Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Uogope Kupigwa na Jua?

Je, Uogope Kupigwa na Jua?

Je, Uogope Kupigwa na Jua?

“Kadiri tabaka la ozoni linavyozidi kuharibiwa na kadiri watu ulimwenguni wanavyozidi kupenda kujianika na kucheza juani, ndivyo madaktari wanavyohangaishwa na hatari ya watu kupatwa na magonjwa yanayotokana na kupigwa sana na miale hatari ya jua.”—DAKT. LEE JONG-WOOK, ALIYEKUWA MKURUGENZI MKUU WA SHIRIKA LA AFYA ULIMWENGUNI.

MARTIN, mwanamume mweupe kutoka Ulaya Kaskazini, alikuwa amelala chini ya mwavuli unaotumiwa ufuoni kwenye pwani ya Italia. Alipoamka, alikuta kwamba kivuli kilikuwa kimesonga na rangi ya miguu yake ilikuwa imebadilika na kuwa nyekundu. “Nililazimika kwenda kwenye idara inayoshughulikia hali za dharura katika hospitali fulani,” anaeleza Martin. “Singeweza kuikunja miguu yangu na ilikuwa imevimba. Siku mbili au tatu zilizofuata, nilihisi maumivu makali. Sikuweza kusimama au kuikunja miguu yangu. Ngozi ya miguu yangu ilikuwa imenyooka sana hivi kwamba niliogopa ingepasuka.”

Watu wengi wanadhani kwamba ni watu wenye ngozi nyeupe tu kama Martin wanaohitaji kuogopa kupigwa na jua. Hata hivyo, ingawa watu wenye ngozi nyeusi hawaathiriwi sana na miale ya jua, bado wanaweza kupata kansa ya ngozi. Na mara nyingi kansa yao haitambuliwi hadi inapokuwa hatari. Matatizo mengine yanayosababishwa na kupigwa na jua kwa muda mrefu yanatia ndani kuharibika kwa macho na mfumo wa kinga, matatizo ambayo huenda yakagunduliwa miaka kadhaa baada ya madhara kutokea.

Ni kweli kwamba, kwa kawaida kiwango cha miale hatari ya jua huongezeka kadiri mtu anavyokaribia ikweta. Kwa hiyo, wale wanaoishi katika maeneo ya Tropiki au maeneo yaliyo karibu na Tropiki, au wale wanaotembelea maeneo hayo wanapaswa kuchukua hatua zinazofaa ili kujikinga. Sababu moja ya kufanya hivyo ni kwamba katika miaka ya hivi karibuni, tabaka la ozoni linalokinga anga letu limepungua. Acheni tuchunguze baadhi ya madhara yanayoweza kusababishwa na kupigwa na jua kwa muda mrefu.

Kuharibika kwa Macho

Watu milioni 15 hivi ni vipofu kwa sababu ya watoto wa jicho. Hicho ndicho kisababishi kikuu cha upofu ulimwenguni. Watoto wa jicho hutokea wakati protini zilizo katika lenzi ya jicho zinapofumuka, kisha zinafungamana, na kufanyiza madoadoa ambayo hufanya lenzi isione vizuri. Watoto wa jicho hutokea kwa sababu ya macho kupigwa na miale hatari ya jua kwa muda mrefu. Kwa kweli, inakadiriwa kwamba asilimia 20 hivi ya watoto wa jicho husababishwa au kuathiriwa zaidi mtu anapopigwa na jua kupita kiasi.

Kwa kusikitisha, eneo lililo karibu na Ikweta ambako watu huathiriwa sana na watoto wa jicho lina nchi zinazositawi zilizo na watu wengi maskini. Hivyo, mamilioni ya maskini huko Afrika, Asia, Amerika ya Kati, na Amerika Kusini ni vipofu kwa sababu hawana pesa za kugharimia upasuaji wa kutoa watoto wa jicho.

