Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kilimo cha Kisasa Kimebadili Ulimwengu

Kilimo cha Kisasa Kimebadili Ulimwengu

Kilimo cha Kisasa Kimebadili Ulimwengu

UNAPATAJE chakula chako? Je, unakinunua au unakikuza mwenyewe? Si zamani sana wanadamu wengi walikuwa wakulima wanaokuza mazao kwa ajili tu ya kujilisha wenyewe. Lakini sasa katika nchi fulani zilizoendelea kiviwanda, ni mtu 1 kati ya watu 50 anayekuza vyakula vyake mwenyewe. Mabadiliko hayo yalianzaje?

Maendeleo katika ukulima yalianza polepole kisha yakapamba moto. Kila hatua ya maendeleo ilileta mabadiliko makubwa kwa familia nyingi, na bado yanaendelea ulimwenguni pote. Kuchunguza jinsi maendeleo katika kilimo yalivyoathiri watu kutakusaidia kuelewa ulimwengu wa sasa.

Mabadiliko Makubwa Yaanza

Kwa kushangaza, katika karne ya 12 mbinu ya kutumia farasi waliofungwa ukanda shingoni huko Ulaya ilikuwa hatua moja muhimu iliyofanya watu waache kukuza mazao kwa ajili tu ya kujilisha wenyewe. Iliwezesha farasi kufanya kazi bila kujinyonga. Farasi waliofungwa wangeweza kuvuta kwa nguvu, kasi, na kwa muda mrefu zaidi kuliko fahali waliokuwa wakitumiwa hapo awali. Kwa kutumia nguvu hizo za farasi, wakulima wangeweza kukuza chakula kingi. Wangeweza kutumia plau za chuma kulima mashamba ambayo hayangeweza kulimwa hapo awali. Hatua nyingine muhimu ilikuwa kukuza mazao kama vile maharagwe, njegere, klova, na alfalfa ambayo yangeweza kurutubisha ardhi kwa nitrojeni. Udongo wenye rutuba ulizalisha mazao mengi zaidi.

Maendeleo hayo ya mapema yalitosha kuwasaidia wakulima kuzalisha chakula cha ziada ili wakauze. Hilo lilisababisha miji kukua ambako watu wangeweza kukunua chakula chao na kufanya kazi viwandani na kufanya biashara. Baadhi ya matajiri waliokuwa wakitokeza bidhaa viwandani, wafanyabiashara, na wakulima walikuja kuwa wabuni wa mashini za kwanza za kulima.

Katika mwaka wa 1700 hivi, Jethro Tull, mkulima Mwingereza, alivumbua mashini ya kupanda mbegu iliyokokotwa na farasi ambayo ilichukua mahali pa kupanda mbegu kwa mikono, mbinu iliyopoteza mbegu nyingi. Mnamo 1831, huko Marekani, Cyrus McCormick, alivumbua mashini ya kuvuna iliyokokotwa na farasi. Mashini hiyo ingeweza kuvuna nafaka mara tano zaidi ya mtu moja akitumia mundu. Pia wakati huohuo, wafanyabiashara walianza kuleta mbolea Ulaya kutoka pwani ya Milima ya Andes huko Amerika Kusini. Kutumiwa kwa mashini na mbolea kulitokeza mazao mengi shambani. Lakini hilo liliwaathirije watu?

Maendeleo katika mbinu za ukulima yalisababisha mvuvumko wa kiviwanda kwa kufanya miji iwe na vyakula vingi vya bei rahisi. Mvuvumko huo ulitukia kwanza huko Uingereza katika mwaka wa 1750-1850 hivi. Maelfu ya familia zilihamia miji yenye viwanda ili watu wakafanye kazi katika migodi ya makaa ya mawe, viwanda vya kufua vyuma, vya kutengeneza meli, na vya nguo. Hali ziliwalazimisha kufanya hivyo. Wakulima wadogo hawangeweza kugharimia mbinu hizo mpya za ukulima kwa hiyo walipokea malipo madogo kwa chakula walichokuza na hivyo hawangeweza kulipa kodi ya nyumba. Walilazimika kuacha mashamba yao na kuishi katika mitaa ya mabanda yaliyosongamana na yenye magonjwa mengi. Badala ya familia kulima pamoja, wanaume walilazimika kufanya kazi mbali na nyumbani. Hata watoto walifanya kazi kwa saa nyingi viwandani. Punde si punde, mataifa mengine yaliathiriwa pia na mabadiliko hayo.

