Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Herode Mkuu—Mjenzi Stadi

Herode Mkuu—Mjenzi Stadi

Herode Mkuu—Mjenzi Stadi

ALITAWALA kwa miaka 30 hivi, zaidi ya miaka 2,000 iliyopita. Alitawala kutoka Yudea na mamlaka yake ilienea mpaka maeneo fulani ya karibu. Vitabu vya historia vinamwita Herode Mkuu.

Herode anajulikana sana kama mwuaji watu wa familia yake na pia wavulana kwa sababu ya wivu. Wanajimu kutoka Mashariki walipomwambia kwamba mfalme wa wakati ujao alikuwa amezaliwa, Herode alisingizia kwamba alitaka kumwabudu mtoto huyo. Aliwaambia wakamtafute mtoto huyo na warudi kumpasha habari. Lakini Mungu alipowaonya wanajimu wasirudi kwake, Herode aliamuru wavulana wote wenye umri wa miaka miwili na chini huko Bethlehemu, jiji ambalo wanajimu hao walimpata Yesu, na wilaya zinazozunguka, wauawe.—Mathayo 2:1-18.

Hata hivyo, mapema maishani Herode aliwavutia watu sana kwa sababu ya miradi yake ya ujenzi. Alijenga mahekalu, viwanja vya michezo, viwanja vya mashindano ya magari yaliyokokotwa na farasi, na mifereji, kutia ndani majumba makubwa ya kifalme yenye bafu za kifahari. Miradi yake ilikuwa yenye kustaajabisha, hata imewastaajabisha mainjinia wa nyakati za kisasa wanaochunguza maeneo hayo.

Herode alichagua maeneo ambayo yangefanya majengo yake yaonekane yenye fahari na yenye kutokeza na yangefaana na mazingira. Majumba yake ya kifalme yalipambwa kwa michoro maridadi, sanaa za chokaa, na sakafu za mawe zilizotiwa nakshi. Pia alijenga bafu za Kiroma huko Yudea, zenye vyumba vya mvuke wenye joto jingi na joto kiasi ambao mfumo wake wa kupasha joto ulijengwa chini ya sakafu. Kwa kweli, alijenga majiji mazima, moja likiwa na bandari isiyo ya kiasili.

Kaisaria—Jiji la Bandarini

Herode alijenga mojawapo ya bandari kubwa zaidi katika ulimwengu wa Roma huko Kaisaria. Ukubwa wake umewashangaza hata wachimbuaji wa vitu vya kale. Kulikuwa na nafasi ya meli 100 kutia nanga, na hilo linaonyesha kwamba wakati mmoja Kaisaria lilikuwa kituo cha kibiashara cha kimataifa.

Gati na kuta za kuzuia mawimbi zilijengwa kwa kutumia tekinolojia ya hali ya juu sana. Hata hivyo, wasomi walishangazwa na jinsi ambavyo wafanyakazi wangeweza kubeba mawe makubwa ambayo mwanahistoria Myahudi Flavio Yosefo alisema yalikuwa na urefu wa mita 15 hivi, upana wa mita 3 hivi, na kimo cha mita 3 hivi. Hivi karibuni, wapiga-mbizi wamegundua kwamba mawe ambayo Herode alitumia yametengenezwa kwa zege. Ili wajenge gati na kuta za kuzuia mawimbi, wafanyakazi walimwaga zege katika viunzi vya mbao, na kisha wakaingiza mawe hayo chini ya maji na kuyashindilia.

Jiji hilo la bandarini lililojengwa kwa mpangilio mzuri sana lilikuwa na hekalu lililowekwa wakfu kwa Kaisari Agusto, jumba la kifalme, kiwanja cha mashindano ya magari yaliyokokotwa na farasi, jumba la maonyesho linaloweza kutoshea watu 4,000, na mfumo wa kuondoa maji-taka wa chini ya ardhi. Mifereji na njia za chini ya ardhi ziliingiza maji baridi jijini Kaisaria kutoka kwenye chemchemi za Mlima Karmeli ulioko umbali wa kilomita 6 hivi.

