Ni Nani Aliyebuni Kwanza?
Ni Nani Aliyebuni Kwanza?
MNAMO 1973, Dakt. Martin Cooper ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kuonyesha jinsi ambavyo simu ya mkononi hutumiwa. Ilikuwa na betri, redio, na kompyuta ndogo. Wakazi wa jiji la New York waliduwaa walipomwona Cooper akipiga simu barabarani. Lakini jambo hilo liliwezekana tu kwa kuwa Alessandro Volta alikuwa amevumbua betri inayohifadhi umeme katika mwaka wa 1800. Isitoshe, simu ilikuwa imetokezwa kufikia mwaka wa 1876, redio mwaka wa 1895, na kompyuta mwaka wa 1946. Mwishowe, kuvumbuliwa kwa kompyuta ndogo mnamo 1971 kuliwezesha simu ya mkononi ibuniwe. Hata hivyo, je, ni jambo jipya kabisa kuwasiliana kwa kutumia vifaa vya hali ya juu?
Kifaa cha mawasiliano ambacho mara nyingi hupuuzwa ni sauti ya mwanadamu. Zaidi ya nusu ya mabilioni ya chembe za neva zilizo katika sehemu ya ubongo inayoongoza misuli zinahusika katika kudhibiti viungo vyako vya usemi, na misuli 100 hivi hutendesha sehemu tata za ulimi, mdomo, taya, koo, na kifua.
Pia sikio lako ni sehemu ya mfumo huo wa kuwasiliana. Sikio hubadili sauti kuwa mawimbi ambayo ubongo wako unaweza kuchanganua. Ubongo wako huchanganua sauti hivi kwamba unaweza kutambua watu kwa kutegemea sauti yao. Pia ubongo hupima upesi sana sauti inayoingia kupitia sikio moja muda mrefu sana kabla ya sikio lile lingine na hivyo kutambua kwa njia hususa kabisa sauti imetokea upande gani. Hayo ni mambo mawili tu yanayokuwezesha kumsikiliza mtu mmoja hata ingawa huenda watu wengine wakawa wanazungumza.
Kwa hiyo, vifaa vya mawasiliano vya hali ya juu visivyounganishwa kwa waya (vilivyo na uwezo wa kutambua unayewasiliana naye) si vipya. Tekinolojia hiyo ilikuwapo kwanza katika vitu vya asili.
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 3]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
1800
Betri inayohifadhi umeme
1876
Simu
1971
Kompyuta ndogo
1973
Dakt. Martin Cooper alivumbua simu ya mkononi
[Hisani]
Dr. Cooper and mobile phone: © Mark Berry
[Picha katika ukurasa wa 2]
Upande wa kulia wa ukurasa wa 2, mbele kwenda nyuma, picha zilizoigizwa: Guglielmo Marconi akiwa na vifaa vya redio yake; Thomas Edison akiwa na balbu; Granville T. Woods, mvumbuzi wa vifaa vya mawasiliano; Wilbur na Orville Wright wakiwa na ndege ya mwaka wa 1903 inayoitwa Flyer