Tabàky—Kipodozi Kutoka Kwenye Mti
Tabàky—Kipodozi Kutoka Kwenye Mti
▪ Katika eneo kame lililo kusini-magharibi ya Madagaska, wanawake huenda kwenye ufuo kutafuta makoa ya kuwauzia watalii. Nyuso za wanawake hao zimepakwa mchanganyiko mweupe unaoitwa tabàky. Mchanganyiko huo ni kipodozi na pia hukinga uso kutokana na miale yenye kudhuru ya jua.
Tabàky hutengenezwa kutoka kwa sehemu laini ya nje ya mti wa masonjoany na fihamy (pia unaitwa aviavy). Ni rahisi kutengeneza mchanganyiko huo: Mwanamke huchukua kipande kidogo cha mti na kukisugua kwenye jiwe, kisha anaongeza matone machache ya maji polepole kwenye unga huo. Huenda akatumia kijiti kidogo cha mbao au plastiki yenye ncha kali au ya mviringo kuchota mchanganyiko huo na kuchora uso wake.
Wanawake fulani hupaka tabàky kwenye uso wao wote isipokuwa tu macho. Wengine hupendelea kuipaka kwenye kipaji, mashavu, au kidevu. Tabàky inaweza kutumiwa kuficha au kufunika alama zilizo usoni, kufanya uso using’ae sana, au kama kipodozi. Nyakati nyingine vitu vingine huongezwa ili kuwezesha mtu achore maumbo na rangi mbalimbali.
Ni nani angeweza kufikiri kwamba kipodozi kinaweza kutolewa kwenye mti? Huko Madagaska, tabàky ni kipodozi kizuri kisicho cha kawaida.