Sayansi Yaleta Mabadiliko Zaidi

Kufikia mwaka wa 1850, mataifa fulani yalikuwa na ufanisi wa kutosha kugharimia utafiti wa kilimo. Uchunguzi wa kilimo umeendelea kuleta mabadiliko hata katika siku zetu. Kwa mfano, wazalishaji wa mimea wamechunguza mbegu za urithi na kutokeza mimea inayoweza kuzaa sana na kustahimili magonjwa. Watafiti pia wamegundua mchanganyiko unaofaa wa nitrati na fosfati kwa ajili ya mimea na udongo mbalimbali. Magugu yaliwafanya vibarua wa shambani wawe na kazi nyingi ya kuyaondoa. Lakini wengi wao walipoteza kazi zao baada ya wanasayansi kugundua dawa za kuua magugu. Wadudu, minyoo, na fukusi wamekuwa maadui wa mkulima tangu jadi. Hata hivyo, sasa wakulima wanaweza kuchagua kemikali mbalimbali za kuwaua wadudu wowote waharibifu. *

Maisha ya wakulima wafugaji pia yamebadilika. Mashini za kulisha na kukamua maziwa zimewawezesha mchungaji na msaidizi wake kuchunga ng’ombe 200 hivi. Wafugaji wanaweza pia kunenepesha ndama na nguruwe haraka kuliko ilivyokuwa zamani kwa kuwafuga kwenye zizi badala ya kondeni, na hivyo wanaweza kudhibiti chakula na joto lao la mwili.

Mara nyingi matokeo ya ukulima wa kutumia mbinu za kisayansi yamekuwa yenye kustaajabisha. Wakulima fulani waliongeza mazao yao mara mia au hata elfu moja zaidi kuliko kabla ya kuanza kutumia mbinu za kisayansi. Lakini maendeleo hayo yote yameathirije maisha ya watu?

Maisha ya Mkulima Yalibadilika

Mashini zimebadili maisha ya mkulima katika sehemu nyingi. Wakulima wengi na vibarua wamelazimika kujifunza kuendesha na kudumisha mashini za hali ya juu. Na mara nyingi, wao hufanya kazi wakiwa peke yao. Sasa hawafurahii tena ushirikiano waliokuwa nao pamoja na marafiki walipokuwa wakipanda, kupalilia, na kuvuna.

Katika nchi nyingi, sasa mkulima pia ni mfanyabiashara mwenye elimu sana ambaye amebobea katika kuzalisha kwa wingi mazao machache tu au zao moja. Ametumia pesa nyingi kununua mashamba, majengo, na mashini. Hata hivyo, bado anawategemea watu wengine. Kampuni kubwa sana za kusindika vyakula na maduka makubwa huamua bei na pia aina, ukubwa, na rangi ya mazao yake. Mainjinia wa kilimo wanabuni mfumo wa kuzalisha mazao, na kampuni za pekee humtengenezea mbolea, dawa za kuua wadudu, na mbegu zinazotokeza mazao mengi ambazo atatumia katika shamba lake. Mbinu anazotumia kulima zimeboreshwa sana zinapolinganishwa na zile walizotumia mababu zake. Lakini bado anakabili hali ngumu, na watu fulani wanahofia kwamba huenda mbinu fulani za ukulima zikawa na madhara.

