Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unavyoathiriwa na Tekinolojia ya Kutunza Siri!

Unavyoathiriwa na Tekinolojia ya Kutunza Siri!

Unavyoathiriwa na Tekinolojia ya Kutunza Siri!

Je, umewahi kujaribu kutafuta neno au sentensi ambayo herufi zake zimebadilishwa? Je, umewahi kununua kitu kupitia Intaneti au ukatumia kompyuta kupata rekodi zako za benki? Ikiwa ndivyo, basi umetumia maandishi ya siri kuficha au kufichua habari.

HADI hivi karibuni, maandishi ya siri yalitumiwa na serikali, mabalozi, wapelelezi, na jeshi. Lakini sasa watu wengi zaidi wanayatumia. Tangu kubuniwa kwa kompyuta na Intaneti, mara nyingi habari muhimu zinafichwa kwa kutumia vitu kama neno au namba ya siri ya utambulisho ambazo zinatumiwa kila mara mtu anapotaka kutazama rekodi zake. Kwa kweli, watu wanaficha sana habari zao siku hizi kuliko wakati mwingine wowote.

Hivyo, huenda tukajiuliza: Je, habari zangu za siri ziko salama? Ninaweza kufanya nini ili ziwe salama zaidi? Kabla ya kujibu maswali hayo, fikiria ushindani wa muda mrefu uliopo kati ya watu wanaotunga maneno ya siri na wale wanaoyatangua—ushindani ambao umekuwepo kwa muda mrefu kama maandishi yenyewe.

Maandishi ya Siri

Mbinu moja ya kuandika kwa siri ambayo imetumika kwa muda mrefu inaitwa steganography. Kusudi la mbinu hii ni kufanya ifikiriwe kwamba hakuna ujumbe wowote. Mwanahistoria wa kale Herodoto aliandika kwamba mhamishwa mmoja Mgiriki aliona kwamba Uajemi ilikuwa ikijitayarisha kuvamia nchi yake. Akitaka kuwaonya watu wake, aliandika ujumbe kwenye mabamba ya mbao na kuyafunika kwa nta ili kuficha ujumbe wake, mbinu ambayo ilitumiwa na Waroma wa kale. Kulingana na Herodoto, Mfalme Shasta wa Uajemi alipotaka kuwavamia Wagiriki wakiwa hawamtarajii, mbinu hii ilivuruga mipango yake na majeshi yake yakashindwa.

Mbinu za kisasa za steganography zinatia ndani matumizi ya maandishi yaliyopunguzwa ukubwa hadi kufikia ukubwa wa nukta ndogo sana na karatasi zenye maandishi au picha inayoweza kuonekana tu kwa kuielekeza kwenye mwanga. Wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, picha zilipunguzwa ukubwa na kutoshana na nukta. Yule anayepokea ujumbe huo alihitaji tu kuongeza ukubwa wa nukta hiyo. Leo, watu wanaosambaza ponografia (picha au habari za ngono) kinyume cha sheria wanatumia mbinu kama hiyo. Wakitumia programu za kompyuta, wanaficha picha hizo katika picha nyingine, maandishi, au rekodi zisizo na mambo machafu.

Kwa kuwa kusudi la mbinu hii ya steganography ni kufanya ifikiriwe kwamba hakuna ujumbe wowote, hakuna mtu anaweza kumshuku mjumbe na mwenye kuupokea. Lakini, ujumbe wenyewe ukigunduliwa unaweza kusomwa, isipokuwa maana yake iwe imefichwa.

Kuficha Maana

Mbinu inayoitwa cryptology ni mbinu ya kuwa na mawasiliano ya siri kwa kuficha si ujumbe bali maana yake. Mbinu hiyo inahusisha kuvuruga habari na kuipanga tena kwa kufuata mfumo wa sheria fulani na hivyo kuwezesha wale wanaoelewa mfumo huo kusoma ujumbe huo.

