Vitu vya Asili Vilitangulia vya Wanadamu
Vitu vya Asili Vilitangulia vya Wanadamu
“Hata korongo juu mbinguni—anajua vema nyakati zake zilizowekwa.”—Yeremia 8:7.
MIAKA 2,500 hivi iliyopita, Yeremia aliandika kuhusu korongo anayehama-hama. Leo, bado watu wanastaajabia viumbe ambao huhamahama, kama vile samoni wanaoweza kuogelea maelfu ya kilomita baharini na kurudi kwenye mto ambako walizaliwa, na kasa aliye na ngozi laini mgongoni ambaye anaweza kusafiri mbali sana pia. Kasa mmoja ambaye alitaga mayai yake huko Indonesia alifuatwa aliposafiri kilomita 20,000 hadi ufuo wa Oregon nchini Marekani. Mara nyingi, kasa hao hurudi kwenye eneo hilohilo la Indonesia kutaga mayai yao.
Viumbe wengine wanaweza kujua mahali makao yao yalipo kwa usahihi, jambo ambalo ni lenye kustaajabisha sana kuliko tu kusafiri kutoka mahali pamoja hadi pengine kisilika. Kwa mfano, wachunguzi walibeba albatrosi 18 kwa ndege kutoka kwenye kisiwa kidogo katikati ya Bahari ya Pasifiki na kuwapeleka kwenye maeneo kadhaa maelfu ya kilomita kutoka huko halafu wakawaachilia. Wengine waliachiliwa karibu na ukingo wa magharibi wa bahari hiyo na wengine karibu na ukingo wa mashariki. Baada ya majuma machache, ndege wengi walikuwa wamerudi nyumbani.
Hua wamesafirishwa zaidi ya kilomita 150 hadi mahali ambako hawajui wakiwa wamedungwa sindano ya kuwafanya walale au wakiwa ndani ya mapipa yanayozunguka, lakini baada ya kuzunguka mara kadhaa, walitambua mahali walipo na wakageuka na kurudi nyumbani moja kwa moja. Kwa kuwa hua wanaweza kutambua jinsi ya kufika nyumbani hata wakiwa wamevishwa vioo vinavyowazuia kuona, watafiti wanaamini kwamba wao hukadiria mahali walipo na wanapoelekea kwa kutambua uvutano fulani unaowaongoza wanakoelekea.
Vipepeo wanaoitwa monarch kutoka maeneo mbalimbali ya Amerika Kaskazini husafiri kwa maelfu ya kilomita hadi sehemu ndogo ya Mexico. Hata ingawa hawajawahi kwenda Mexico tena, wao hutambua wanakoelekea, na mara nyingi wao hutua kwenye miti ambayo mababu zao walitua mwaka uliotangulia. Jambo hilo bado linawashangaza watafiti.
Tofauti na vifaa vya kutuongoza vinavyotegemea hasa habari kutoka kwa setilaiti, wanyama wengi hutumia njia mbalimbali za kutambua mahali walipo na wanapoelekea—iwe ni kutazama alama za dunia, jua, kutambua nguvu za sumaku za dunia, kunusa harufu fulani za pekee, na hata sauti. Profesa wa biolojia James L. Gould anaandika hivi: “Wanyama ambao maisha yao hutegemea kufuata ramani sahihi wamebuniwa kwa ustadi sana. . . . Wamebuniwa wakiwa na mbinu nyingine za kutumia ili kutambua walipo na wanapoelekea ikitegemea ni mbinu gani inayotoa habari zenye kutegemeka zaidi.” Bado watafiti wanashangazwa na utata wa ramani zinazowaongoza wanyama.