Wakulima Bado Wakabili Matatizo

Katika nchi zenye utajiri, bado wakulima wengi wanalazimishwa kuyaacha mashamba yao kwa kuwa hawawezi kushindana na mashirika makubwa ya kilimo. Wakulima fulani wanaweza tu kuendelea kuishi maisha ya kawaida kwa kugeuza mashamba yao kuwa mahali pa tafrija kutia ndani kujenga vyumba vya kukodi watalii au kuwa viwanja vya kupigia kambi, kucheza gofu, na kutokeza sanaa. Wengine huanza kukuza mazao ya pekee kama vile chakula kilichokuzwa kwa mbolea ya kiasili, maua, na kufuga mbuni, na alpaca.

Katika nchi maskini, ambako asilimia 80 hivi ya idadi ya watu wanapata riziki yao kwa kukuza mazao yao, wakulima wengi pia wanakumbwa na badiliko kubwa. Kampuni za kimataifa zinazotumia mbinu za kulima mashamba makubwa zinaweza kununua mashamba bora zaidi na kukuza mimea itakayouzwa katika nchi za mbali. Kwa upande ule mwingine, wakulima wadogo-wadogo hulima mashamba madogo sana au yasiyo na rutuba mara nyingi bila kutumia mashini ili waandalie familia zao chakula.

Katika nchi nyingi, kuhama kwa watu wengi sana kutoka vijijini hadi majijini ni jambo lililoanza karne nyingi zilizopita. Watu fulani hufaidika na wengine huumia wanapoacha kuishi vijijini na kuishi jijini. Ni serikali chache ambazo zimechukua hatua ya kuwasaidia watu walioathiriwa. Wanadamu wanahitaji sana Ufalme wa Mungu ambao utaleta maisha bora!—Isaya 9:6.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Amkeni! haipendekezi mbinu yoyote ya ukulima.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

MBINU MBILI ZA KILIMO

Eusebio anaishi kwenye Milima ya Andes, ambako anakuza mimea na kulisha ng’ombe 14. “Wote wana majina,” anasema. “Ninapenda kulima. Tunakuza mboga zetu wenyewe. Mimi, mke wangu, na majirani husaidiana kulima na kuvuna. Hatuna mashini zozote. Tunalima kwa plau zinazokokotwa na mafahali, na kwenye miteremko mikali tunalima kwa majembe.

“Wakati mmoja karibu mifugo yetu yote ilikufa kutokana na ugonjwa. Baada ya msiba huo, nilisomea jinsi ya kutibu wanyama wagonjwa. Hakuna mnyama ambaye amekufa tangu wakati huo, na sasa ninaweza kuwasaidia majirani kutunza mifugo yao. Tunauza jibini sokoni, lakini tunapata pesa kidogo sana. Siku zote sisi huwa na chakula cha kuwalisha watoto wetu sita.”

Richard analima shamba lenye ukubwa wa ekari 1,300 hivi huko Kanada. Anafanya kazi peke yake ingawa ana kibarua mmoja ambaye humsaidia katika majira ya kupanda na kuvuna.

“Siku hizi, mkazo wa kilimo unaathiri mtu kiakili kuliko kimwili,” anasema Richard. “Trekta yangu na mashini ya kuvuna ina mfumo wa kupunguza joto ambao hunilinda kutokana na vumbi na wadudu. Nina mashini zenye upana wa mita 9, kwa hiyo ninaweza kupanda au kuvuna upana wa ekari 160 hivi kwa siku moja. Lakini ninategemea sana mashini hizo, na jambo hilo ndilo husababisha mkazo. Mara kwa mara ninalazimika kukopa pesa ili kununua mashini nyingine. Kulipa mkopo huo kunategemea mambo ambayo siwezi kuyadhibiti kama vile, mvua, baridi kali, bei ya bidhaa sokoni, na riba ambayo benki itanitoza. Mkazo unaotokezwa na ukulima umesababisha matatizo mengi katika ndoa katika eneo hili, na hata kujiua.”

[Picha katika ukurasa wa 21]

Mashini ya kuvuna iliyovumbuliwa na “McCormick” mnamo 1831, iliwasaidia wakulima kuvuna nafaka mara tano zaidi ya walivyofanya awali

[Hisani]

Wisconsin Historical Society, WHi-24854