Mfupa—Una Ugumu Usio na Kifani
Je, Ni Kazi ya Ubuni?
Mfupa—Una Ugumu Usio na Kifani
● Imesemekana kwamba mfupa umebuniwa ukiwa na ugumu wenye uwezo wa kupanuka, kukua, na kustahimili kukandamizwa. Kwa nini isemwe hivyo?
Fikiria hili: Inakadiriwa kwamba mwanadamu ana mifupa 206 na maungio 68. Mfupa mrefu zaidi ni mfupa wa paja; mdogo zaidi ni ule unaoitwa stapi, mfupa ulio ndani ya sikio. Unapomtazama mwanasarakasi stadi, unaona wazi kwamba mifupa, misuli, gegedu, na maungio yanaweza kumfanya mtu awe na uwezo mkubwa wa kunyumbulika na kusonga. “Kidole gumba peke yake kinatosha kumsadikisha mtu yeyote kwamba yule aliyebuni mwili wetu (haidhuru unaamini huyo ni nani) alikuwa na akili nyingi ajabu!” inasema Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Matibabu Yanayohusiana na Anga za Juu.
Pia mifupa inaweza kustahimili kishindo. “Imeundwa kwa njia ileile ambayo zege lililokorogewa juu ya vyuma huundwa,” inasema taasisi hiyo. “Chuma kilichokorogewa zege hufanya ukuta uwe na nguvu za kustahimili kuvutwa, kisha saruji, mchanga, na kokoto hufanya zege liwe na uwezo wa kustahimili kukandamizwa. Hata hivyo, mfupa unaweza kustahimili kukandamizwa zaidi kuliko zege lililokorogwa kwa njia bora zaidi.” “Tunatamani tu tungeweza kuiga ugumu wake,” akasema Robert O. Ritchie, profesa wa sayansi ya vifaa katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley, huko Marekani.
Tofauti na zege, mfupa ni sehemu muhimu ya viumbe vingi sana. Una uhai. Unaweza kujirekebisha, kutenda kulingana na jinsi homoni zinazoathiri ukuzi wake zinavyotaka, na hata kutimiza sehemu muhimu katika kutokezwa kwa chembe nyekundu za damu. Pia, kama tu misuli, mfupa huzidi kuwa na nguvu kadiri unavyobeba vitu vizito. Kwa sababu hiyo, wanariadha wana mifupa mizito kuliko watu ambao hawafanyi mazoezi.
Una maoni gani? Je, mfupa ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?
[Picha katika ukurasa wa 25]
Muundo wa mfupa (umeongezwa ukubwa)
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Leg bone: © MedicalRF.com/age fotostock; close-up: © Alfred Pasieka/Photo Researchers, Inc.; gymnast: Cultura RF/Punchstock