Kuharibika kwa Ngozi

Kati ya visa vyote vya kansa ulimwenguni, asilimia 33 ni kansa ya ngozi. Kila mwaka, visa 130,000 hivi vya kansa inayoathiri chembe za ndani ya ngozi huripotiwa. Hiyo ndiyo kansa hatari zaidi ya ngozi. Kati ya visa milioni mbili na milioni tatu vya kansa nyingine za ngozi kama vile kansa inayoathiri chembe za katikati za ngozi na kansa inayoathiri chembe za juu za ngozi huripotiwa. Inakadiriwa kwamba watu 66,000 hivi hufa kila mwaka kutokana na kansa ya ngozi. *

Miale ya jua inaweza kuharibu ngozi yako jinsi gani? Kuunguzwa na jua ndiyo madhara yanayojulikana zaidi ya kupigwa na jua kwa muda mrefu. Dalili zinazoonekana kwanza zinaweza kuendelea kwa siku kadhaa na zinaweza kutia ndani malengelenge na kubambuka ngozi.

Ngozi inapounguzwa, miale hatari ya jua huua chembe nyingi zilizo katika tabaka la juu la ngozi na kuharibu matabaka ya ndani. Unaweza kujua ngozi ya mtu imeharibika rangi yake inapobadilika kwa sababu ya kupigwa na jua. Mtu anaweza kupatwa na kansa wakati chembe za DNA zinazodhibiti ukuzi na kugawanyika kwa chembe za ngozi zinapoharibiwa. Pia, miale ya jua huathiri wororo wa ngozi na kuifanya iwe nyepesi. Hilo husababisha makunyanzi, ngozi kulegea na vilevile kuchubuka kwa urahisi.

Kuharibika kwa Mfumo wa Kinga

Uchunguzi mbalimbali unaonyesha kwamba ngozi inapofyonza kiasi kikubwa cha miale hatari ya jua, utendaji wa sehemu fulani za mfumo wa kinga huathiriwa sana. Hilo linaweza kupunguza uwezo wa mwili wa kujilinda dhidi ya magonjwa fulani. Imeonekana kwamba hata mtu anapopigwa na jua kwa muda mfupi anaweza kuongeza hatari ya kushambuliwa na bakteria, kuvu, vijidudu, au virusi. Watu wengi wametambua kwamba wanapopigwa na miale ya jua, wao hupatwa na vidonda vya ngozi, au herpes simplex. Ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) inaeleza kwamba aina moja ya miale ya urujuanimno, inayoitwa UVB, “huonekana kana kwamba inapunguza uwezo wa mfumo wa kinga. Mtu anapokuwa na vidonda vya ngozi, mfumo wake wa kinga unashindwa kupigana na virusi vya Herpes simplex na hivyo kusababisha maambukizo.”

Hivyo basi, miale ya jua inaposababisha kansa inaweza kuathiri sehemu mbili. Kwanza, inaweza kuharibu chembe za DNA, na pili, kupunguza uwezo wa asili wa kinga ya mwili wa kukabiliana na madhara hayo.

Hivyo basi, tunahitaji kujikinga ili tusipigwe na miale ya jua kwa muda mrefu. Huenda afya na hata uhai wetu ukawa hatarini.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Ili upate habari zaidi kuhusu kansa ya ngozi, ona Amkeni! la Juni 8, 2005 (8/6/2005), ukurasa wa 3-10.

[Sanduku katika ukurasa wa 11]

JINSI YA KUJILINDA

▪ Usitumie muda mwingi kwenye jua wakati wa mchana kati ya saa 4:00 asubuhi na saa 10:00 jioni, ambapo miale hatari ya jua huwa na nguvu zaidi.

▪ Ikiwezekana, kaa chini ya kivuli.

▪ Funika mikono na miguu kwa kutumia vazi lisilopenyeza mwangaza na lisilobana mwili.

▪ Valia kofia pana ili kulinda macho, masikio, uso, na sehemu ya nyuma ya shingo lako.

▪ Miwani mizuri inayozuia miale ya urujuanimno kwa asilimia 99 hadi 100 inaweza kupunguza hatari ya kuharibika macho.

▪ Tumia losheni ya kujikinga na jua yenye kinga (SPF) namba 15 hivi, na ujipake tena kila baada ya saa mbili.

▪ Hakikisha kwamba unawakinga watoto, kwa sababu ngozi yao inaweza kuathiriwa kwa urahisi.

▪ Usilale usingizi kamwe ukiwa kwenye jua.

▪ Ukipatwa na baka, madoadoa, au doa jeusi linalokupa wasiwasi, mwone daktari.