Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Makosa Yaliyoanzisha Vita vya Ulimwengu

Makosa Yaliyoanzisha Vita vya Ulimwengu

Makosa Yaliyoanzisha Vita vya Ulimwengu

Je, vita vya tatu vya ulimwengu vinaweza kuanza kwa aksidenti tu? Je, viongozi wa ulimwengu na washauri wa kijeshi wanaweza kukosea na kusababisha vifo vya mamilioni ya watu?

HATUJUI. Lakini tunajua kwamba jambo hilo liliwahi kutokea. Karne moja iliyopita, viongozi wa Ulaya waliingiza mataifa yao katika Vita Vikuu ambavyo vilikuja kuitwa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, bila kujua mauaji makubwa ambayo yangetokea. “Tulijiingiza katika vita bila kujua,” akakiri David Lloyd George, aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza kutoka 1916-1922. Fikiria matukio makuu yaliyoongoza kwenye mauaji hayo ya kikatili.

“Hakuna kiongozi aliyetaka kupigana katika vita vikubwa,” akaandika mwanahistoria A.J.P. Taylor, “lakini walitaka kutisha na kushinda.” Maliki wa Urusi alisema kwamba kila kitu kinapaswa kufanywa ili kudumisha amani. Hakutaka kulaumiwa kwa sababu ya mauaji ya kikatili. Lakini kwa njia fulani, mambo yalianza kuharibika risasi mbili zilipofyatuliwa mwendo wa saa 5:15 asubuhi, Juni 28, 1914 (28/6/1914).

Risasi Mbili Zilizobadili Ulimwengu

Kufikia mwaka wa 1914, uhasama kati ya serikali zenye nguvu za Ulaya ulisababisha wasiwasi kati ya mataifa na hivyo kutokeza miungano miwili iliyopingana: Shirikisho la Nchi Tatu, yaani, Austria-Hungaria, Italia, na Ujerumani na Maelewano ya Nchi Tatu, ya Uingereza, Ufaransa, na Urusi. Isitoshe, nchi hizo zilikuwa na mahusiano ya kisiasa na kiuchumi pamoja na nchi nyingine kutia ndani nchi kadhaa za eneo la Balkani.

Wakati huo, eneo linaloitwa Balkani lilikuwa na misukosuko ya kisiasa chini ya utawala wa mataifa hayo makubwa, na lilikuwa limejaa mashirika mengi ya siri yaliyokuwa yakipanga njama za kupata uhuru. Kikundi kidogo cha vijana katika eneo hilo kilipanga njama ya kumwua Dyuki Mkuu wa Austria, Francis Ferdinand, wakati wa ziara yake huko Sarajevo, mji mkuu wa Bosnia, Juni 28. * Kulikuwa na polisi wachache tu wakati huo na hivyo kurahisisha kazi yao. Hata hivyo, wauaji hao hawakuwa na uzoefu mwingi. Kijana mmoja alitupa bomu dogo lakini akakosa kulenga shabaha, na wenzake vilevile walishindwa kutimiza lengo lao wakati ulipofika. Gavrilo Princip, ndiye aliyefaulu, lakini alimwua bila kutarajia. Jinsi gani?

Princip alipomwona dyuki mkuu akimpita bila kuathiriwa na bomu hilo, alijaribu kukaribia gari lake lakini hakufaulu. Akiwa amekata tamaa alivuka barabara na kwenda kwenye mkahawa. Wakati huohuo, dyuki mkuu, akiwa amekasirishwa na jaribio hilo la kumwua, akaamua kutumia njia tofauti. Hata hivyo, dereva wake, ambaye hakujua kwamba mipango imebadilika, akaelekea upande usiofaa na ikambidi ageuze gari. Wakati huohuo, Princip alitoka kwenye mkahawa na kumwona dyuki mkuu akiwa ameketi kwenye gari lake ambalo halijafunikwa likiwa mita 3 tu mbele yake. Princip alikaribia gari hilo na kufyatua risasi mbili, na hivyo kumwua dyuki mkuu na mke wake. * Akiwa mzalendo wa Serbia, huenda Princip hakujua jinsi tendo lake lingeanzisha wimbi la matukio mabaya. Hata hivyo, kuna wengine wanaopaswa kulaumiwa kwa mambo yenye kuogopesha ambayo yangefuata.

