Mont Blanc—Sehemu Iliyo Juu Zaidi Ulaya
Mont Blanc—Sehemu Iliyo Juu Zaidi Ulaya
TANGU utotoni, Horace-Bénédict de Saussure (1740-1799), Mswisi aliyekuwa mtaalamu wa vitu vya asili alivutiwa sana na mlima unaoitwa Mont Blanc, jitu la Milima ya Alps. Kwa kuwa aliona ni vigumu sana kupanda mlima huo, aliahidi kumtuza mtu wa kwanza kufikia kilele chake cha juu zaidi kilicho na kimo cha mita 4,807. Jitihada za mapema zaidi za kufikia kilele hicho zilifanywa mnamo 1741. Lakini Agosti 1786 ndipo wakazi wawili wa Chamonix, Ufaransa—Jacques Balmat, mchimbaji wa fuwele, na Michel-Gabriel Paccard, aliyekuwa daktari—walipanda hadi kilele cha juu zaidi cha safu za milima inayofanyiza Mont Blanc. Mwaka uliofuata, Saussure alifika kwenye kilele hicho cha juu zaidi Ulaya alipokuwa akifanya uchunguzi wa kisayansi, na mnamo 1788 alipanda juu ya kilele kinachoitwa Col du Géant, naye akakaa huko kwa siku 17. Hao ndio watu wa kwanza kushindana kupanda mlima.
Mnamo 1855 kikundi fulani kilichoongozwa na Waitaliano kilipanda mlima huo kupitia upande mwingine wa Mont Blanc, sehemu iliyokuwa ngumu kuliko ile ya kwanza. Miaka tisa baadaye, kilele hicho kilifikiwa kutoka upande wa Italia. Wapandaji hao wa kwanza hawakuwa na vifaa vya kisasa. Walitumia tu vyombo vilivyo na ncha yenye chuma. Wakati huo, “ili kufika kilele cha mlima walihitaji kupanda kuanzia ndani ya bonde wakifuata njia zisizojulikana kabisa, na hivyo walihitaji kuwa wenye nguvu na ujasiri mambo ambayo huenda ikawa vigumu kwa wale wanaopanda milima leo kuwazia,” anasema mwanajiografia Giotto Dainelli. Hata vilele ambavyo vilionekana kuwa haviwezi kufikiwa, leo vimeweza kufikiwa mara kadhaa.
Hapo kale, mlima Mont Blanc ulionekana kuwa eneo lisilojulikana, ingawa uko katikati ya bara la Ulaya. Hati ya kwanza kutaja kuhusu mlima huo, iliandikwa mnamo 1088 W.K. Ramani ya watawa wa Benedict wa Chamonix inauita mlima huo rupes alba, ikimaanisha “mlima mweupe.” Hata hivyo, kwa miaka mingi wenyeji wa eneo hilo waliuita Mlima Uliolaaniwa kwa sababu ilisemekana kuwa
mashetani na majoka makubwa yaliishi kwenye mlima huo. Huenda jina Mont Blanc lilionekana kwenye mchoro kwa mara ya kwanza mnamo 1744, na hiyo ilikuwa ishara ya kwamba watu wataacha kuuona mlima huo kuwa umelaaniwa.Mambo Mbalimbali ya Milima Hiyo
Unaweza tu kuona vilele vya milima yote inayofanyiza Mont Blanc ukiwa ndani ya ndege. Milima hiyo ina ukubwa wa kilomita 600 za mraba, bonde lenye urefu wa kilomita 50 linalogawanya Italia, Ufaransa, na Uswisi, na pia vilele kadhaa vyenye urefu unaopita mita 4,000. Milima hiyo imefanyizwa kwa fuwele na mawe ya matale yanayotokezwa kwenye tabaka la juu la dunia. Wanajiolojia wanasema kuwa safu hizo za milima hazikutokea zamani sana, zilitokea miaka milioni 350 “tu” iliyopita. Hali ya hewa na barafu imebadili muundo wa milima hiyo na
kuifanya iwe na nyufa, mabonde yaliyochanika-chanika ovyoovyo, na vilele vinavyopendeza na kuwavutia wapanda mlima.Kutazama Mont Blanc kwa Ukaribu Zaidi
Hata wale ambao hawana ujuzi wa kupanda mlima, wanaweza kutazama safu hizo za milima kwa ukaribu wakitumia gari linaloning’inia kwa nyaya, lililoanza kutumiwa mwaka wa 1958. Kilele cha juu zaidi ambacho gari hilo hufika ni kile kinachoitwa Aiguille du Midi, kilicho na urefu wa mita 3,842 juu ya usawa wa bahari ambapo watu wanaweza kutazama mandhari yenye kustaajabisha ya Bonde la Chamonix.
