Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mti Wenye Matumizi Mengi

Mti Wenye Matumizi Mengi

Mti Wenye Matumizi Mengi

▪ Wanapotembelea sehemu za mashambani za Urusi majira ya kupukutika kwa majani yanapoanza, huenda wageni wakaona kichaka au mti unaoitwa sea buckthorn, * uliojaa matunda madogo kama shanga yenye rangi ya chungwa. Badala ya kukua yakiwa mafungu-mafungu, matunda hao hukua kwenye mti na matawi yake na kufanya mti huo uwe na rangi yenye kupendeza.

Matunda yake yanaweza kuliwa, lakini jihadhari usichomwe na miiba unapoyachuma! Lazima uchume tunda mojamoja na uwe mwangalifu usiyaponde. Kwa kuwa mti huo hukua vizuri kwenye maeneo yenye baridi, mara nyingi unapatikana kwenye maeneo ya milimani ya kaskazini-magharibi mwa Ulaya hadi Milima ya Altai huko Asia ya Kati, na pia China magharibi na kaskazini na Himalaya ya kaskazini. Kwa karne kadhaa, matunda ya mti huo yalipendwa sana huko China, Urusi, na Tibet.

Mti huo unatajwa katika vitabu vya kitiba vya Tibet na Ugiriki ya kale. Jina lake la Kigiriki, Hippophaë, linamaanisha “farasi anayeng’aa.” Inadhaniwa kwamba jina hilo linarejelea zoea la kale la Wagiriki la kutumia beri hizo au majani yake kwa njia fulani ili kuwafanya farasi wa mashindano wawe na ngozi inayong’aa.

Mti huo uliletwa Amerika Kaskazini na wahamiaji Warusi mwanzoni mwa karne ya 20 wakati vichaka kutoka Siberia vililetwa Kanada na Marekani ili matunda hayo yakuzwe kwa ajili ya biashara. Sasa nchi nyingi hukuza mti huo kwa ajili ya chakula na dawa.

Kati ya mambo mengine, beri hizo zina vitamini C na E, aina fulani ya vitamini B, asidi zenye mafuta, karotini, na kemikali zinazozuia kuharibika kwa chembe mwilini. Utafiti wa kitiba wa hivi karibuni umechunguza madai ya kwamba mti huo unaweza kutibu kansa, kupunguza hatari za magonjwa ya moyo na kutibu vidonda vya tumbo, matatizo ya ngozi, na magonjwa ya ini. Beri hizo pia hutengeneza kinywaji chenye kuburudisha chenye ladha ya limau na pia hutumiwa kutibu magonjwa mbalimbali.

Sehemu muhimu sana ya beri ya mti huo ni mbegu yake ndogo nyeusi. Mafuta yanayopatikana katika mbegu hiyo huwa na virutubisho vingi vya beri. Utafiti fulani unasema kwamba mafuta hayo husaidia kuimarisha mfumo wa kinga. Kwa kuongezea, mafuta hayo hutumiwa katika vipodozi na mafuta ya ngozi kwa sababu yana uwezo wa kufanya ngozi iwe kama ya kijana.

Ukitembelea Urusi, huenda ukaona na kuvutiwa na beri zenye rangi ya chungwa za mti wa sea buckthorn. Hata hivyo, mti huo hauvutii kwa sababu tu ya uzuri wake. Kwa kweli, ni mojawapo wa uumbaji unaoonyesha hekima na wema wa Muumba wetu!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Huenda mti huo umepewa jina hilo kwa sababu unakua katika fuo huko Ulaya na Asia.