Wakazi wa kale wa Sparta walitumia kifaa kisicho na mambo mengi kilichoitwa scytale kuvuruga habari. Mtu aliyeandika maandishi ya siri alifunga kipande cha ngozi kwenye fimbo kwa kukizungusha, kisha akaandika kutoka juu kwenda chini kwenye ngozi hiyo. Ngozi hiyo ilipofunguliwa, ilionekana kuwa herufi hazina maana yoyote. Lakini mtu aliyekusudiwa kupata habari hiyo alipofunga ngozi hiyo kwenye fimbo nyingine yenye ukubwa uleule, angeweza kusoma maandishi hayo. Nyakati nyingine, mbinu ile nyingine ya steganography ingetumiwa pamoja na mbinu hii kwani mjumbe angefunga ngozi hiyo kama mshipi maandishi yakiwa upande wa ndani.

Inasemekana kwamba Kaisari Yulio alificha ujumbe wake wa vita kwa kubadilisha herufi, kama vile kubadili herufi ya kwanza na ile ya tatu. Kwa hiyo, a itaandikwa d, b iandikwe e, na kadhalika.

Kipindi cha Mwamko barani Ulaya kiliboresha mbinu ya kuficha maana inayoitwa cryptography. Mmoja kati ya watu walioboresha mbinu hiyo alikuwa Blaise de Vigenère, balozi wa Ufaransa aliyezaliwa mnamo 1523. Vigenère alipendekeza kutumia herufi moja iwakilishe herufi kadhaa mtu anaposoma ujumbe, mbinu iliyokuwa imevumbuliwa mapema. Mbinu yake ambayo ilifikiriwa kuwa haiwezi kutanguliwa na hivyo ikasemwa kuwa “kuficha kisichoweza kufichuliwa” (le chiffre indéchiffrable). Hata hivyo, maendeleo yaleyale yaliyofanywa katika kuficha maandishi yalisawazishwa na maendeleo katika mbinu za kufichua maandishi.

Kwa mfano wasomi Waislamu walipochanganua Kurani, iliyoandikwa katika Kiarabu, waligundua kwamba herufi fulani zilitumiwa mara nyingi zaidi kuliko nyingine, jambo linaloonekana katika lugha nyingine pia. Ugunduzi huo ulisaidia katika kusitawishwa kwa mbinu ya kufichua maandishi kwa kutegemea mara ambazo herufi au vikundi fulani vya herufi vinatokea katika ujumbe wa siri.

Kufikia karne ya 15, ilikuwa kawaida kwa mabalozi wa Ulaya kutumia mbinu hii ya cryptography. Lakini haikuwa rahisi kuhakikisha kwamba ujumbe unabaki ukiwa siri. Kwa mfano, Mfaransa François Viète alitangua ujumbe wa siri uliotumwa kwa mfalme wa Hispania. Isitoshe, alifaulu mara nyingi sana hivi kwamba Mfalme Filipo wa Pili alisema kuwa Viète alikuwa akisaidiwa na Ibilisi na kwamba anapaswa kufikishwa mbele ya mahakama ya Kikatoliki!

Tekinolojia Yaanza Kutumiwa

Mbinu za kuficha maana ya ujumbe zilichukua mkondo mpya katika karne ya 20 hasa wakati wa vile vita viwili vya ulimwengu, kwa kuwa mashini tata sana zilianza kutumiwa kama ile ya Ujerumani inayoitwa Enigma, ambayo ni mashini inayofanana sana na taipureta. Mtu anapochapa maneno, mfumo fulani wa umeme unabadili maandishi hayo kuwa ya siri. Kisha ujumbe huo unatumwa kwa kutumia njia ya mawasiliano ya Morse na unatanguliwa kwa kutumia Enigma nyingine. Hata hivyo, makosa na hali ya kutojali ya watu wanaochapa yaliwasaidia watu wanaotangua ujumbe wa siri kupata habari zilizowawezesha kutangua maandishi ya siri yaliyokuwa yakitumwa.

Leo habari nyingi zinahifadhiwa kupitia kompyuta, kuweka pesa katika benki, kutuma pesa, malipo mbalimbali, pia rekodi kuhusu tiba, biashara, na serikali zinalindwa kupitia maandishi ya siri. Habari hizo za siri zinasomwa na wale ambao wana ufunguo wa kuzirudisha katika hali ya kawaida.