Tayari kwa Ajili ya Vita

Kabla ya 1914, watu wengi huko Ulaya walipendezwa na vita. Licha ya kwamba walidai kuwa Wakristo waliona vita kuwa kitu chenye faida, chenye kuheshimiwa, na chenye kutukuzwa. Viongozi fulani walifikiri kwamba vita vingefanya nchi zao ziwe na umoja na kuwachochea watu! Isitoshe, majenerali fulani waliwahakikishia viongozi wao kwamba wangeweza kushinda vita haraka. “Tutashinda Ufaransa katika majuma mawili tu,” alijigamba jenerali Mjerumani. Hakuna mtu aliyetarajia kwamba mamilioni ya watu wangefyatuliana risasi kutoka kwenye mahandaki kwa miaka mingi.

Isitoshe, katika miaka kabla ya vita, “kulikuwa na msisimuko mkubwa sana wa uzalendo ulienea kotekote Ulaya,” kinasema kitabu Cooperation Under Anarchy. “Shule, vyuo vikuu, vyombo vya habari, na wanasiasa waliungana ili kuwachochea watu wawe wazalendo na kujitukuza.”

Viongozi wa kidini hawakufanya chochote kuzuia mtazamo huo wenye madhara. Mwanahistoria Paul Johnson anasema: “Kwa upande mmoja kulikuwa na Ujerumani ya Kiprotestanti, Austria ya Kikatoliki, Bulgaria ya Kiothodoksi, na Uturuki ya Kiislamu. Upande ule mwingine kulikuwa na Uingereza ya Kiprotestanti, Ufaransa na Italia za Kikatoliki, na Urusi ya Kiothodoksi.” Anaendelea kusema kwamba makasisi wengi “walisema kwamba ili uwe Mkristo mzuri lazima uwe mzalendo. Askari-jeshi Wakristo wa dini zote walihimizwa wauane kwa jina la Mwokozi wao.” Hata makasisi na watawa wa kike walihusishwa katika vita, na maelfu ya makasisi waliuawa vitani.

Miungano ya Ulaya ambayo ilikusudiwa kulinda watu dhidi ya vita vikubwa, huenda ndiyo iliyochangia vita hivyo. Kwa njia gani? “Serikali kubwa za Ulaya zilitegemeana ili kupata ulinzi,” kinasema kitabu Cooperation Under Anarchy. “Kila serikali ilihisi kwamba usalama wake ulitegemea serikali nyingine za muungano, na hivyo ilihisi inapaswa kutetea serikali hizo, hata ikiwa serikali hizo ndizo zilizochokoza maadui.”

Jambo lingine hatari lililochangia vita lilikuwa Mpango wa Schlieffen wa Ujerumani. Jina Schlieffen lilitokana na jina la aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Ujerumani, Jenerali Alfred von Schlieffen. Mpango huo ambao ulihusisha shambulizi moja la haraka, ulitegemea wazo la kwamba Ujerumani ingelazimika kupigana na Ufaransa na Urusi. Hivyo, lengo lilikuwa kushinda Ufaransa upesi Urusi ilipokuwa ikikusanya jeshi lake polepole, kisha washambulie Urusi. “Mpango wa [Schlieffen] ulipoanzishwa, mfumo wa miungano ulihakikisha kwamba kungekuwa na vita kotekote Ulaya,” kinasema kitabu World Book Encyclopedia.

Wimbi Laanza

Ingawa uchunguzi rasmi haukupata uthibitisho uliohusisha serikali ya Serbia katika mauaji ya dyuki mkuu, Austria ilikuwa imeazimia kukomesha uasi wa Waslavi katika milki hiyo kabisa. Austria ilitaka sana “kufunza Serbia somo,” anasema mwanahistoria J. M. Roberts.

Ili kujaribu kutuliza hali, Nicholas Hartwig, aliyekuwa balozi wa Urusi katika mji mkuu wa Serbia, alijitahidi kufanya pande hizo mbili zikubaliane. Lakini alipatwa na mshtuko wa moyo na akafa alipokuwa akikutana na wajumbe wa Austria. Mwishowe, Julai (Mwezi wa 7) 23, Austria ilitumia Serbia orodha ya matakwa waliyopaswa kutimiza. Kwa sababu Serbia haingekubali matakwa yote, Austria ilikatiza mara moja mahusiano yote nao. Wakati huo muhimu sana, mahusiano ya kidiplomasia yalikoma.

Hata hivyo, bado watu fulani walijaribu kuzuia vita. Kwa mfano, Uingereza ilipendekeza kuwe na kongamano la kimataifa, na kiongozi wa Ujerumani alimsihi maliki wa Urusi asikusanye jeshi. Lakini mambo yakaenda mrama. “Viongozi, majenerali, na mataifa mazima-mazima yalilemewa kabisa na matukio yaliyokuwa yakikaribia,” kinasema kitabu The Enterprise of War.

