Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nguzo Juu ya Bahari

Nguzo Juu ya Bahari

Nguzo Juu ya Bahari

▪ Je, umewahi kuona upepo wa kisulisuli juu ya bahari? Desemba 25, 2005, kulitokea kisulisuli kama hicho kwenye pwani ya Tahiti. Upepo huo mkali wa kisulisuli uliokuwa umebeba maji mengi na kusimama wima kwa dakika 30 hivi kati ya bahari na anga. Kisha kisulisuli hicho kikawa cheupe na kupotea.

Nyakati nyingine visulisuli vya aina hiyo vinasemwa kuwa vimbunga, lakini havina nguvu kama vimbunga. Kwa kawaida, visulisuli hivyo huendelea kwa dakika kumi hivi, ingawa kuna wakati ambapo vimeendelea kwa saa zima. Kwa kuwa visulisuli hivyo hutokea juu ya bahari, vinaweza kuonekana tu kwa sadfa. Hilo hufanya iwe vigumu kwa wataalamu wa hali ya hewa kuelewa visulisuli hivyo. Ripoti zinasema kwamba visulisuli hivyo vinaweza kupiga kelele kama ile inayotolewa na gari-moshi la kubeba mizigo.

Akieleza kuhusu hisia zake zilizokuwa zikimhangaisha, mtunga-zaburi mmoja wa Biblia wa nyakati za kale aliandika hivi: “Kilindi kinaita kilindi kwa sauti ya nguzo zako za maji.” (Zaburi 42:7, Zaire Swahili Bible) Ingawa hatuwezi kusema ni nguzo ya aina gani mtunga-zaburi huyo wa Biblia alikuwa akizungumzia, huenda alikuwa akilinganisha hisia zake na visulisuli hivyo. Alisema kwamba nafsi yake ilikuwa ‘imekata tamaa’ na ndani yake kulikuwa ‘na msukosuko.’ Lakini alipata faraja kutoka kwa Mungu wake. “Mngojee Mungu,” akaiambia nafsi yake, “kwa maana bado nitamsifu kuwa ndiye wokovu wangu mkuu na kuwa ndiye Mungu wangu.”—Zaburi 42:11.

Kama tu mtunga-zaburi huyo, tunaweza pia kupatwa na matatizo yaliyo kama kisulisuli juu ya bahari. Lakini tukimngojea Mungu, atathibitika kuwa wokovu wetu mkuu.