Visiwa vya Faeroe—Vimeunganishwa kwa Njia ya Pekee
Visiwa vya Faeroe—Vimeunganishwa kwa Njia ya Pekee
VISIWA vya Faeroe, ambavyo ni visiwa vidogo 18 vilivyo karibu-karibu kwenye Bahari iliyochafuka ya Atlantiki Kaskazini, vinamilikiwa na watu wanaozungumza lugha yao wenyewe, yaani, Kifaeroe. Kwenye visiwa hivyo maridadi, kuna milima yenye ncha kali ambayo inateremka moja kwa moja baharini. Karibu na bahari, nyumba katika vijiji zimepakwa rangi nyingi. Wakati wa kiangazi, milima hiyo hung’aa kwa rangi maridadi ya kijani.
Ingawa wakazi 48,000 wa visiwa hivyo hushirikiana kama jamii, si rahisi kufanya hivyo sikuzote. Meli zinazoendeshwa kwa makasia zilitumiwa kusafirisha watu na bidhaa kutoka kisiwa kimoja hadi kingine. Watu walikuwa wakisafiri kutoka kijiji kimoja hadi kingine kwa miguu wakipanda milima mirefu na wakipita kwenye mabonde makali. Ilikuwa kazi ngumu kujenga nyumba kwani vifaa vyote vya ujenzi vilihitaji kuletwa kwa meli ya makasia. Kabla ya ujenzi kuanza, vifaa hivyo vilihitaji kubebwa hadi kijijini kutoka kwenye bandari iliyo ufuoni.
Wakazi wa Zamani
Masimulizi ya zamani zaidi kuhusu Visiwa vya Faeroe yaliandikwa na mtawa wa Ireland katika mwaka wa 825 W.K. hivi. Anasimulia kwamba kulikuwa na watawa mmojammoja kutoka Ireland kwenye visiwa hivyo zaidi ya miaka 100 kabla yake. Hata hivyo, inasemekana kwamba watu walianza kukaa katika visiwa hivyo mapema katika karne ya tisa wakati ambapo Grímur Kamban alifika kutoka Norway.
Ingawa wakazi wa mapema walijiruzuku kwa kuvua samaki, wahamiaji hawa pia walianza kufuga kondoo. Katika Kifaeroe jina Føroyar (Visiwa vya Faeroe) linamaanisha “Visiwa vya Kondoo,” na bado ufugaji wa kondoo ni muhimu. Wakazi wa huko wametumia manyoya ya kondoo kujikinga dhidi ya upepo, mvua, na baridi. Kwa kweli, wakati fulani ilisemwa kwamba ‘manyoya ndiyo dhahabu ya Visiwa vya Faeroe.’
Hata leo, kuna kondoo wengi zaidi kuliko watu katika visiwa hivyo. Kondoo huchinjwa kwa njia ya kitamaduni, kwani nyama huanikwa ili ikauke katika vibanda ambavyo upepo hupita bila kuzuiwa na kuta. Hilo hufanya nyama iwe na ladha fulani yenye kupendeza na hivyo watu wanaipenda sana.
Kama tu inavyokuwa katika maeneo ambako kuna watu wachache, wakazi wa Faeroe huhisi wakiwa na uhusiano wa karibu, jambo la kawaida kwa watu ambao wanategemeana ili kuendelea kuishi. Bado wakazi wa huko wanahisi hivyo kwa kuwa usafiri na mawasiliano ya kisasa yamefanya iwe rahisi kwa wenyeji wa visiwa hivyo kuwasiliana.
Kuunganishwa na Barabara za Chini ya Ardhi
Barabara ya kwanza ya chini ya ardhi katika Visiwa vya Faeroe ilifunguliwa katika mwaka wa 1963. Ilichimbwa chini ya mlima kwenye kisiwa cha mbali zaidi upande wa kusini, kinachoitwa Suðuroy, na inaunganisha vijiji viwili. Uchimbaji huo uliohusisha kuchimba sana na kupasua miamba, ulifanywa pande zote za mlima wakati uleule.
Barabara ya chini ya ardhi iliyochimbwa hivi karibuni zaidi inapitia mita 150 hivi chini ya bahari na kuunganisha visiwa viwili vikubwa zaidi. Ili kuichimba, kekee yenye urefu wa mita 5 ilitumiwa kuchimba miamba. Kisha baruti zilitegwa kwenye mwisho mmoja wa shimo na kuwashwa. Baada ya mlipuko, mawe na miamba iliondolewa katika sehemu hiyo yenye urefu wa mita 5. Walirudia kufanya hivyo mara nyingi hadi barabara hiyo ikawa na urefu wa kilomita 6 hivi. Ilifunguliwa Aprili 29, 2006 (29/4/2006).
Sasa Visiwa vya Faeroe vina barabara 18 za chini ya ardhi, mbili kati yake zinapitia chini ya bahari na kuunganisha visiwa. Hakuna taifa lingine lililo na kilomita nyingi zaidi za barabara za chini ya ardhi kwa kulinganishwa na idadi ya wakazi wake. Hata hivyo, bado kuna barabara nyingine za chini ya ardhi zinazopangiwa kujengwa. Bunge limeamua kujenga barabara nyingine mbili kati ya visiwa vikubwa. Moja inatarajiwa kukamilishwa mnamo 2012, na itakuwa na urefu wa kilomita 11.9, na hivyo kuifanya iwe moja kati ya barabara ndefu zaidi ya chini ya maji ulimwenguni.
Kifungo Kingine cha Pekee
Visiwa vya Faeroe vina kikundi kimoja cha watu waliounganishwa kwa njia nyingine ya pekee, yaani, muungano wenye nguvu wa kiroho uliopo kati ya Mashahidi wa Yehova. Mashahidi wa kwanza kutembelea visiwa hivyo walikuwa wanawake wawili waliojitolea kabisa ambao walifika kutoka Denmark mnamo 1935, na walitembea nyumba kwa nyumba wakiwa na ujumbe wa Biblia kuhusu Ufalme wa Mungu. Baada ya muda, wakazi fulani wa visiwa hivyo walikubali ujumbe huo wenye kutia moyo na wakashiriki katika kuuhubiri.—Mathayo 24:14.
Leo, kuna Mashahidi 100 hivi ambao hukutana katika Majumba manne ya Ufalme kwa ajili ya mikutano yao katika visiwa hivyo. Wao huhubiri kwa bidii, wakitumia barabara za juu na chini ya ardhi ambazo huunganisha visiwa hivyo maridadi katika Bahari ya Atlantiki Kaskazini iliyochafuka.
[Picha katika ukurasa wa 17]
Barabara hii ya chini ya ardhi hupitia mita 150 hivi chini ya bahari na huunganisha visiwa viwili vikubwa zaidi