Julai 28, maliki wa Austria, akiwa amehakikishiwa kwamba Ujerumani itamuunga mkono, alitangaza vita dhidi ya Serbia. Urusi iliunga Serbia mkono na hivyo ikajaribu kutisha Austria kwa kukusanya wanajeshi milioni moja hivi kwenye mpaka wa Austria. Kwa sababu kufanya hivyo kungeacha mpaka wa Urusi na Ujerumani bila ulinzi, maliki wa Urusi aliamuru jeshi lote likusanywe.

Maliki huyo alijaribu kumhakikishia kiongozi wa Ujerumani kwamba hakutaka vita na Ujerumani. Hata hivyo, kukusanywa kwa jeshi la Urusi kulifanya Ujerumani itende kwa kasi, na Julai 31, Ujerumani ilianza kutekeleza mpango wa vita wa Schlieffen, na hivyo ikatangaza vita dhidi ya Urusi Agosti (Mwezi wa 8) 1, na siku mbili baadaye ikatangaza vita dhidi ya Ufaransa. Kwa sababu mipango ya vita ya Ujerumani ilihusisha kupitia Ubelgiji, Uingereza ilionya Ujerumani kwamba itatangaza vita dhidi yake ikiwa ingewaingiza Wabelgiji vitani. Majeshi ya Ujerumani yaliingia Ubelgiji Agosti 4. Sasa vita havingeweza kuepukwa.

“Msiba Mkubwa Zaidi wa Kidiplomasia Katika Nyakati za Kisasa”

“Uingereza ilipotangaza vita ilichangia msiba mkubwa zaidi wa kidiplomasia katika nyakati za kisasa,” akaandika mwanahistoria Norman Davies. Mwanahistoria mwenzake Edmond Taylor aliandika kwamba baada ya Austria kutangaza vita Julai 28, “kuchanganyikiwa kulichangia sana katika kuchochea [vita]. Mambo mengi sana yalikuwa yakitendeka upesi sana katika maeneo mengi sana. . . . Hata watu makini zaidi na wenye akili zenye utaratibu zaidi hawangeweza kuchanganua habari waliyomwagiwa kwa wakati mmoja.”

Raia na askari zaidi ya milioni 13 walikufa kwa sababu ya “kuchanganyikiwa” huko. Matumaini ya wakati ujao na ubinadamu uliathiriwa sana wakati watu wanaojiita wastaarabu walipojihami kwa silaha nyingi, mpya, na zenye nguvu, na kuchinjana kwa kadiri kubwa sana. Ulimwengu ulibadilika kabisa.—Ona sanduku  “Vita vya Ulimwengu—Je, Ni Ishara ya Nyakati?”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Sasa Bosnia ni sehemu ya Bosnia na Herzegovina.

^ fu. 8 Princip alimwua kimakosa mke wa dyuki mkuu. Alikuwa amekusudia kumwua gavana wa Bosnia, Jenerali Potiorek, aliyekuwa ndani ya gari hilo pamoja na dyuki mkuu na mke wake, lakini kitu fulani kilifanya asilenge shabaha.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 20]

 VITA VYA ULIMWENGU—JE, NI ISHARA YA NYAKATI?

Biblia ilitabiri kwamba vita vitakuwa sehemu ya ishara inayoashiria siku za mwisho za ulimwengu huu mwovu. (Mathayo 24:3, 7; Ufunuo 6:4) Utimizo wa ishara hiyo leo unaonyesha kwamba tunakaribia sana wakati ambapo serikali ya Ufalme wa Mungu itatawala kabisa dunia yote.—Danieli 2:44; Mathayo 6:9, 10.

Isitoshe, Ufalme wa Mungu utaondoa nguvu isiyoonekana inayoongoza mambo ya ulimwengu, yaani, roho waovu wanaoongozwa na Shetani Ibilisi. “Ulimwengu mzima unakaa katika nguvu za yule mwovu,” inasema 1 Yohana 5:19. Uvutano mbaya wa Shetani umechangia matatizo mengi ya wanadamu, bila shaka kutia ndani matukio yenye kusikitisha yaliyosababisha Vita vya Kwanza vya Ulimwengu.—Ufunuo 12:9-12. *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 30 Unaweza kupata habari zaidi kuhusu siku za mwisho na roho waovu katika kitabu cha kujifunzia Biblia kinachoitwa Biblia Inafundisha Nini Hasa? kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

[Hisani]

U.S. National Archives photo

[Picha katika ukurasa wa 19]

Kuuawa kwa Dyuki Mkuu Ferdinand

[Hisani]

© Mary Evans Picture Library