Vitu vya Asili Vilitangulia vya Wanadamu
Vitu vya Asili Vilitangulia vya Wanadamu
“Tafadhali uliza . . . viumbe vya mbinguni vyenye mabawa, navyo vitakuambia. . . . Ni mkono wa Yehova ambao umefanya haya.”—Ayubu 12:7-9.
NI KANA kwamba kila sehemu ya ndege imeumbwa ili kumsaidia aruke angani. Kwa mfano, mihimili ya manyoya ya mabawa yanapaswa kubeba uzito wa ndege anapopaa. Mabawa hayo yanawezaje kuwa mepesi na wakati uleule yawe yenye nguvu sana? Ukiupasua mhimili wa manyoya, huenda ukajua sababu. Sehemu ya ndani ni kama sifongo lakini nje si laini. Mainjinia wamechunguza mihimili ya manyoya na hivyo wanatumia vyuma vilivyoundwa kwa kuiga mihimili hiyo.
Pia mifupa ya ndege imebuniwa kwa njia ya ajabu. Mifupa mingi ina shimo kama mrija ndani na nyingine huwa imetegemezwa kwa vitu vigumu vinavyoweza kunyumbulika. Kwa kupendeza, mbinu hiyo ilitumiwa kutengeneza mabawa ya chombo cha kusafiria angani.
Marubani husawazisha ndege za kisasa kwa kuinua au kuinamisha baadhi ya miisho ya mabawa na mkia wa ndege. Lakini ndege hutumia misuli 48 hivi iliyo katika mabawa na mabega yake kupanua, kufunga, na kupiga mabawa yake, mara kadhaa kwa sekunde. Si ajabu kwamba wataalamu wanatamani kubuni eropleni yenye uwezo wa kuchezacheza angani kama ndege wanavyofanya!
Ndege hutumia nishati nyingi sana kupaa angani, hasa wakati wa kuinuka. Kwa hiyo, ndege wanahitaji “injini” yenye nguvu na uwezo wa kutokeza nishati upesi. Moyo wa ndege hupigapiga haraka na kwa kawaida ni mkubwa zaidi na wenye nguvu zaidi kuliko wa mnyama aliye na ukubwa kama wake. Pia, mapafu ya ndege yamebuniwa kwa njia tofauti kwa kuwa yana njia moja tu ya kuingiza na kutoa hewa ambayo ni bora zaidi kuliko ya wanyama.
Ndege wengi wana uwezo wa kuruka kwa muda mrefu kwa sababu wana nishati ya kutosha. Ndege anayeitwa kurumbizi anaweza kupoteza karibu nusu ya uzito wa mwili wake anaposafiri kwa saa kumi. Lakini aina fulani ya chamchanga wanaporuka kutoka Alaska hadi New Zealand, zaidi ya nusu ya uzito wa mwili wao ni mafuta. Kwa kushangaza, hilo humwezesha ndege huyo kupaa kwa saa 190 (siku nane) bila kutua. Hakuna eropleni inayoweza kufanya hivyo.