Yerusalemu na Hekalu la Herode

Mradi mkubwa zaidi wa Herode ulikuwa ujenzi wa hekalu la Yerusalemu. Hekalu la awali lilijengwa na Mfalme Sulemani, ambaye alifuata ramani za ujenzi za baba yake Daudi, ambaye alizipokea kutoka kwa Mungu. (1 Wafalme 6:1; 1 Mambo ya Nyakati 28:11, 12) Hekalu hilo liliharibiwa na Wababiloni miaka 420 hivi baadaye, na miaka 90 hivi baadaye, mahali pake palichukuliwa na jengo lisilo la kifahari sana lililojengwa na Gavana Zerubabeli wa Yuda.

Yosefo aliandika hivi kuhusu hekalu ambalo Herode alijenga mahali hapo: Lilikuwa “limefunikwa pande zote kwa mabamba makubwa ya dhahabu, punde tu jua lilipochomoza, hekalu hilo liliangaza sana hivi kwamba watu waliojaribu kulitazama walilazimika kufunika macho yao, kana kwamba walikuwa wakimulikwa na jua lenyewe. Kwa umbali wageni waliliona kuwa kama mlima uliofunikwa kwa theluji; kwa kuwa chochote ambacho hakikufunikwa kwa dhahabu kilikuwa cha rangi nyeupe pepepe.”

Maelfu ya watu walishiriki katika ujenzi wa kuta za hekalu, ambazo kwenye upande wa magharibi zilikuwa na urefu wa mita 500 hivi. Hayo mawe makubwa hayakuunganishwa kwa saruji. Jiwe moja lilikuwa na uzito wa tani 400 hivi na kulingana na msomi mmoja “hakuna mawe mengine yanayoweza kulinganishwa nayo kwa ukubwa katika ulimwengu huo wa kale.” Si ajabu kwamba wanafunzi wa Yesu walistaajabu! (Marko 13:1) Zaidi ya kuta hizo kulikuwa na jukwaa kubwa lililoitwa Eneo la Hekalu la Mlimani, ambalo ndilo jukwaa kubwa zaidi lililojengwa katika ulimwengu wa kale. Ukubwa wa jukwaa hilo ulikuwa sawa na zaidi ya viwanja 25 vya mpira.

Herode alijenga majengo mengine huko Yerusalemu. Moja kati ya majengo hayo ilikuwa ile ngome ya Antonia, iliyoungana na hekalu alilojenga hapo awali. Pia Herode alijenga jumba la kifalme, na vilevile akajenga minara mitatu yenye orofa kadhaa kwenye malango ya jiji.

Samaria na Yeriko

Kaisari Agusto alimpa Herode jiji la kale la Samaria kama zawadi, naye akabadili jina la Samaria kuwa Sebaste. Alirembesha jiji hilo kwa majengo mbalimbali, huenda majengo hayo yalitia ndani uwanja wa michezo uliozungukwa na nguzo nyingi. Pia, alijenga majengo mengi makubwa yaliyopambwa kwa picha zilizochorwa ukutani.

Jiji la Yeriko liko mita 250 hivi chini ya usawa wa bahari katika Bonde la Yordani ambalo huwa na hali nzuri ya hewa. Yeriko lilikuwa na ukubwa wa ekari 2,500 hivi na lilifanana na jiji la bustani. Herode alijenga jumba la kifalme la majira ya baridi kali katika jiji hilo. Aliunganisha majumba matatu ya kifalme kuwa jengo moja kubwa na kuhakikisha kwamba kila jumba lilikuwa na eneo la mapokezi, mabafu, bustani, na mabwawa ya kuogelea. Si ajabu kwamba alipenda kukaa Yeriko wakati wa majira ya baridi kali!

Majumba ya Kifalme ya Kifahari

Hata hivyo, Herode alikuwa na majumba mengine ya kifalme aliyoyatumia katika majira ya baridi kali. Alijenga ngome kwenye mwamba tambarare ulioinuka zaidi ya mita 400 juu ya Bahari ya Chumvi unaoitwa Masada. Katika eneo hilo, alijenga jumba la kifalme lenye orofa tatu lililokuwa na veranda na vidimbwi vya kuogea, na pia jumba lingine la kifalme lililokuwa na bafu zenye mabomba ya kupasha maji moto na choo cha kuvuta maji!

