Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ndege Yenye Injini

Ndege Yenye Injini

Ndege Yenye Injini

KWA karne nyingi wanadamu wamekuwa na ndoto ya kupaa angani. Lakini misuli ya mwanadamu haina nguvu za kumwezesha kupaa angani. Katika mwaka wa 1781, James Watt alivumbua injini inayotumia mvuke na inayoweza kuzungusha mtaimbo, na katika mwaka wa 1876, Nikolaus Otto aliendeleza wazo hilo kwa kutokeza injini inayotumia mafuta. Sasa wanadamu walikuwa na injini inayoweza kufanya mashini ipae angani. Lakini ni nani ambaye angeweza kujenga mashini kama hiyo?

Ndugu wawili, Wilbur na Orville Wright, walitamani sana kupaa tangu walipojifunza kurusha tiara walipokuwa wavulana wadogo. Baadaye walijifunza uinjinia kwa kutengeneza baiskeli. Ndugu hao walitambua kwamba changamoto kubwa ni kutengeneza ndege inayoweza kuongozwa na rubani. Ndege ambayo haiwezi kuongozwa hewani ni kama baiskeli ambayo haiwezi kuelekezwa. Wilbur alipowatazama hua wakipaa, alitambua walikuwa wakiinama upande mmoja ili wageuke na kwenda upande mwingine kama mwendesha baiskeli anavyofanya. Alifikia mkataa wa kwamba ndege hugeuka na kujisawazisha kwa kupinda ncha za mabawa yao. Hivyo ndivyo alivyopata wazo la kujenga bawa linaloweza kujipinda.

Mwaka wa 1900, Wilbur na Orville walifaulu kutengeneza ndege yenye mabawa yanayoweza kujipinda. Kwanza waliirusha kama tiara na baadaye wakaiongoza kama ndege isiyo na injini. Waligundua kwamba inahitaji kuwa na uwezo wa kufanya mambo matatu ya msingi: Uwezo wa kuinua na kuinamisha pua, kuinua na kuinamisha bawa moja juu ya lingine, kugeuza pua kuelekea kulia au kushoto. Hata hivyo, walisikitika kwamba mabawa hayo hayakuwa na uwezo wa kuinua ndege juu zaidi, kwa hiyo walitengeneza bomba kubwa sana linalopuliziwa upepo ambamo walijaribu mamia ya mabawa yenye maumbo tofauti-tofauti hadi walipopata bawa lenye umbo, ukubwa, na pembe inayofaa zaidi. Katika mwaka wa 1902, walifaulu kuongoza ndege yao mpya angani bila kutatizwa na upepo. Je, sasa wangeweza kutumia injini kwenye ndege hiyo?

Kwanza walihitaji kutengeneza injini yao. Wakiwa na ujuzi walioupata walipokuwa wakijaribu mabawa, walifaulu kutatua tatizo kubwa la kutengeneza propela. Mwishowe, Desemba 17, 1903 (17/12/1903), waliwasha injini hiyo, propela zikaanza kuzunguka na kuvuma, na ndege ikapaa angani. Orville alisema hivi: “Tulikuwa tumetimiza tamaa tuliyokuwa nayo toka utotoni. Tulikuwa tumejifunza kupaa angani.” Ndugu hao wawili wakawa mashuhuri ulimwenguni pote. Lakini je, walitimiza mambo hayo yote kwa uwezo wao wenyewe? La, walisaidiwa sana na vitu vya asili.

[Picha katika ukurasa wa 4]

Ndege inayoitwa “Flyer,” huko North Carolina, Marekani, iliyotengenezwa na Wilbur na Orville Wright mnamo 1903 (picha ya kuigiza)