Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jihadhari na Sumu ya Madini ya Risasi!

Jihadhari na Sumu ya Madini ya Risasi!

Jihadhari na Sumu ya Madini ya Risasi!

Katika miaka ya hivi karibuni serikali mbalimbali zimetoa mwito wa dharura kwamba vitu vya watoto vya kuchezea na vito fulani viondolewe madukani. Kwa sababu gani? Baadhi ya vitu hivyo vimepatikana vikiwa na viwango vya juu sana vya madini ya risasi, na watoto wachanga hupenda kuvimumunya na kuvitafuna. Sumu ya madini ya risasi inaweza kuwa hatari hasa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka sita kwa sababu bado mfumo wao mkuu wa neva haujakomaa.

UCHUNGUZI uliofanywa na Chuo cha Afya ya Umma cha Johns Hopkins Bloomberg, ulisema kwamba madini ya risasi huzuia protini ambayo ni muhimu kwa ukuzi wa ubongo na uwezo wa kutambua mambo isiingie mwilini. Uchunguzi umeonyesha kwamba asilimia 50 ya madini hayo ya risasi ambayo watoto humeza huingia kwenye damu, ilhali katika watu wazima, ni asilimia 10 hadi 15 tu inayoingia kwenye damu.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kwamba hata kiwango kilicho chini ya kiwango kilichowekwa na serikali cha madini hayo kinaweza kudhuru afya. Shirika la Usalama wa Kitaifa la Marekani linasema kwamba madhara hayo kwa watoto yanatia ndani “matatizo ya kujifunza, ya kukaza fikira, tabia zisizo za kawaida, kutoweza kukua [kwa kiwango cha kawaida], matatizo ya kusikia, na matatizo ya figo.” Wanawake waja-wazito wanapaswa kuwa waangalifu sana na kuepuka madini hayo kwa kuwa yanaweza kumdhuru mtoto aliye tumboni. *

Sumu ya madini ya risasi pia huingia kwenye vyakula na vinywaji vilivyowekwa katika vyombo vya udongo vilivyopakwa rangi na kuchomwa ambavyo hutumiwa katika sehemu fulani za Asia na Amerika ya Latini. Nyakati nyingine, maji ya kunywa huwekwa katika vyombo vya udongo ili yawe baridi, na vinywaji moto huwekwa kwenye vikombe vilivyopakwa rangi na kuchomwa. Uchunguzi uliofanyiwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano huko Mexico City ulionyesha kwamba karibu nusu ya watoto walio na umri wa miezi 18 na kuendelea walikuwa na viwango vya juu vya madini ya risasi katika damu yao. Ilisemekana kwamba hilo lilisababishwa na vyakula vilivyopikwa katika vyombo vya udongo vilivyopakwa rangi na kuchomwa. Madini ya risasi hupakwa kwenye vyombo vya udongo ili viwe laini na kung’aa, lakini madini hayo yanaweza kuvuja hasa ikiwa chombo hicho kitapashwa moto au matunda na mboga fulani zitatiwa ndani ya chombo kama hicho.

Vyanzo Vingine vya Sumu ya Madini ya Risasi

Ingawa katika miaka ya hivi karibuni nchi nyingi zilizoendelea zimeacha kutumia mafuta yenye risasi, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linasema kwamba karibu nchi 100 ulimwenguni bado zinatumia mafuta yenye madini ya risasi. Risasi haiwezi kuvunjwavunjwa au kuchomeka. Hivyo, visehemu vya risasi vinavyotolewa kwenye magari huchafua udongo barabarani. Kwa sababu hiyo, watu hupumua vumbi lenye risasi au kulibeba hadi nyumbani.

Kisababishi kingine kikubwa cha sumu ya risasi ni rangi yenye risasi iliyotumiwa kupaka nyumba kabla ya sheria kuwekwa ili kudhibiti matumizi yake. Nchini Marekani peke yake, inakadiriwa kwamba nyumba milioni 38, yaani, asilimia 40 ya nyumba zote, zimepakwa rangi yenye risasi. Nyumba inapofanyiwa marekebisho rangi hubambuka na vumbi la risasi hutokea na linaweza kuwa hatari.

Majiji na nyumba nyingi za zamani hupata maji kupitia mabomba yaliyotengenezwa kwa madini ya risasi au mabomba ya shaba yaliyounganishwa kwa risasi. Kliniki ya Mayo, kituo cha kitiba chenye kuheshimika nchini Marekani, kinapendekeza kwamba mtu aache maji baridi yatiririke kutoka kwenye mabomba kama hayo kwa sekunde 30 hadi 60 kabla ya kuyanywa. Maji moto kutoka kwenye mabomba kama hayo hayapaswi kunywewa au kupikiwa—na hasa hayapaswi kutumiwa kutayarisha chakula cha watoto.

Kiwango cha risasi katika damu hupungua sana wakati chanzo cha risasi hiyo kinapoondolewa. Watu walio na wasiwasi kwamba wana madini ya risasi katika damu yao wanaweza kupimwa. Mtu anapogundua kwamba ana kiwango kinachoweza kusababisha madhara anapaswa kutibiwa.

Uhitaji wa Kuwaelimisha Watu

Madini ya risasi yanaweza kumdhuru mtu ikiwa yatarundamana mwilini kwa muda mrefu. Lakini hata mtu akimeza madini hayo mara moja tu, anaweza kufa. Kituo cha Marekani cha Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza kinaripoti kwamba mnamo 2006, mtoto mwenye umri wa miaka minne alikufa alipomeza kito fulani kilichokuwa na viwango vya juu vya madini ya risasi.

Ikikazia uhitaji wa kuwaelimisha watu, ensaiklopidia moja ya kitiba inasema kwamba, sasa, mtoto 1 kati ya 20 nchini Marekani ambaye hajaingia shuleni ana kiwango cha juu sana cha madini ya risasi ndani ya damu. Ikiwa hali iko hivyo katika nchi ambazo matumizi ya madini hayo yanadhibitiwa, vipi katika nchi ambako hakuna sheria za kudhibiti matumizi yake? Kwa kweli, kila mtu anapaswa kujihadhari!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Watu wazima wanaweza pia kuathiriwa na madini hayo na kuwa na matatizo ya neva, maumivu ya misuli na vifundo, au kusahau-sahau na kushindwa kukaza fikira.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 29]

DALILI FULANI ZINAZOONYESHA MTOTO ANA SUMU YA RISASI

Maumivu ya tumbo, kuwa mkali, upungufu wa damu, kutoweza kuwa makini, kufunga choo, uchovu, maumivu ya kichwa, kukasirika upesi, ukosefu wa ustadi mbalimbali, ukosefu wa hamu ya kula, kukosa nguvu, kukua polepole.—MEDLINE PLUS MEDICAL ENCYCLOPEDIA.