Vitu vya Asili Vilitangulia vya Wanadamu
Vitu vya Asili Vilitangulia vya Wanadamu
“Sikio lenye kusikia na jicho lenye kuona—Yehova ndiye aliyevifanya vyote viwili.”—Methali 20:12.
MACHO yako ni kama kamera ndogo za televisheni. Yanabadili picha kuwa mawimbi na kuyatuma kupitia neva ya jicho hadi nyuma ya ubongo wako ambako mawimbi hayo hubadilika tena kuwa picha halisi.
Jicho ni lenye kustaajabisha na limeundwa kwa akili nyingi sana hata ingawa ni dogo sana. Lina kipenyo cha milimita 24 na uzito wa gramu 7.5. Kwa mfano, jicho lina mifumo tofauti ya kuliwezesha kuona mahali palipo na mwangaza mdogo na mwangaza mwingi hivi kwamba dakika 30 baada ya kuingia katika chumba kilicho na giza, macho yako yanaanza kuathiriwa na nuru mara 10,000 zaidi ya kawaida.
Unapokuwa mahali penye mwangaza wa kawaida, ni nini kinachokusaidia kuona vizuri? Jicho lako lina chembe zenye uwezo wa hali ya juu wa kutambua mwangaza mara 100 kuliko uwezo wa kamera nyingi za video. Pia, nyingi ya chembe hizo zimehifadhiwa katika sehemu ndogo katikati ya retina inayoitwa fovea, ambayo ndiyo sehemu inayoona vizuri zaidi. Kwa kuwa unatazama mahali mbalimbali mara kadhaa kwa sekunde, unaweza kuona kila kitu vizuri. Kwa kushangaza, fovea ya jicho lako ina ukubwa unaokaribia kulingana na kituo kilicho mwishoni mwa sentensi hii.
Mawimbi kutoka kwenye chembe zenye uwezo wa hali ya juu wa kutambua mwangaza hupita kutoka kwenye chembe moja ya neva hadi kwenye neva ya jicho. Lakini chembe hizo hazipitishi tu mawimbi hayo. Zinachanganua habari hiyo, kuboresha habari muhimu na kuchuja habari isiyohitajika.
Sehemu ya ubongo ambayo hupokea habari kutoka kwa jicho ili tuweze kuona, hufanya kazi kama kipokezi cha video cha hali ya juu. Inaboresha picha kwa kuzifanya sehemu zote zionekane vizuri na kulinganisha mawimbi kutoka kwa chembe ambazo hutambua zile rangi za msingi, hivyo unaweza kutofautisha mamilioni ya rangi. Ubongo wako pia hulinganisha tofauti ndogo sana ambazo macho yako mawili yanaona ili uweze kutambua umbali kati ya vitu.
Fikiria jinsi macho yako yanavyotazama nyuso katika umati wa watu walio mbali na kutuma habari kwenye ubongo wako ambao hubadili habari hiyo kuwa picha. Pia, fikiria jinsi habari hususa kuhusu nyuso hizo inavyolinganishwa na habari zilizo katika kumbukumbu yako hivi kwamba unaweza kumtambua rafiki yako mara moja. Je, hilo si jambo lenye kustaajabisha?
[Picha katika ukurasa wa 7]
Njia ambayo jicho huchanganua habari inaonyesha kwamba akili nyingi ilitumika kulibuni