Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
▪“Tunakabili janga kubwa sana [mzozo wa kisiasa nchini Georgia] . . . Mungu yuko pamoja nasi na Bikira Maria anatulinda, lakini kuna jambo linalotuhangaisha sana—kwamba wafuasi wa Kanisa Othodoksi la Urusi wanawapiga kwa mabomu wafuasi wa Kanisa Othodoksi la Georgia.”—ASKOFU MKUU WA KANISA OTHODOKSI LA GEORGIA, ILLIA WA PILI.
▪ “Idadi ya watu wanaoomba dawa ya dharura ya kupanga uzazi, yaani tembe ya kutoa mimba, iliongezeka mara tatu katika miezi sita iliyopita na uuzaji wa dawa hiyo umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 200 tangu 2004. . . . Simu nyingi kutoka kwa watu wanaoomba dawa hiyo hupokewa siku ya Jumatatu. Wengi wanaoomba dawa hiyo ni vijana wanaobalehe.”—CLARÍN, ARGENTINA.
▪ Nchini Marekani, watu wanaotumia simu za mkononi walio na umri wa kati ya miaka 13 na 17 “walituma au kupokea wastani wa ujumbe mfupi 1,742 kwa mwezi katika miezi ya Aprili, Mei, na Juni [mwaka wa 2008].”—THE NEW YORK TIMES, MAREKANI.
▪ “Asilimia 12 ya watu ulimwenguni pote wana matatizo ya akili.”—SHIRIKA LA ULIMWENGUNI POTE LA AFYA YA AKILI, MAREKANI.
▪ “Huko Ulaya, inakadiriwa kwamba mmoja kati ya watu watano amewahi kutumia bangi wakati fulani maishani.”—KITUO CHA ULAYA CHA KUCHUNGUZA DAWA NA URAIBU WA DAWA ZA KULEVYA, URENO.
Majina Yaliyo Katika Biblia Yapatikana
Wachimbuaji wa vitu vya kale waliokuwa wakichimba karibu na Jiji la Daudi la kale huko Yerusalemu wamechimbua muhuri uliotiwa miaka 2,600 iliyopita kwenye chombo cha udongo, kinachoitwa bulla, ulio na jina la “Gedalia mwana wa Pashuri.” Gedalia anatajwa katika Biblia kwenye andiko la Yeremia 38:1. Andiko hilo pia linataja “Yukali [ufupisho wa Yehukali (Yehukhali)] mwana wa Shelemia” ambaye jina lake lilipatikana kwenye bulla katika eneo hilohilo mnamo 2005. Wanaume hao wawili walikuwa maofisa wa makao ya Mfalme Sedekia. Jarida The Jerusalem Post linaripoti hivi: “Hii ndiyo mara ya kwanza katika maandishi ya kihistoria huko Israel kwa bulla mbili za udongo zenye majina mawili yanayotajwa katika mstari uleule wa Biblia kuchimbuliwa katika eneo moja.”
Tekinolojia Yatumiwa Kukabiliana na Uhalifu
Idara ya Polisi ya New York hupokea simu nyingi zaidi za dharura kutoka kwa raia. Hivi karibuni, maendeleo katika tekinolojia yamefanya iwezekane kuwasiliana na polisi kwa kuwatumia ujumbe mfupi kutoka kwenye simu ya mkononi. “Sasa raia wanatiwa moyo watumie simu zao za mkononi kupiga picha za video vitendo vya uhalifu na kisha kuwatumia polisi video hizo,” linaripoti gazeti The New York Times. Gazeti hilo linaendelea kusema kwamba mipango inafanywa “ili kuwezesha Kituo Maalumu cha Kukabiliana na Uhalifu kitume picha kwa magari yote ya polisi yanayoshika doria katika eneo ambalo uhalifu umefanywa.”
Magpie Hujitambua
“Ilidhaniwa kwamba ni sokwe, pomboo na ndovu tu ndio walio na uwezo kama wa mwanadamu wa kuitambua miili yao katika kioo,” inasema ripoti ya Reuters. Sasa, ndege aina ya magpie wanaopatikana huko Ulaya na Asia wamejiunga na “kikundi” hiki, ingawa ilidhaniwa kwamba ni wanyama wachache tu walio na uwezo huo. Watafiti waliwatia ndege hao doa kwa kutumia rangi ambayo wangeiona tu katika kioo. Ripoti hiyo ilisema kwamba “ndege hao waliikwaruza-kwaruza alama iliyotiwa kwenye mwili wao, na hivyo kuthibitisha kwamba waliitambua miili yao walipoiona katika kioo bila kufikiri kwamba ni mnyama mwingine.”