Ufunguo wa chuma una mabonde mbalimbali, ufunguo wa kompyuta ni mchanganyiko wa nambari sufuri na moja zilizofuatana. Ufunguo mrefu una mchanganyiko wa nambari nyingi zaidi, na inakuwa vigumu kuutangua. Kwa mfano, ufunguo wenye nambari nane, unaweza kuchanganywa mara 256, lakini ufunguo wenye nambari 56 unaweza kuchanganywa zaidi ya mara quadrillion 72. Kwa sasa ufunguo wenye nambari 128 ndio unaotumiwa kuficha habari kwenye Intaneti. Ufunguo huo unaweza kuchanganywa mara sextillion 4.7 zaidi ya ufunguo wenye nambari 56! *

Hata hivyo, bado maneno ya siri hutanguliwa. Kwa mfano, mnamo 2008, waendesha-mashtaka wa serikali nchini Marekani waliwashtaki wanaume 11 kwa kile kinachosemekana kuwa wizi mbaya zaidi wa vitambulisho. Ilisemekana kwamba wezi hao walitumia kompyuta, tekinolojia isiyotumia nyaya, na programu fulani za pekee za kompyuta ili wapate namba za kadi za benki watu walipokuwa wakizitumia kulipa.

Je, Habari Zako za Siri Ziko Salama?

Ni kweli kwamba si rahisi kutangua maandishi ya siri yanayolinda akaunti yako ya benki na ununuzi unaofanya kupitia kompyuta. Lakini mengi yanakutegemea. Biblia inasema: “Mtu mwerevu ni yule ambaye ameona msiba na kujificha, lakini wasio na uzoefu wameendelea mbele nao lazima waumie.” (Methali 22:3) Kwa hiyo, uwe mwerevu na “kujificha” ili usiibiwe au kufanyiwa ulaghai kwa kuchukua hatua zifuatazo:

▪ Tumia programu za kompyuta za kuzuia virusi.

▪ Weka programu za kutambua mtu anapotaka kuingia katika kompyuta yako.

▪ Weka programu ya kumzuia mtu asiingie katika kompyuta yako.

▪ Hakikisha kwamba programu zilizotajwa juu ni za kisasa kila wakati, na uweke mfumo kuboresha ulinzi kila wakati.

▪ Jihadhari na mialiko ya kutumia Intaneti inayotumwa kupitia barua-pepe au ujumbe mfupi, hasa ikiwa barua hiyo inatoka kwa mtu usiyemfahamu na inaomba utume habari za kibinafsi au utume neno au namba ya siri ya utambulisho.

▪ Unapotuma habari muhimu sana, kama vile habari kuhusu kadi ya benki, tumia vituo vya Intaneti vyenye uwezo kuficha habari, na ufunge kituo hicho mara tu unapomaliza. *

▪ Chagua neno au namba ya siri ya utambulisho ambazo si rahisi mtu afikirie, na uzilinde.

▪ Usinakili au kutumia programu za kompyuta kutoka katika vyanzo usivyovijua.

▪ Uwe na kawaida ya kunakili habari zako, na uzihifadhi mahali salama.

Ukifuata hatua hizo za msingi za kujilinda na nyingine zozote zinazofaa sasa au wakati ujao, utakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kulinda habari zako za siri.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 19 Quadrillion ni nambari 1 ikifuatwa na sufuri 15. Sextillion ni nambari 1 ikifuatwa na sufuri 21.

^ fu. 28 Vituo vya Intaneti vyenye uwezo wa kuficha habari vina ishara fulani, kama vile ishara ya kufuli au “https://” kwenye kisanduku cha anwani. Herufi s inamaanisha salama (secure).

[Picha katika ukurasa wa 26]

“Scytale” ya kale ya Sparta

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mashini ya karne ya 20 ya Ujerumani inayoitwa “Enigma”

[Picha katika ukurasa wa 26]

Leo maandishi ya siri hulinda habari za kibinafsi