Leo, sehemu zote za Mont Blanc zinajulikana vizuri sana. Wakati wa mapambazuko na wa machweo, miale ya jua inapoipiga miamba ya milima hiyo inatokeza mchanganyiko wa rangi nyekundu na kufanya miamba ya matale ionekane kama moto unaowaka.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]
Barabara ya Chini ya Ardhi ya Mont Blanc—Ndoto Yatimia
“Ninaona mabonde mawili ambapo lugha ileile inazungumzwa na ambapo watu hawana ubaguzi. Siku itakuja ambapo barabara itajengwa chini ya Mont Blanc na mabonde hayo mawili yataunganishwa.” Karne mbili zilipita kabla ya ndoto hiyo ya Horace-Bénédict de Saussure kutimia. Mnamo 1814 ombi la kwanza lilitumwa kwa mfalme wa Piedmont na Sardinia; hata hivyo, kazi ilianza mnamo 1959 na ikakamilishwa mnamo 1965. * Barabara hiyo ya chini ya ardhi, yenye urefu wa kilomita 11.6, inaanzia upande wa Italia mita 1,381 juu ya usawa wa bahari na kutokea upande wa Ufaransa mita 1,274 juu ya usawa wa bahari.
Machi 24, 1999, lori fulani lilishika moto ndani ya barabara hiyo ya chini ya ardhi na kusababisha msiba. Joto lilipanda na kufikia nyuzi 1,000 Selsiasi na kuyeyusha magari mengi. Watu 39 walikufa kwa sababu ya kukosa hewa na watu 30 zaidi wakajeruhiwa. Baada ya uchunguzi wa mwaka mzima, kazi ya ujenzi ilianza tena. Barabara hiyo ilifunguliwa tena Juni 25, 2002, licha ya malalamiko kutoka kwa wanamazingira na wakazi wa eneo hilo wanaosema kwamba malori mengi makubwa yanayopitia humo yanasababisha uchafuzi. Hivi karibuni, katika muda wa miezi minne magari 132,474 yalipitia kwenye barabara hiyo ya chini ya ardhi.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 12 Kwa habari zaidi ona gazeti Amkeni! la Kiingereza la Februari 8, 1963 (8/2/1963), ukurasa wa 16-19.
[Picha]
Nguzo ya H. B. de Saussure, huko Chamonix, Ufaransa
[Hisani]
Library of Congress, Prints & Photographs Division, Photochrom Collection, LC-DIG-ppmsc-04985
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24, 25]
KULIZUNGUKA “JITU”
Ingawa wataalamu wa kupanda milima ndio tu wanaoweza kufika kwenye vilele vya Mont Blanc, hata wale ambao hawajawahi kupanda hadi sehemu za juu wanaweza kufurahia mandhari hizo kwa kuuzunguka. Kwa kawaida, picha nzuri zaidi za mlima huo si zile zinazopigwa kutoka kileleni, bali ni zile zinazopigwa kutoka mbali. Mont Blanc umezungukwa na vituo mbalimbali ambavyo watu wanaweza kutazama mandhari ya mlima huo kwa njia nzuri. Watu wanaopenda vitu vya asili na wanaoweza kutembea bila matatizo wanaweza kupitia kwenye vijia vya milima hiyo vilivyo na urefu wa kilomita 130 hivi. Matembezi ya Mont Blanc yaliyoanzishwa kwa kuunganisha baadhi ya vijia hivyo hupitia Ufaransa, Italia, na Uswisi. Matembezi hayo yanayochukua saa tatu hadi saba kila siku yamegawanywa katika vituo kumi na yanakuwezesha kutazama mandhari mbalimbali zenye kuvutia sana. Watu ambao hawana wakati mwingi wanaweza kutembelea mlima mmoja tu kati ya milima hiyo.
[Picha]
Aiguille du Midi ndiyo sehemu ya juu zaidi inayoweza kufikiwa kwa gari linaloning’inia
[Hisani]
Courtesy Michel Caplain; http://geo.hmg.inpg.fr/mto/jpegs/020726/L/12.jpg
[Ramani katika ukurasa wa 22]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
UFARANSA
USWISI
ITALIA
Mont Blanc
[Picha katika ukurasa wa 22]
Saussure akipanda Mont Blanc mnamo 1787 (mchoro wa msanii)
[Hisani]
© The Bridgeman Art Library International
[Picha katika ukurasa wa 23]
Mont Blanc