Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

▪ “Karibu asilimia 33 ya wasichana nchini Marekani wanashika mimba kabla ya kufikia umri wa miaka 20.”—KITUO CHA KUDHIBITI MAGONJWA YA KUAMBUKIZA, MAREKANI.

▪ Uchunguzi wa “kutendewa kwa jeuri nyumbani” uliofanyiwa wanaume 420 nchini Marekani ulionyesha kwamba “karibu [wanaume] watatu kati ya 10 wamepigwa au kutendewa vibaya kwa njia nyingine.”—AMERICAN JOURNAL OF PREVENTIVE MEDICINE.

Watoto Wajifunze Lugha Nyingi?

Wazazi wengi wanahofia kwamba ikiwa mtoto atajua lugha ya pili itamfanya ashindwe kuzungumza lugha yake ya asili. Hata hivyo, utafiti uliofanywa na kikundi kilichoongozwa na mwanasayansi wa mfumo wa neva Laura-Ann Petitto huko Toronto, Kanada, unaonyesha kwamba “sehemu fulani za neva ambazo wewe huzaliwa nazo . . . huwa tayari kwa ajili ya kujifunza lugha,” Petitto anasema, “na inaweza kushughulikia lugha nyingi.” Mara nyingi watoto wanaoweza kuzungumza lugha mbili hufanya vizuri zaidi shuleni kuliko wale wanaojua lugha moja tu. Hata hivyo, gazeti Toronto Star, linasema kwamba “wazazi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuwafundisha watoto wao lugha ya pili ikiwa wanataka watoto wao wapate manufaa ya kuzungumza lugha mbili.”

Watoto Husumbuliwa na Ponografia

Watoto hukabiliana na picha chafu za ngono zenye kudhuru na video zenye jeuri kwenye Intaneti wakiwa na umri mdogo sana. Kulingana na Heinz-Peter Meidinger, mwenyekiti wa Taasisi ya Ujerumani ya Kusitawi kwa Lugha, wavulana wenye umri wa kuanzia miaka 12 na kuendelea wanajua jinsi na wapi wanapoweza kupata tovuti zinazoonyesha jeuri kupita kiasi au picha chafu za ngono. Kwa nje huenda watoto wakaonekana kuwa hawajali na hawajaathirika, lakini kwa ndani wengi husumbuliwa wanapoziangalia. Meidinger anawahimiza wazazi wachunguze watoto wao wanafikiri kuhusu nini na kompyuta zao zina mambo gani.

Kupanga kwa Ajili ya Talaka

Waaustralia wengi zaidi wanafanya mikataba kabla ya kuoana wakitaka wenzi wao waishi kwa njia fulani hususa, linaripoti gazeti la Sydney la Sunday Telegraph. Mikataba hiyo inaonyesha jinsi wenzi wa ndoa watakavyogawana mali zao wanapotalikiana. Mikataba mingi sasa inataja waziwazi maisha ambayo kila mwenzi anapaswa kudumisha ili ndoa iendelee. Mikataba hiyo inaweza kuonyesha ni nani atakayepika, kufanya usafi, au kuendesha gari, kutia ndani ikiwa watakuwa na wanyama vipenzi, uzito ambao kila mwenzi anapaswa kudumisha, ni nani atakayemtembeza mbwa, na ni nani atakayekuwa na kazi ya kutupa takataka. Wakili Christine Jeffress anasema kwamba watu “hawatarajii kwamba uhusiano wao utaendelea milele.”

Wazazi Wanang’ang’ana Kuonyesha Upendo

“Idadi inayozidi kuongezeka ya wazazi wanahitaji kitabu kinachotoa mwongozo wa jinsi ya kuwatendea watoto wao wadogo, kwa kuwa inaonekana hawana uwezo wa kuwaonyesha upendo wa asili,” linasema gazeti la Poland Newsweek Polska. Wazazi wanahitaji kufundishwa mambo ya msingi, kama vile kuwakumbatia watoto wao, kucheza nao, na kuwaimbia. Mambo hayo ni muhimu ili watoto wakue vizuri. Hata hivyo, utafiti unaonyesha kwamba “familia nchini Poland zinaona kwamba kutazama televisheni na kwenda kununua vitu ndiyo pindi ambazo wazazi hutumia kuwa pamoja na watoto wao.” Kucheza nao kulikuwa namba sita katika orodha.