Katika eneo hilo la jangwani, Herode alijenga mahali ambapo angestarehe na kuboresha afya yake. Alijenga visima 12 ambavyo vingeweza kubeba lita milioni 40 hivi za maji. Kwa kuwa ngome hiyo pia ilikuwa mfumo mzuri wa kukusanya na kuhifadhi maji ya mvua, kulikuwa na maji ya kutosha kwa ajili ya kilimo, kuoga, na kuogelea.

Mradi mwingine wenye kustaajabisha ulikuwa ujenzi wa jumba la kifalme lenye ngome linaloitwa Herodium, lililojengwa kwenye mlima ulioinuka ambao ulikuwa karibu kilomita 5 kusini mashariki ya Bethlehemu. Jumba hilo lilikuwa na sehemu mbili kuu: Herodium ya Juu na Herodium ya Chini. Sehemu ya juu ya ilikuwa na jumba la kifalme lililojengwa kama ngome lililokuwa na mnara wenye orofa tano upande wa mashariki ambalo wakati mmoja lilikuwa jengo refu zaidi katika eneo hilo lakini sasa ni magofu. Miaka miwili iliyopita vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa viliripoti kwamba magofu ya kaburi la Herode yaligunduliwa katika miteremko ya Herodium, na vilisema kwamba hilo lilithibitisha ripoti ya Yosefo wa karne wa kwanza kwamba kulikuwa na msafara wa mazishi ya Herode hapo.

Wakati mmoja, kulikuwa na ofisi na majengo mengine madogo kando ya jumba la kifalme la Herodium ya Chini. Katikati kulikuwa na bustani ya Kiroma iliyopambwa kwa nguzo na iliyozunguka bwawa kubwa lililokuwa na kisiwa bandia katikati. Bwawa hilo lilikuwa na ukubwa karibu maradufu wa bwawa la kisasa la Olimpiki. Bwawa hilo lilitumiwa hasa kama hifadhi ya maji, lakini pia lilikuwa bwawa la kuogelea na hata kuendesha mashua. Maji yaliingia kwenye bwawa hilo kupitia mfereji uliotoka kwenye chemchemi iliyokuwa umbali wa kilomita 5.

Miaka kadhaa iliyopita, mtu fulani aliyetembelea eneo hilo alisema hivi kuhusu mandhari yake: “Upande wa mashariki, ungeweza kuona eneo lote hadi Bahari ya Chumvi. Mbele yetu kulikuwa na nyika ya Yudea ambapo huenda ndipo Daudi alijificha kutoka kwa Sauli, aliyekuwa akimsaka. Tulipotazama eneo hilo lililojaa mawe, tulielewa jinsi Daudi angeweza kujificha hapo hasa tukizingatia kwamba alilijua eneo hilo vizuri tangu ujana wake. Pia tuliwazia kwamba alipokuwa akilisha kondoo wake, huenda mara kwa mara Daudi alipanda mlima huo ili atazame mandhari nzuri tuliyokuwa tukiitazama.”

Vitabu vingi vimeandikwa kuhusu miradi ya ujenzi ya Herode. Kumekuwa na makisio mengi kuhusu ni kwa nini Herode alianzisha miradi mingi ya ujenzi. Wengine wamesema kwamba alifanya hivyo ili ajiletee sifa au ajinufaishe kisiasa. Iwe nia yake ilikuwa nini, uchunguzi huu mfupi umethibitisha kwamba ingawa Herode Mkuu alikuwa mtawala mkatili, alikuwa pia mjenzi stadi.

[Picha katika ukurasa wa 25]

KAISARIA

Mchoro wa msanii

[Picha katika ukurasa wa 25]

KASRI LA YERUSALEMU

Mfano

[Picha katika ukurasa wa 25]

HEKALU LA HERODE

Mfano

[Picha katika ukurasa wa 26]

MASADA

Magofu ya kasri lenye orofa tatu

[Hisani]

Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.

[Picha katika ukurasa wa 26]

“HERODIUM”

Mchoro wa msanii

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Caesarea: Hiram Henriquez/National Geographic Stock; Palace: Courtesy of Israel Museum, Jerusalem, and Todd Bolen/Bible Places.com