Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sloth—Mnyama Mvivu Sana

Sloth—Mnyama Mvivu Sana

Sloth—Mnyama Mvivu Sana

“LETA kamera yako haraka!” Nilimwambia dada yangu nilipomwona mnyama wa kijani anayeitwa sloth mbele yangu. Tulicheka tulipotambua hakukuwa na sababu ya kuharakisha kwa kuwa mnyama huyo ni mmoja kati ya wanyama wanaosonga polepole zaidi ulimwenguni.

Ili nijifunze zaidi kuhusu mnyama huyo, nilitembelea Hifadhi ya Wanyama ya Ave huko La Garita de Alajuela, Kosta Rika. Hiyo si hifadhi tu bali pia ni kituo cha kuokoa, kutunza, na kurudisha wanyama msituni. Nilikutana na mwanabiolojia Shirley Ramírez, msimamizi wa utafiti katika hifadhi hiyo. Alinionyesha sloth wa hifadhi hiyo anayeitwa Pelota, jina ambalo katika Kihispania linamaanisha “mpira.” Wanyama hao hujikunja kama mpira wanapolala. Pelota ana vidole viwili vikubwa, na ukubwa kama wa mbwa mdogo, ana manyoya mengi, pua fupi, na macho makubwa ya rangi ya kahawia.

Nilijifunza kwamba wanyama hao hupenda kukaa peke yao, nao huzaa mtoto mmoja mara moja hivi kwa mwaka. Mtoto hubebwa na mama yake kwa majuma manne hadi sita hadi anapoachishwa kunyonya lakini huenda akaendelea kubebwa na mama yake juu ya tumbo kwa miezi mitano hadi nane baadaye. Wakati huo mama hutumia mdomo wake kumlisha mtoto wake majani laini yanayoweza kumeng’enywa kwa urahisi. Baadaye, mtoto huanza kujichukulia majani yake mwenyewe bila kumwachilia mama. Wakati wanapokuwa pamoja, mama humwonyesha mtoto eneo dogo la nyumbani ambamo atapaswa kuishi.

Aina Mbalimbali za Sloth

Niligundua kwamba mnyama niliyemwona msituni ana vidole vitatu. Alikuwa na manyoya meusi kuzunguka macho yake, mkia mfupi mnene, manyoya membamba, miguu mirefu ya mbele kuliko ya nyuma, na manyoya ya manjano katikati ya mabega yake. Kwenye shingo, aina hii ya sloth ana mifupa tisa iliyounganishwa kwenye uti wa mgongo na hilo humwezesha kuzungusha kichwa chake hadi aone mgongo wake. Lakini kwa nini anaonekana kuwa na rangi ya kijani? Shirley anasema, “Rangi hiyo ya kijani ni miani inayokua kwenye manyoya yake.”

Tofauti na sloth wenye miguu mirefu ya mbele na vidole vitatu vikubwa, wale wenye vidole viwili vikubwa wana miguu inayotoshana. Wana manyoya marefu, laini, ya rangi ya kahawia.

Mnyama huyo hujianika juani kwa muda mrefu sana juu ya miti. Usiku joto la mwili wake linaweza kufikia nyuzi 24 Selsiasi na mchana linaweza kufikia nyuzi 33 Selsiasi. Hakuna mnyama mwingine anayenyonyesha anayeweza kustahimili badiliko kubwa kama hilo la joto mwilini. Sloth ana misuli michache sana mwilini hivi kwamba hawezi kutetemeka ili kudumisha joto mwilini. Hiyo ndiyo sababu mara nyingi analala akiwa amejikunja kama mpira ili kudumisha joto. Manyoya yake mafupi na laini humsaidia kuhifadhi joto. Naam, mnyama huyo anaweza kulala kwa saa 20 kwa siku!

Anakula Polepole Sana

Kwa kuwa ili chakula kimeng’enywe mwili unahitaji kuwa na joto kwa ajili ya utendaji wa bakteria na uchachishaji, kiasi kidogo cha joto katika mwili wa sloth humfanya asiweze kumeng’enya chakula chake haraka. Majani yanaweza kuchukua mwezi mzima kabla ya kupitishwa katika tumbo lake lenye sehemu nyingi na kuingia katika utumbo mdogo. Kwa sababu katika majira ya mvua kunakuwa na siku nyingi zenye baridi, wanyama hao wanaweza kufa njaa wakiwa wameshiba. Shirley anaeleza, “Jua ni muhimu sana ili sloth wameng’enye chakula.”

Shirley anaongezea hivi: “Mimi hutunza wanyama na kusafisha makao yao katika hifadhi hiyo, na jambo ninalopenda kuhusu wanyama hao ni kwamba wao huenda haja kubwa na haja ndogo mara moja tu kwa juma! Wanapotaka kwenda haja, wao hushuka chini na kuchimba shimo na kufunika kinyesi chao. Hilo tu ndilo jambo linalowafanya washuke chini!”

Wameumbwa Waning’inie Chini Juu

Wanyama hao hufanya karibu kila kitu wakiwa wamening’inia kwenye miti, iwe ni kula, kulala, kujamiiana, na kuzaa. Wanyama hao wadogo walikusudiwa na Muumba wao waishi wakiwa wamening’inia kwenye miti. Mnyama huyo hushikilia miti na mimea inayotambaa kwa kucha zake za mikono na miguu zilizo na urefu wa sentimita saba. Ili mnyama huyo asilowe maji wakati wa mvua kubwa, manyoya yake hukua chini juu! Manyoya yake ya tumboni hujigawanya mara mbili na hukua yakielekea chini, kinyume na manyoya ya wanyama wengine wa nchi kavu. Ingawa yeye hutembea kizembe anapokuwa kwenye nchi kavu, mnyama huyo hutembea taratibu na kwa madaha anapokuwa kwenye miti. Mnyama huyo pia ni mwogeleaji stadi!

Nilijifunza nini kingine kuhusu mnyama huyo mnyamavu anayeishi juu ya miti? Nilijifunza mambo mawili muhimu. Kwanza, ana uwezo wa ajabu wa kupona anapojeruhiwa na hata haathiriwi na sumu zinazowaua wanyama wengine. Majeraha yake hupona haraka, na hayaambukizwi kwa urahisi. Hivyo, kuelewa vizuri zaidi mfumo wa kinga wa mnyama huyo kutasaidia katika utafiti wa kitiba. Na pili, watu ambao kila wakati wanakazwa na pilikapilika nyingi wanaweza kufaidika, angalau kwa kiasi fulani, wakimwiga mnyama huyo ambaye hana haraka.—Tumetumiwa makala hii.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

“MKARIBISHAJI BORA”

Ushirikiano wake na miani ambayo hukua kwenye manyoya ya nje ya mnyama huyo humfanya awe na rangi ya kijani. Mnyama huyo huruhusu miani ikue kwenye manyoya yake, na miani hiyo humthawabisha kwa kumpa virutubisho ambavyo yeye huramba au vinaingia mwilini kupitia ngozi. Rangi hiyo ya kijani-kijivu humfanya aonekane kama majani yaliyokauka yanayoning’inia kwenye tawi na hilo humfanya asionekane kwa urahisi! Na kadiri mnyama huyo anavyozeeka, ndivyo manyoya yake yanavyozidi kuwa ya kijani!

[Hisani]

Top right: © Michael and Patricia Fogden; bottom: © Jan Ševčík