu maswali hayo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Imetolewa katika Tovuti ya TeensHealth.

[Sanduku katika ukurasa wa 4]

WATAFANYA LOLOTE ILI WALEWE

Watu fulani watajaribu kufanya jambo lolote lile ili tu walewe. Mazoea yenye kudhuru sana yanatia ndani kuvuta kemikali za kusafisha, rangi za kupaka kucha, kemikali za kung’arisha fanicha, petroli, gundi, rangi, na kemikali nyingine zinazoweza kugeuka kuwa mvuke. Mtu anapovuta harufu ya kemikali, harufu hiyo huingia moja kwa moja kwenye mfumo wa damu na hivyo kumfanya mtu alewe mara moja.

Zoea lingine lenye kudhuru ni matumizi mabaya ya dawa zinazonunuliwa bila maagizo ya daktari ambazo zina alkoholi au zinazomfanya mtu ahisi kulala. Zinapotumiwa kwa kiasi kikubwa, zinaathiri hisi za mtu, hasa hisi ya kusikia na kuona, na zinaweza kumfanya mtu achanganyikiwe, aone njozi, afe ganzi, na aumwe na tumbo.

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

“MBINU ZA KUPATA DAWA”

“Waraibu na watu wanaotumia dawa vibaya wana ‘mbinu za kupata dawa,’” linasema jarida Physicians’ Desk Reference. “Mbinu za kupata dawa hutia ndani kupiga simu za dharura au kwenda kwenye vyumba vya matibabu ya dharura saa za kazi zinapokaribia kwisha, kukataa kufanyiwa uchunguzi unaofaa wa kitiba au kutumwa kwa daktari mwingine, kudai mara nyingi kwamba wamepoteza karatasi ya dawa, kubadili maandishi ya dawa, na kukataa kutoa habari za matibabu ya awali au majina ya madaktari wengine ambao wamewahi kumtibu. Ni jambo la kawaida kwa watu wanaotumia dawa vibaya na kwa waraibu kubadilisha-badilisha madaktari ili kuandikiwa dawa zaidi.”

Aina tatu zifuatazo za dawa hutumiwa vibaya mara nyingi:

Dawa zenye kasumba (Opioids)—dawa za kutuliza maumivu

Dawa za kupunguza wasiwasibarbiturate na benzodiazepine zinazotumiwa kupunguza wasiwasi au kumfanya mtu apate usingizi

Dawa za kuchochea utendaji wa mwili—zinatumiwa kutibu tatizo la upungufu wa makini kutokana na utendaji wa kupita kiasi, kusinzia mchana, au kunenepa kupita kiasi. *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 24 Habari hii imetolewa na Taasisi ya Kitaifa ya Dawa za Kulevya.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

MIONGOZO YA KUTUMIA DAWA VIZURI

1. Fuata maagizo kwa uangalifu.

2. Usibadili kiasi cha dawa bila kumuuliza daktari.

3. Usiache kutumia dawa ulizoandikiwa bila kuagizwa na daktari.

4. Usipondeponde au kuvunja tembe ikiwa hujaagizwa kufanya hivyo.

5. Tambua madhara ambayo dawa hizo zinaweza kukusababishia unapoendesha gari au unapofanya utendaji mwingine.

6. Chunguza madhara ya kuchanganya dawa hiyo na alkoholi au dawa nyingine, iwe umeandikiwa na daktari au umeinunua bila maagizo ya daktari.

7. Ikiwa umewahi kutumia dawa vibaya au vitu vingine vinavyolewesha, mwambie daktari.

8. Usitumie dawa alizoandikiwa mtu mwingine, na usiwape watu wengine dawa ulizoandikiwa. *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 36 Habari hii inategemea madokezo yaliyotolewa na Shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa la Marekani.